Mkoa Geita waingia ubia na wachimbaji wakubwa kufukia mashimo, kupanda

04May 2023
Marco Maduhu
GEITA
Nipashe
Mkoa Geita waingia ubia na wachimbaji wakubwa kufukia mashimo, kupanda

WACHIMBAJI wadogo wa madini, ikiwamo dhahabu, sifa moja yao kuu inatajwa wanaharibu mazingira wawapo kazini, kwa sababu hawana vifaa maalumu kubaini uwapo wa madini katika eneo husika, hivyo wanachimba kwa kubashiri, hata wanaacha mashimo.

 

Ni hali inayotajwa kuchangia kuachwa mashimo, huku wakikata miti muhimu kwa kutunza mazingira. Katika kata ya Mgusu, Halmashauri ya Geita Mji, machimbo ya Nyamatagata, yaliyoanza Mei 20, mwaka jana, wachimbaji baada ya kusikia kuna madini, wanaelezwa wakapavamia na kuanza shughuli za uchimbaji, hata kusababisha uharibifu mkubwa wa mazingira.

Ofisa Mazingira wa Halmashauri ya Geita Mji, Bingile Washima, anasema serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwamo Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT), anasema wamekuwa wakijitahidi kuwapa elimu wachimbaji wadogo wachimbe bila ya kuathiri mazingira.

Tito Mlelwa, ni Ofisa Mazingira Mkoa wa Geita, anasema kwa kawaida wachimbaji wadogo wanafahamika kuwa waharibifu wa mazingira, lakini kwa machimbo ya Nyamatagata, kupitia wamiliki wa leseni, wamebadili mwenendo kurejea utunzaji mazingira, ikaianza na elimu sahihi kwa jamii husika.

Katika hilo, Ofisa Mtendaji wa Mtaa wa Manga, Kata ya Mgusu, ndani ya Halmashauri ya Geita Mji, Boniphace James, anasema  eneo ambalo shughuli za uchimbaji madini zinafanyika katika Machimbo ya Nyamatagata, kuna marufuku kwa mchimbaji kukata miti  na hata miti inayotumika hapo sasa, inatoka maeneo mengine ya nchi, ikwamo Bukoba, Tarime na Mbeya.

Anasema katika utunzaji mazingira mgodini, viongozi wanaoshirikiana na kampuni yenye leseni kama, Geita Resources, wanafukia mashimo maeneo yote ya ardhi, ambako kumeathiriwa, wakipanda miti, ikiwa ni jukumu endelevu, kuzuia uharibifu wa mazingira katika machimbo hayo.

Kamanda wa jeshi la jadi Sungusungu katika machimbo hayo, Mathias Mwita, anasema wamekuwa wakifanya doria za kila mara kudhibiti uharibifu wa mazingira, ikiwamo ukataji miti na wanaofanya makosa huchukuliwa za kisheria.

“Watu ambao tunawakamata wakichafua mazingira huwa tunawatoza faini kuanzia shilingi 2,000 hadi 5,000, wale wanaokata miti faini zao zipo juu kuanzia shilingi 50,000 na kuendelea,” anasema Kamanda huyo Sungusungu.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mgusu, Halmashauri ya Geita Mji, Elias Galila, anasema wakati machimbo hayo yanaanza mwaka jana, hali mahali hapo ilikuwa mbaya, kwa sababu ya kuwapo idadi kubwa ya wakazi, wastani tu 20,000.

Anaeleza hatua walizochukua ni kuwakamisha jukumu la kufukia mashimo wamiliki wa leseni, ikiwamo kampuni ya Geita Resources, pia wakapanda miti maeneo hayo, huku viongozi wa eneo hilo wakitumia sheria za usimamizi mazingira kupadhibiti.

“Kihistoria eneo hilo lilikuwa na miti sana ya asili, lakini baada ya shughuli za uchimbaji madini kuanza, miti ya asili ilikatwa, na sisi tumewekeana sheria zetu marufuku kukata miti ambayo imesalia, bali wachimbaji wanunue miti kutoka maeneo mengine,” anasema Kamanda wa Sungusungu, Mwita.

