Kikosi cha Yanga kinatarajia kuondoka nchini kesho kuelekea Algers kukabiliana na USM Algers kwenye mchezo wa pili wa fainali ya kombe la Shirikisho Afrika.
Taarifa ambazo Nipashe Digital imezipata kutoka ndani ya uongozi wa Yanga, tayari wametuma watu mapema nchini humo ambao watahakikisha wanaikwepesha timu na hujuma zote.
Yanga wanatarajia kuondoka nchini kesho na ndege waliyopewa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan ambayo itakaa kuwasubiri baada ya mechi kuwarudisha nchini.
“Mambo yanaenda vizuri kuelekea mchezo wetu wa marudiano, tumejipanga kukwepa hujuma zozote wanazoeweza kutufanyia wapinzani wetu, huu mpira wa Afrika una mambo mengi hivyo tumejipanga,” alisema mmoja wa viongozi wa klabu hiyo.
Kwenye mchezo huo wa marudiano, Yanga inahitaji ushindi wa kuanzia mabao 2-0 kuweza kutwaa ubingwa huo. Hii ni kutokana na kufungwa mabao 2-1 nyumbani kwenye mchezo wa kwanza.










