Membe ambaye alipozaliwa katika Kijiji cha Chiponda-Rondo, hakuna aliyejua kuwa alikuwa na maono makubwa kwenye siasa, amekuwa Naibu na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa katika awamu ya Rais Jakaya Kikwete, kuanzia 2005 hadi 2015.
Amefariki Ijumaa Mei 12, muda mfupi baada ya kuugua ‘nyumonia’ kali na kulazwa katika hospitali ya Kairuki jijini Dar es Salaam. Kifo chake kimekuja kipindi kifupi baada ya kurejea CCM, akijiondoa tena ACT-Wazalendo, aliyojiunga nayo 2020 na kuwa mshauri mkuu wa chama na baadaye kuwa mgombea urais kupitia chama hicho akipambana na mgombea wa CCM, John Magufuli.
Waziri Membe alisifika kwa upole, akizungumza au kuongea kwa sauti ya utulivu, yenye unyenyekevu na muda wote, alikuwa akitabasamu na kuwasiliana na kila mmoja awe mzee au kijana kwa taratibu na utaratibu.
Ni jambo linalodhihirisha kuwa hakuwa au hakupenda kufoka wala kukemea, lakini akifanya kila kitu katika utumishi wa umma kwa kuheshimu, kuthamini na kushirikiana na kila mmoja, huku akisikiliza kwa moyo kila aliyewasiliana naye.
Anastahili sifa kwa kulitumikia taifa kwa heshima kuu, lakini pia kuwa mwanadiplomasia aliyeishi muda mrefu katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Nchi.
Mwanadiplomasia huyu ni msomi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Johns Hopkins University huko Marekani, hatasahaulika na wapigakura wake wanajimbo lake la Mtama mkoani Lindi, aliowatumika kwa miaka 10.
MWANADIPLOMASIA WA AFRIKA
Waziri wa zamani Membe ameacha alama Afrika hasa kutafuta ufumbuzi wa migogoro ya Maziwa Makuu mathalani ule wa DRC, ni juhudi ambazo hazitasahaulika barani humo.
Aliamini kuwa DRC mzozo wake, siyo tu kuwa una vipimo na athari za kikanda na kuvuka mipaka, lakini pia ulihitaji juhudi za kikanda katika kuutatua kwa njia endelevu na za kidiplomasia.
Katika uhai wake aliamini na kufanyakazi usiku na mchana kupata suluhu ya mgogoro wa DRC akisema ni taifa linalopakana na nchi tisa za Afrika za Angola, Burundi, Rwanda, Uganda, Jamhuri ya Congo, Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), Sudan Kusini, Tanzania na Zambia.
Katika juhudi zake alifanyakazi kubwa kumaliza mizozo ya Maziwa Makuu na wa DRC, hasa akisema kukosekana utulivu , kuna hatari nyingi kwa nchi jirani na ukanda mzima wa kusini, mashariki na hata Afrika ya Kati na kungeleta matokeo mabaya kwa watu kuishi katika migogoro isiyokwisha.
HAKUWA MWOGA
Wakati wa uongozi wa Magufuli Membe hakutaka kukaa kimya na kuzibwa mdomo, licha ya kuwa mwana CCM kindakindaki na pia shushushu, alikuwa akitoa sauti ya kukosoa serikali ya JPM jambo lililokatisha uanachama wake ndani ya chama hicho.
Alikuwa hana hofu na kile alichokizungumza na wakati mwingine alizungumza na vyombo vya habari vya kimataifa, akisifia kazi ya JPM hata hivyo akikosoa na kueleza kuwa kuna baadhi ya mambo yalipaswa kurekebishwa.
Historia ndani ya CCM, inaonyesha kuwa Februari 2020, ulikuwa ni mwanzo mgumu kwa Membe ndani ya chama kilichomlea, kumkuza na kufanikisha kung’ara kwa nyota yake kitaifa na kimataifa.
Mwaka unaanza kwa kukabiliana uso kwa uso na chama chake –CCM ambacho kilimfukuza uanachama. Ni maamuzi ya Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, iliyokuwa chini ya Mwenyekiti John Magufuli, iliyomuweka pembeni, akidaiwa kuwa ni kutokana na matendo yake yasiyokuwa na maadili.
Ilipotimu Mei 29, 2022 mwaka mmoja uliopita, mgombea urais wa ACT Wazalendo, Bernard Membe alirudishiwa kadi yake ya uanachama wa CCM, baada ya kufukuzwa.
Baada ya kutimuliwa Februari 2020, hakuwa na papara ila alinyamaa kwa miezi kadhaa na ilipofika Julai alitoa ya moyoni japo hakumaliza kila kitu.
Ni pale Membe anapotangaza rasmi mbele ya jamaa zake wakazi wa nyumbani kwao huko kijijini Rondo, kuwa atagombea urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020.
Hata hivyo, aliwaachia maswali mengi , hakutangaza wazi wazi kuwa atagombea kupitia chama gani ila wapo waliokuwa wanaeleza kuwa atajiunga na chama cha ACT Wazalendo, kwa kuwa CHADEMA tayari Tundu Lissu, alikuwa ameshaweka wazi msimamo wake kuwa anapambana na Magufuli kuwania uongozi wa Tanzania.
Kwa ujumla alikuwa ngangari na asiyeogopa kuvunjwa mwiko. Japo si vibaya kwa mujibu wa katiba ya CCM lakini ni kama Membe alitaka kwenda kinyume na mazoea kwa kuanzisha upinzani wa ndani ya chama kwenye kugombea urais wakati chama kimeweka mazingira ya aliyekuwapo madarakani kugombea bila kupingwa kwenye muhula wa pili wa miaka mitano ya kumalizia ngwe ya uongozi wake.
Baada ya uchaguzi, alibaki kimya hadi aliporudishwa tena ndani ya CCM na Katibu wa Itikadi na Uenezi Taifa wakati huo, Shaka Hamdu Shaka, aliyefika nyumbani kwao katika Kijiji cha Chiponda- Rondo kumpokea tena.
Mwenezi wa CCM Shaka, alisema anarudishwa kundini baada ya Membe kuomba msamaha, lakini naye hakufanya ajizi akijibu kuwa hakuwa tena na sababu za kumzuia kuwa mwanachama wa CCM, bila kufafanua kwa kina.
Lakini ujumbe ukafika na kila mmoja akaelewa kama alivyojaliwa na ufahamu wake, kwa vile wengi walihusisha kutimuliwa kwake na kuonyesha nia ya kugombea urais, wakati wa uongozi wa Rais JPM, akimaanisha kuchuana na mwanaCCM aliye madarakani.
Kutikiswa kwa Membe kwenye siasa kunakohusishwa na kukosa maadili hadi kufa kwake hakukueleza bayana ni makosa gani ambayo anatuhumiwa kuyafanya , wakati huo akituhumiwa pamoja na makada ambao ni pamoja na makatibu wakuu wastaafu, Yusufu Makamba na Abdulrahman Kinana.
Hayati Membe aliyezikwa jana kijijini kwake, alizaliwa Novemba 9, 1953 na taratibu baada ya miaka kadhaa ya utumishi aling’ara zaidi kuanzia 2005, aliposhinda kiti cha ubunge wa jimbo la Mtama.










