NEMC yaja na meno kamili kutafuna wabishi wanaopiga kelele mitaani

04May 2023
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
NEMC yaja na meno kamili kutafuna wabishi wanaopiga kelele mitaani

HIVI karibuni Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), lilitangaza mwezi huu linaanza operesheni kudhibiti kelele, ili kulinda afya za wananchi.

Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk. Samuel Gwamaka, anasema afya za watu wengi zinaathirika kwa kelele chafuzi zinazotokana na vyanzo mbalimbali.

Anatoa tafsiri ya Sheria ya Mazingira 2004, kwamba:“Kelele ni kila uchafuzi usababishwao na sauti ambayo kwa asili inakataliwa au ile iwezayo kusababisha athari mbaya kwa afya ya binadamu, maisha au mazingira; pia ni pamoja na sauti iwezayo kubainishwa na Kamati ya Taifa ya Viwango vya Mazingira.”

Dk. Gwamaka anazitaja kuwa shughuli za kibinadamu zinasababisha kelele chafuzi na mitetemo, utafiti ukionyesha vyanzo vyake unajumuisha mitetemo,  pamoja na ujenzi, nyumba au kumbi za starehe, viwanda, nyumba za ibada, vyombo vya usafiri na magari ya matangazo.

Anaeleza athari za wazi za ni kuhatarisha afya, mfano kukosesha wagonjwa muda wa kupumzika au wanafunzi muda wanapokosa muda wa kusoma, pia inaharibu mahusiano ya kijamii.

NAMNA YA KUZUIA

 

Meneja wa Ufuatiliaji wa Sheria wa NEMC, Ndimbumi Joramu, anatamka kifungu cha Sheria ya Mazingira, 2004: “Si ruhusa kwa mtu yeyote kupiga kelele au kusababisha kupiga kelele kuzidi kiwango kilichoainishwa au kitakachobainishwa kuhusiana na upigaji kelele… Litakuwa ni kosa kwa mtu yeyote kumwaga uchafu au kupiga kelele bila kuzingatia njia iliyobainishwa kuwa ni bora katika kanuni zinazoweza kutungwa na waziri.”

Anasema katika kudhibiti kelele chafuzi, waziri mwenye dhamana ya mazingira kupitia Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, ametunga Kanuni za Usimamizi wa Mazingira za Viwango vya Udhibiti wa Kelele na Mitetemo za Mwaka 2015.

Joramu anasema, NEMC inanuia kuhakikisha ulinzi wa afya ya binadamu na mazingira kwa kudhibiti viwango vya kelele na mitetemo kutoka vyanzo mbalimbali. Anafafanua hatua zingine: “Kubainisha viwango vya juu vya kelele vinavyoruhusiwa kutoka katika shughuli mbalimbali, kuweka udhibiti wa kelele na mitetemo na namna bora ya kuzuia athari zinazoweza kujitokeza.”

VIWANGO VINAVYORUHUSIWA

Mwanasheria huyo anataja kanuni za viwango vya kelele na mitetemo vilivyoruhusiwa na vinavyoweza kuvumilika kwa nyakati za mchana na usiku kwamba: “Viwango vya sauti vilivyoruhusiwa katika maeneo ya burudani, nyakati za mchana zinaanzia saa 12.00 asubuhi hadi saa 4.00 usiku. Viwango vya sauti vilivyoruhusiwa ni desibeli 60 katika makazi ya watu, 75 katika maeneo ya biashara na 85 katika maeneo ya viwanda.”

Pia, anasema kuanzia saa 4.00 usiku hadi saa 12.00 asubuhi, viwango vya sauti vilivyoruhusiwa kwa nyakati hizo ni desibeli 40 katika makazi ya watu, 50 katika maeneo ya biashara na 65 viwandani.

Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria ya Mazingira NEMC, Mhandisi Redempta Samuel, anataja kanuni inayotoa katazo la ujumla dhidi ya kelele chafunzi kwa yoyote hataruhusiwa kupiga au kusababisha kelele zilizo kubwa na zisizo na ulazima, au zisizo za kawaida na zinakera, kuleta usumbufu au kusababisha madhara katika afya na usalama wa watu ama mazingira.

“Kanuni ya 7(2) imeainisha mambo muhimu ya kuzingatia ili kujua au kupima kama sauti inayotoka imezidi au haijazidi kiwango kinachotakiwa; mambo hayo ni pamoja na muda (mchana au usiku), ukaribu na makazi ya watu, na ukaribu na hospitali au shule,” anasema.

Hata hivyo, anasema wajibu wa mmiliki wa miundombinu wanaelekezwa na kanuni husika, wajibu wa mmiliki wa miundombinu au mtambo, ikiwamo vifaa vya muziki wanapaswa kuwa na kifaa cha kupima sauti, ambacho kinafaa kuwekwa katika miundombinu na ni kosa la kisheria kutokuwa nacho.

Pia, kunatajwa mamlaka za serikali za mitaa zina wajibu wa kusimamia utekelezaji Sheria ya Mazingira na kwa mujibu wa kanuni iliyopo, maofisa mazingira katika serikali za mitaa wamepewa mamlaka  kutoa amri za utekelezaji kwa mhusika yeyote.

Mkurugenzi huyo anasema, NEMC ina nafasi ya kuwatumia wakaguzi wa mazingira na maofisa mazingira katika halmashauri zote, kuwa na mamlaka ya kusimamia kanuni au kutoa amri mbalimbali, zikiwamo za kumzuia mtumiaji mtambo wa kutoa sauti inayokiuka viwango viliyoainishwa.

FAINI NA ADHABU

Redemta anataja mamlaka ya NEMC, inaweza kumuamuru mkosaji kulipa faini ya fedha kisheria kwa kosa alilolitenda chini ya kanuni zilizopo kisheria. Anafafanua: “Mtu yeyote atakayekiuka matakwa ya kanuni hizi, anaweza kutozwa faini isiyopungua shilingi milioni mbili na isiyozidi shilingi milioni kumi au kifungo cha miaka miwili jela na kisichozidi miaka saba au vyote kwa pamoja.”

Anasema, NEMC imebaini tatizo la baadhi ya wamiliki kutokuwa na kifaa cha kupima kiwango cha sauti inayotoka, uelewa hafifu juu ya madhara yatokanayo na sauti na mitetemo, hata hawana ushirikiano mzuri na mamlaka nyingine zinazosimamia utekelezaji sheria.