Magoli ya Aymen Mahious kipindi cha kwanza na Islam Merili kipindi cha pili ndiyo yaliyowatonesha Watanzania kidonda cha mwaka 1993, Simba ilipofungwa 0-2 na Stella Abidjan ya Ivory Coast katika fainali ya michuano hiyo wakati huo ikiitwa Kombe la CAF.
Michuano hiyo ilibadilishwa jina na kuwa Kombe la Shirikisho mwaka 2004. Mechi ilichezwa Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru) baada ya mchezo wa kwanza ugenini Simba kulazimisha suluhu.
Rekodi za Yanga msimu hizo ndizo zinazotoa matumini 'haijaisha' kwa kuwa. Sasa itatakiwa 'kupindua meza' ugenini watakaporudiana Juni 3 katika mechi ya pili fainali.
Mshambuliaji Fiston Mayele aliwarudisha mashabiki wa Yanga katika shangwe dakika ya 82 baada ya kusawazisha kwa bao la ajabu, akipokea pasi ya kichwa ndani ya eneo la boksi kutoka kwa Mudadhir Yahaya. Kwa utulivu mkubwa, aliutuliza mpira kisha kuachia shuti kali la mguu wa kulia, kimo cha kuku.
Ni goli lililoamsha matumaini kwa wanajangwani waliokuwa na huzuni baada ya kutanguliwa kufungwa kwa bao la kichwa la Mahious dakika moja baada ya nusu saa ya mchezo. Lilitokana na mpira wa adhabu ndogo baada ya Brahim Benzaza kuangushwa pembeni mwa lango la Yanga.
Hata hivyo, furaha ya watoto wa Jangwani ilidumu kwa dakika mbili tu huku mvua nayo ikiwaongeza uchungu baada ya mshambuliaji Islam Merili kuipatia USM Alger bao la pili na la ushindi. Wageni walianza vizuri ndani ya boksi la Yanga.
Mfungaji hakuwa amezongwa na mshambuliaji yeyote wa Yanga alipopokea pasi murua kutoka kwa Khaled Bousseliou. Akamtungua kipa Djigui Diarra.
Katika robo saa ya kwanza ya mchezo, Yanga ilifanya shambulizi kali, Mayele na Kennedy Musonda walipowatoka mabeki wa USM ALger na kumpa pasi ya upendo Tuisila Kisinda aliyekuwa amebaki na kipa Oussama Benbot lakini akapiga shuti mtoto lililoishia mikononi mwa kipa huyo.
Mfungaji wa bao la kwanza, Mahious, pia alikaribia kufunga la pili dakika tano kabla ya saa ya mchezo baada ya kuupata mpira pembeni kidogo mwa boksi, akawalamba chenga mabeki wa Yanga kabla ya kupiga shuti kwa mguu wa kushoto, lakini Diarra akafuta makosa ya mabeki wake.
Ni shambulizi lililojibiwa na Yanga dakika moja baadaye, Kisinda alipoambaa na mpira akipita winga ya kulia na kumpasia Stephane Aziz Ki ambaye alipiga shuti lilitoka nje kidogo na kugusa nyavu.
Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi alifanya mabadiliko ya mkupuo, kwa kuwaingiza Bernard Morrison, Joyce Lomalisa na Djuma Shaaban na baadaye akamwingiza Clement Mzize na kuipa nguvu timu kwa kiasi kikubwa kusukuma mashambulizi langoni mwa USM Alger.
Bao la Mayele ni la saba kwake katika michuano hiyo na anaongoza akiwa na nafasi kubwa ya kuibuka kuwa mfungaji bora katika michuano hiyo msimu huu.
VURUGU, KIFO
Kabla ya mechi hiyo kuanza, kulikuwa na vurugu za mashabiki waliolazimisha kuingia uwanjani, baadhi wakiruka ukuta wa uzio wa Uwanja wa Mkapa. Polisi walilazimika kutumia nguvu kuwadhibiti.
Milango ya uwanja huo ilifunguliwa saa tano asubuhi lakini wakati huo tayari kulikuwa na kundi kubwa la mashabiki waliokuwa wanasubiri kuingia.
Wingi wa mashabiki ulisababisha mashabiki hao kuvunja mageti mawili ya uwanja kutokana na wahusika kuchelewa kuyafungua huku askari wakishindwa kuwadhibiti kutokana na wingi huo.
Hadi kufikia saa 6:30 mchana, eneo la nje ya uwanja huo lilikuwa limeshafurika mashabiki waliokuwa wamevaa jezi za rangi ya kijana na njano.
Ndani ya uwanja huo kulikuwa 'ntiti'. Hadi kufikia saa nane mchana, tayari mashabiki walishapendezesha eneo kubwa la uwanja huku nje kukiwa na idadi kubwa ya mashabiki ambao nao walikuwa katika harakati za kuingia.
Jana jioni, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, alitoa alichokiita taarifa za awali kuhusu majeruhi wa vurugu hizo. Alibainisha kuwa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Temeke ilikuwa imepokea majeruhi 30, huku mmoja akifariki dunia.
Alifafanua kuwa aliyefariki dunia ni mwanamume mwenye umri unaokadiriwa miaka 40. Alisema "...majeruhi wengi wanaendelea vizuri. Wana majeraha madogo madogo. Wanaendelea na vipimo."
Ummy alisema kuwa timu kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ilikuwa uwanjani, ikifuatilia kwa karibu kuangalia kama kulikuwa na majeruhi wengine.
Pia timu ya wataalamu wa huduma za dharura ya Hospitali ya Rufani ya Taifa Muhimbili (MNH) iliwasiliana na Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Temeke na ilikuwa tayari kuwapokea na kutoa huduma kwa majeruhi wanaohitaji matibabu zaidi.










