Dawa uwepo sheria kutenga maslahi binafsi, kazi za umma

17May 2023
Faustine Feliciane
DAR ES SALAAM
Nipashe
Dawa uwepo sheria kutenga maslahi binafsi, kazi za umma

RIPOTI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), inaonyesha utafunaji wa fedha za serikali ambao chanzo au chimbuko linahusishwa na kutozingatia maslahi ya taifa kwa baadhi ya watunga sera na wafanya maamuzi.

Ujenzi wa miradi duni ni matokeo ya viongozi na watendaji kuwa na maslahi kwenye maamuzi na mkono ndani ya utekelezaji. PICHA: MTANDAO

Badala ya kujali Tanzania yenye neema wanawekeza kwenye maslahi binafsi hata kusababisha utekelezaji wa miradi au shughuli za umma kuwa na ufanisi duni.

Mazoea hayo huleta malalamiko mengi kutoka kwa wananchi ambao ndiyo walengwa wakuu. Katika makala iliyotangulia ilimalizika kwa mfano wa kukarabati ofisi ya Mkuu wa Wilaya kwa kutumia fedha kidogo alizopata kutoka serikali kuu lakini hakuwa tayari kufafanua zaidi.

Hata hivyo, baada ya kupitia wilaya na halmashauri kadhaa kilichogundulika ni kwamba fedha zinatolewa lakini matumizi yake, kwa kiasi kikubwa, yalikuwa hayaendani na malengo ya kile kilichokusudiwa au kupangwa.

Kimsingi, hali kama hiyo matokeo yake ni kushuhudia ‘madudu’ mengi kama zilivyobainisha Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya Serikali na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU).

Hali ilivyo suala la kuzuia rushwa nchini bado halijawa shwari ndiyo maana katika harakati za kupambana na kutoa na kupokea mlungula ubadhirifu wa fedha za umma unajitokeza mara-kwa mara.

Kichocheo kwa hayo yote, kinatokana na ‘uhuru au ruksa’ waliyonayo viongozi wakuu wa serikali kushiriki masuala ya biashara na kunufaika wao na jamaa zao.

Tunaweza kusema hiki ni kikundi cha watu wachache walioshikilia usukani serikalini na hapohapo wanayo maslahi binafsi kupitia milango mbalimbali ya kibiashara.

Inakuwepo dira au maono ya kitaifa yanayotakiwa kutekelezwa na serikali kuu na serikali za mitaa na katika michakato ya kuweka mikakati kutekeleza malengo, ndipo ‘kujipenda’ zaidi kwa baadhi ya wahusika serikalini kunapoanzia.

Fedha zipo, mipango ya kuzitumia kutekeleza malengo yanayokusudiwa ipo changamoto inakuja, ‘mimi mhusika nitanufaika vipi’?

Kwakuwa wahusika wanazo nguvu za kisera na uwezo wa kufanya maamuzi papo kwa hapo wanao ‘uhuru fulani’ unawampa mwanya kuhusika na maslahi binafsi hivyo wanajitahidi kadri wawezavyo kupindisha mambo kwa faida binafsi.

 Kuna usemi fedha ni sabuni ya roho, tutajiuliza kivipi? Sina jibu wakati huo kwamba nyakati hizi ibilisi amejikita katika fedha hivyo kugeuza akili za wengi.

Hivyo, kuwa na madaraka serikali yanapochanganyika na roho za kupenda fedha sana’ kuliko maslahi ya taifa dira au maono na mipango ya kitaifa pamoja na utekelezaji wake vinabaki zaidi kwenye makabrasha na au nadharia  kuliko kivitendo.

 

KUDHARUA UMMA

Maono binafsi yanapewa kipaumbele zaidi kuliko ya kitaifa. Kwa msingi huo viongozi wengi na watendaji serikalini wapo lakini hawabebi moja-kwa-moja dira auaono ya taifa kama timu moja badala yake mwelekeo na kutii haja  binafsi unadhoofisha taifa. Katika mazingira kama hayo, kwa vyovyote vile, fedha zilizolenga kukidhi malengo ya kitaifa ‘zitaelekezwa yalipo maslahi binafsi’.

Kumbuka usemi ‘hazina ya mtu ilipo ndiko na roho yake ilipo’ hivyo, yaliyo katika nafsi ya mhusika, ndiyo yanayopewa kipaumbele zaidi kuliko mengineyo.

Aidha, hali hiyo inaashiria ukosefu wa uzalendo kwa baadhi ya Watanzania na kusababisha kukosekana umoja imara kitaifa hivyo kuzorotesha utekelezaji maono, mipango ya kitaifa. Ndiko kuwapo  watendaji kuvutia kwao na kuchukua chao mapema.

