Sababu 5 Wydad kuitoa Simba CAF

01May 2023
Adam Fungamwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Sababu 5 Wydad kuitoa Simba CAF

USIKU wa Ijumaa iliyopita, wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba walihitimisha safari yao kwenye hatua ya robo fainali, walipotolewa kwa mikwaju ya penalti 4-3 dhidi ya Mabingwa Watetezi, Wydad Athletic Club yenye maskani yake Casablanca nchini Morocco.

 

Penalti zilipigwa kwenye Uwanja wa Mohamed wa Tano, baada ya mabingwa hao kufurukuta na kushinda bao 1-0 lililoowekwa wavuni na Msenegal  Bouly Sambou, hivyo ubao kusomeka bao 1-1 kwa matokeo ya jumla, kwani Aprili 22, Simba ikiwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam ilishinda bao 1-0.

Inakuwa ni mara ya nne kwa Simba kuishia hatua hiyo kwenye michuano ya kimataifa kwa misimu mitano ambayo imecheza, na mara tatu kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mara ya kwanza ilikuwa ni mwaka 2019 ilipotolewa dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, baada ya suluhu nyumbani ilikwenda kupigwa mabao 4-1 mjini Lubumbashi na mwaka 2021 ilikomea hatua hiyo kwa kuondolewa dhidi ya Kaizer Chiefs ya Aftrika Kusini jumla ya mabao 4-3, ilianza kupoteza mabao 4-0 ugenini, na ikashinda nyumbani 3-0.

Mwaka jana iliiishia pia hatua kama hiyo kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika, ilipotolewa kwa mikwaju ya penalti 4-3 dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini baada ya kila timu kushinda bao 1-0 nyumbani.

Kwenye mechi dhidi ya Wydad Casablanca, Simba ilionekana kama iko karibu zaidi kufuzu hatua ya nusu fainali, lakini kuna vitu kadhaa ambavyo vilikosekana, au kusababisha kuishia hatua hiyo.

Katika makala haya, tunakuorodheshea sababu kadhaa ambazo zilisababisha  Simba kushindwa kutinga hatua ya nusu fainali dhidi ya mabingwa watetezi hao, twende sasa...

 

1. Kutotumia vema uwanja wa nyumbani

Simba inaonekana kutojipanga vema kutumia uwanja wa nyumbani kwenye hatua hizi za robo fainali. Pamoja na kwamba huwa na uwezo wa kushinda hata mabao 3-0 au hata 7-0 kama ilivyofanya dhidi ya Horoya ya Guinea, lakini inapofika hatua hiyo inashinda mabao machache ambayo yanawagharimu kwenye mechi ya marudiano.

Rejea mechi dhidi ya TP Mazembe 2019 ilipolazimishwa suluhu kwenye mechi ambayo ilipaswa kufunga mabao kadhaa, lakini pia 2022 ilipofunga bao 1-0 dhidi ya Orlando Pirates. Kama ingefunga angalau 2-0 ingeweza kufuzu hatau ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho, na kama ingeshinda mabao kadhaa dhidi ya TP Mazembe ingeweza kuipa mlima mrefu kwao.

Simba ilikuwa na uwezo wa kushinda mabao mengi kwenye mechi iliyopita dhidi ya Wydad Casablanca nyumbani kwani wachezaji wake walipoteza nafasi kadhaa, zikiwamo mbili za Clatous Chama na Pape Sakho kubaki ana kwa ana na kipa, lakini walishindwa. Iwapo ingetumia nafasi hizo, saa hizi Simba ingekuwa inajiandaa kucheza nusu fainali dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

 

2. Makosa binafsi ya wachezaji

Ukiangalia kwenye mechi nyingi hasa za kimataifa, mabao ambayo Simba inaruhusu siyo ya kimfumo, bali ni makosa binafsi ya mchezaji mmoja mmoja, hasa Joash Onyango.

Kwenye mechi za kimataifa hasa msimu huu tayari ameshasababisha penalti tatu, na makosa mengine ambayo yamesababisha mabao kadhaa yaliyoigharibu Simba.

