Uamuzi huo wa Wekundu wa Msimbazi unalenga kuimarisha kikosi chao kuelekea msimu ujao wa mashindano kwa ajili ya kufanya usajili wa wachezaji wenye viwango bora.
Akizungumza na Nipashe jana, Ofisa Mtandaji Mkuu wa Simba, Imani Kajula, alisema eneo la skauti ya wachezaji ni muhimu ingawa lilikuwa haipewi nafasi kubwa miaka ya nyuma na klabu yao imeamua kwenda kisasa kwa kumwajiri Mels.
Kajula alisema mtaalum huyo atashirikiana vizuri na Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliviera 'Robertinho' katika kufanya usajili kulingana na 'mapinduzi' anayotaka kuyafanya mwalimu huyo.
"Tunafuraha kubwa kumkaribisha Mels ili kuja kuboresha ufanisi kwenye Skauti kwa sababu ni eneo muhimu katika mafanikio ya klabu yetu.
Tunaendelea na maboresho muhimu kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano ya kimataifa," alisema Kajula.
Wakati huo huo taarifa zaidi kutoka Simba zinasema wanajipanga kuibomoa Vipers kwa kuwanasa waliokuwa wasaidizi wa Robertinho alipokuwa akiifundisha klabu hiyo ya Uganda.
Katika hatua nyingine, hatima ya kiungo, Hassan Dilunga, ambaye amerejea kwenye mazoezi ya kikosi cha Simba bado haijajulikana.
Dilunga ambaye aliwahi kuonekana akifanya mazoezi na JKT Tanzania iliyorejea kwenye Ligi Kuu Bara, anawindwa pia na Mtibwa Sugar.
Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema mchezaji huyo alikuwa chini ya uangalizi wa madaktari na makocha kwa miezi miwili kwa ajili ya kumwangalia utimamu wake wa mwili pamoja na maeneo ya majereha yake.
Alisema Simba ilikosa moja ya wachezaji wa aina ya Dilunga msimu huu ambaye ana uwezo wa kucheza kama winga, kiungo mzuiaji, kiungo wa kati na hata namba 10, hivyo kama atakuwa na kiwango chake kile kile basi atakuwa msaada mkubwa kwenye kikosi.