 

UMOJA KITAIFA

Dhana ya kujenga umoja wa kitaifa ulio imara siyo tu katika demokrasia na siasa pekee bali pia katika utendaji, serikali kuu na  zile za mitaa.

Wakati huohuo, viongozi warejee kwenye misingi ya utawala imara kwa kuzingatia kanuni muhimu ikiwa ni pamoja na kutenganisha shughuli za kibiashara na watendaji serikalini.

Kanuni aliyokuwa nayo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere irejeshwe. Siyo dhambi kukiri kwamba kuna kukosea sasa ni kujirekebisha itakuwa jambo la kheri kuliko shari.

 Kwa mataifa yaliyoendelea kama Marekani au barani  la Ulaya, suala la biashara kwa watendaji serikalini ni kitu cha kawaida kutokana na wahusika kutenganisha maslahi binafsi na shughuli za umma.

Lakini kwa mataifa yanayoinukia kiuchumi ni majanga matupu kama ripoti za CAG na TAKUKURU zinavyobainisha kila mwaka.

Zinahitajika juhudi kubwa kujenga timu za kitaifa na watendaji wazalendo, watumishi wenye uchungu na nchi yetu na wenye maslahi kwa taifa na Watanzania wote, mijini na vijijini.

 Dhana hii maana yake ni uwepo wa timu za kitaifa zenye dira na maono mapana kwa taifa  yaliyoandikwa kwenye nafsi na mioyoni mwao. Kuanzia mkubwa aliye juu kimadaraka,  hadi mtendaji wa chini akiwa ni mhudumu ofisini,  kwa mnyororo wote, lao liwe moja kuhakikisha vya taifa vinatekelezwa bila kuchechemea na mafanikio yaonekake kama ilivyokusudiwa.

 Vilevile, kuwepo na mikakati thabiti ya kuzuia au kugundua ubadhirifu na kuepusha matumizi mabaya ya fedha na rasilimali za umma, mapema na si kungojea mwaka uishe ni hasara kubwa.

Mazoea ni kuona ripoti za CAG au kuiagiza TAKUKURU kufanya uchunguzi wakati mambo yameishaharibika. Ndani ya wizara, taasisi za serikali, mashirika na mawakala wake.

Idara ya wakaguzi wa ndani iongezewe nguvu ili iweze kufuatilia kwa ukaribu kinachofanyika wakati wa michakato ya manunuzi au matumizi mengine ya fedha za umma.

Kadhalika, kungekuwepo na jicho la ndani kunusa harufu ya rushwa au ubadhirifu na kuarifu mamlaka mapema kabla malipo au wizi haujatekelezwa.

Hivyo, kufanya mamlaka kuchukua hatua haraka mambo yasitetereke na wahusika kufikishwa mbele ya sheria au uongozi ipasavyo.

 

MASHIRIKA YA UMMA

Kuna mashirika kulingana na ripoti ya CAG yanapata hasara.

 Sawa matarajio ni kutengeneza faida lakini kabla ya kukimbilia kuyafuta, uchunguzi wa kina ufanyike kujiridhisha kiini cha kupata hasara kijulikane bayana ili makosa kama hayo yasirudiwe.

Itakapogundulika kuwa kumekuwepo uzembe na ubadhirifu au wizi ama udanganyifu katika utekelezaji wa majukumu hatua zichikuliwe kwa waliohusika na  kusababisha hasara.

Watakaobainika kuhusika na hasara au wizi ama rushwa hatua kali za kisheria zichukuliwe pamoja na kuwafilisi ili kilichopotea kirejeshwe.

Sheria ziwe kali sana ili kusiwepo mianya ya mahakama kuwaonea huruma ili mradi-mhusika avune alichokipanda.

Kama ni wema kwa watanzania atavuna mema,  lakini ukiwa ubadhirifu avune adhabu kali vilevile, kuwepo umakini katika harakati za kuyafuta mashirika yaliyobeba alama za kitaifa.

Watendaji wanaosababisha hasara kwa uzembe wajione kuwa wanajiweka kitanzi wenyewe na wasionewe haya wala huruma. Ukitaka kumuanganiza nyani usimwangalie usoni atajifanya analialia umwonee huruma wakati ni mharibifu.

Ni aibu kubwa kwa baadhi  kushindwa kusimamia shughuli za kitaifa kikamilifu na kwa weledi na kwa maslahi ya taifa .

Ripoti za CAG na TAKUKURU, ifike mahali ziwe ni za kupongeza zaidi kuliko hali ilivyo sasa. Hakuna lisilowezekana taifa, serikali na Watanzania wachukue hatua stahiki kurekebisha uovu kwa faida ya  wote.