Ijumaa iliyopita, bao ambalo Wydad Casablanca walifunga pia lililotokana na kosa binafsi la Onyango.

Kwanza aliutoa nje na kuwa kona mpira ambao kipa Ally Salim alikuwa ameshafika kuukamata, lakini mawasiliano yakawa hafifu.

Na kona hiyo ilizaa kona nyingine ambayo ndiyo iliyosababisha bao pekee kwenye mechi hiyo. Na hata mfungaji alipopiga kichwa, Onyango alizubaa na kuuruhusu mpira kudunda mbele yake. Hakujishughulisha hata kumbugudhi mpigaji asiwe huru.

 

3. Mipira mirefu

Kwenye mechi hiyo ukitazama, Simba ilikuwa ikipiga mipira mirefu hasa mabeki na viungo. Afadhali ile iliyopigwa pembeni ilikuwa ikidhibitiwa vizuri na kina Kibu Denis, Chama na Saido Ntibazonkiza, lakini ile ya katikati yote ilikuwa ikimezwa na mabeki wawili wa Wydad pamoja na kiungo wao mkabaji ambao wote walikuwa wanakaa na straika mmoja tu, Jean Baleke.

Beleke hakuwa na cha ziada dhidi ya mabeki hao warefu wenye nguvu ambao walikuwa wamesimama na mtu mmoja tu.

Simba walitumia mfumo sahihi ambao uliwadhibiti wapinzani wao, lakini kosa walilokuwa wakifanya ni kupiga mipira mirefu ambayo ilikuwa inachukuliwa tena na adui. Labda mbele kungekuwa na mtu kama mshambuliaji wao wa zamani, Chris Mugalu, mwenye nguvu na uwezo wa kushindana na mabeki wawili, akakaa na mpira. Kama wangejiamini na kwenda na soka la pasi walizozoea kama ambavyo walikuwa wakifanya mara moja moja, wangekuwa hatari zaidi kwa wapinzani wao.

 

4. Kiungo mkabaji bado tatizo

Bado tatizo la namba sita asilia linaendelea kuitafuna Simba, kwani inaonekana hata makosa binafsi yanayofanyika hayasaidiwi na mwingine kutokana na kutokuwa na namba sita.

Miaka kadhaa nyuma, Thadeo Lwanga alikuwa ana uwezo wa kurekebisha au kusawazisha makosa ya wenzake kwa sababu alikuwa ni namba sita asilia.

Mzamiru Yassin Na Sadio Kanoute ukiwatazama wote wale ni namba nane, wanacheza kwa kubadilishana nafasi. Nina uhakika kama Simba ingekuwa na namba sita asilia eneo ambalo Bouly Sambou alifunga, kama namba sita angecheza Lwanga au James Kotei enzi zake asingeruhusu mpira uzagae eneo lile.

 

5. Kikosi finyu

Angalia mabingwa watetezi, kipindi cha pili watatoa wachezaji watatu na wanaingiza wengine watatu, baadaye wanatoa wawili wanaingiza mashine mbili. Ina maana ndani kuna nusu nzima ya wachezaji wapya, dhidi ya wale wale 11 wa wapinzani ambao walianza tangu mwanzo.

Simba ilianza kuingiza wachezaji kuanzia dakika ya 80 kuendelea na ilionekana ni kwa sababu ya penalti. Nao ni Erasto Nyoni na Moses Phiri.

Simba ndiyo timu pekee kwenye Ligi ya Mabingwa ambayo haipumzishi wachezaji mpaka ifikie dakika 15 au 10 kabla mechi kumalizika. Hii ina maana wanaokaa benchi wengi wao hawana viwango ama vya kucheza mechi za kimataifa, au kuchezea Klabu ya Simba.

Kuna wachezaji hao hao tegemezi kuwachosha sana, ikizingatiwa wenzao wanakuwa wameshaingiza wachezaji wengine ambao wana uwezo kama wale au kushinda. Na hii ilionekana pia kwenye mechi ya Ijumaa dhidi ya Wydad Casablanca.