UONGOZI MKOA

Mkuu wa Wilaya ya Geita, Cornel Magembe, anasema asilimia 70 ya wananchi mkoani Geita wanajishughulisha na uchimbaji madini na anataka uchimbaji huo uendane na utunzaji mazingira kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004, ambazo zinasisitiza utunzaji mazingira.

“Tunataka uchimbaji wa nadini hapa Geita uendane sambamba na utunzaji wa nazingira, wachimbaji wakichimba madini wasiache mashimo ovyo wayafukie hii ni kwa faida ya vizazi vijavyo,” anasema Magembe.

Kaimu Ofisa Madini Mkazi Mkoa wa Geita, Mhandisi Martin Shija, anawakumbusha wachimbaji wadogo wa madini, wanapaswa kutekeleza mpango wa utunzaji mazingira kwa mujibu wa sheria na wasiotekeleza, sheria ziko wazi, ikiwamo kunyang’anywa leseni za uchimbaji, kwa  sababu wanakuwa wamekiuka mpango huo.

WENYE MGODI

Meneja wa Kampuni ya Mgodi wa Stamico Gold Mining Operative Society uliopo Nyarugusu wilayani Geita, Hoja Shikome, anakiri wachimbaji wadogo wanaharibu mazingira, akitaja sababu, hawana vifaa maalumu vya kubaini madini yalipo, wanachimba kwa kubahatisha, hata wanapokosa wanahamia kwingineko, wakiacha  mashimo na kuharibu miti.

 “Uchimbaji mdogo wa madini huwa ni wakubahatisha unakuta mtu amewekeza mtaji wake hata wa shilingi milioni 20, halafu mwisho hawapati madini na mtaji umekatika, unafikiri huyo ataweza tena kufukia mashimo na wakati hana hela? Itabidi atoroke usiku na kuacha mashimo ovyo,” anasema Shikome.

Mkurugenzi Msaidizi wa kampuni ya Geita Resources, Yusuph Kulwa, anasema kunakofanyika uchimbaji mdogo, ni lazima kuwapo uharibifu mkubwa wa mazingira, kutokana na matumizi ya zana duni.

Kulwa ambaye ni mtaalamu wa mazingira, anasema wakati mfumuko wa madini ulipotokea katika machimbo hayo, kulikuwapo na watu zaidi ya 20,000 waliokuwa wakifanya uchimbaji holela.

“Wachimbaji wadogo wa madini wanaposikia eneo lina madini huwa wanavamia kila mmoja akitafuta mali, lakini madini yanapokwisha au kupungua eneo hilo huhama na kuacha uharibifu mkubwa wa mazingira, miti ya asili ikiwa imekatwa na mashimo kuachwa bila ya kufukiwa,” anasema Kulwa.

“Mwaka jana wakati shughuli za uchimbaji madini zinaendelea ungefika katika eneo hili ungeshuhudia uharibifu mkubwa wa mazingira ambao ulikuwa wepo, kwa kweli tulichakaza hii ardhi ilikuwa hitamaniki tofauti unavyoiona hivi sasa tumepanda miti,”anaongeza Kulwa.

Anafanua kwamba, kutokana na yeye kupata elimu ya kutunza mazingira na baada ya kushuhudia uharibifu mkubwa wa mazingira kutokea na hakuna madini tena, ndipo akashauriana na timu nzima ya uongozi, kwamba ni vyema wakafukia mashimo na kupanda miti ili kutunza mazingira.

Kulwa anaeleza kwamba, kwa sasa ni eneo ambalo wamepanda miti ni hekta 2,000 na wameanzisha vitalu vya miche, ili kila eneo wanakomaliza kufanya shughuli za uchimbaji madini, wapafukie mashimo na kupanda miti.

 

Valeria Macha kutoka Timu ya Wanasheria watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT), anasema wachimbaji wadogo wakipewa elimu ya utunzaji mazingira na usimamizi wa sheria, wana uwezo mkubwa wa kubadilika, hata kuifanya Tanzania kuwa na uchimbaji madini usio na uharibifu wa mazingira.

 

Top of Form

Bottom of Form

Top of Form

Bottom of Form