Ndiyo inayosogeza udadisi wa Nipashe katika maisha ya kijana Abdul -Azizi Khamis Ali (18), mwenye ulemavu wa uziwi, ambaye licha ya hali hiyo, sasa anaingia katika orodha ya vinara waliofanya vizuri shuleni kwake.
Shule ya Sekondari ya Dk John Joseph Magufuli, alikohitimu Abdul, wamekuwa jumla 103, katika matokeo ya elimu kidato cha nne, imemtoa mwanafunzi mmoja mwenye ufaulu daraja la kwanza, kijana huyo akiwamo, katika orodha watahiniwa tisa waliopata daraja la pili, sita wenye daraja la tatu 28, daraja la nne 59 na sita daraja sifuri.
Akizungumza na Nipashe nyumbani kwao Mwanakwerekwe mkoa wa Mjini Magharib Unguja, Abdul anasema hakutarajia ngazi hiyo ya ufaulu, kwani alilenga daraja la kwanza, lakini changamoto za elimu, zilimkwamisha.
Kijana Abdul -Azizi akisimulia alikopita shuleni, alikabiliwa na changamoto kukosa mkalimani wa lugha ya alama shuleni na kumsababisha achukue hatua ya ziada apate uelewa, jambo lililompa ugumu masomoni
Anaeleza, namma ugumu huo ulivyo, ni mwalimu anapofundisha bila ya mkalimani, inamuacha nyuma kimawasiliano, tofauti na wanafunzi wengine, hata ikambidi kutafuta wakalimali wa kujitolea kumfafanulia anachozungumza mwalimu.
Kuhusu siri ya mafanikio yake, anadokeza ni juhudi za kusoma, pia msaada wa walimu wake, wazazi na wakalimani, waliojitolea shuleni, hali kadhalika ushirikiano kutoka kwa wanafunzi wenzake shuleni.
“Mwalimu anapomaliza kusomesha darasani huwa sioni tabu kuuliza pale ambapo sijafahamu au huwauliza wanafunzi wezangu na wakinipa ushirikiano mzuri bila ya kuninyanyapaa”anasema.
Sasa anasema malengo yake ya baadae ni kuwa daktari wa binadamu, kwa ajili ya kutoa huduma za matibabu ya afya kwa wananchi hasa watu wenyeu ulemavum akishauri ni vyema Wizara ya Elimu ikaandaa mitihani maalum kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum, ili kuwathmini kwa haki zaidi.
Anasema, wasiwasi wake sasa ni masomo ya kidato cha tano, akifafanua: “Kila ukipanda juu zaidi, masomo ndio yanakuwa magumu kutokana na mazingira ya kupata elimu kwa watu wenye ulemavu, bado sio rafiki sana.”
Mwanafunzi huyo anasema awali alifaulu kuingia shule ya vipawa maalum darasa la saba na kubahatika kupelekwa shule maalum, lakini akashindwa kusoma huko, kutokana na changamoto za walimu wanaofundisha lugha ya alama.
WAZAZI WA WANAFUNZI
Mama wa mwanafunzi huyo, Maua Abdallah (53), anasema mwanawe huyo ni wa sita kati ya watoto wake saba, wawili wana shida ya kusikia tangu kuzaliwa na hajajua sababu, licha ya kuhangaikia matibabu katika hospitali mbalimbali.
“Hali yake tumeipokea na tunampa haki zake zote zinazostahiki ikiwamo elimu,” anasema mama huyo, huku baba wa mwanafunzi huyo, Khamis Ali (67), anaelekeza pongezi kwa serikali kupitia Baraza la Watu wenye Ulemavu, kwa msaada wa kuwajali watoto wenye ulemavu na kufuatilia maendeleo yao.
“Dada yake Abdulazizi ambaye nae ni kiziwi, anasoma elimu ya juu Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU), lakini ada ya chuo analipiwa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Watu, Wenye Ulemavu maana hali zetu za kiuchumi ni duni sina uwezo wa kumlipia ada,” anasema, akiiomba serikali kuajiri wakalimani kuwawezesha darasani wanafunzi wenye uziwi.
JUMUIYA WAKALIMANI
Muhammed Wahabi kutoka jumuiya ya wakalimani wa lugha ya alama Zanzibar (JUWALAZA), anasema lugha ya alama alianza kujifunza darasani wakati huo akisoma shule pamoja na wanafunzi viziwi lakini baada ya kuingia kidato cha tatu aliacha kuwasiliana na viziwi kwa sababu hawakufanikiwa kuendelea na masomo.
Anasema baada ya kukutana na mwanafunzi Abdul-Azizi mwaka 2021 wakati akimfundisha masomo yake katika muda wa masomo ya ziada (Tuisheni) ndipo alipomshauri kwenda kusoma lugha ya alama ili kumsaidia katika mawasiliano hasa katika masomo yake.
Wahabu anasema, hakupuuza ushauri wake na ndipo alipoanza kujifunza lugha hiyo ya alama, baada ya kuona jitihada zake kutafuta elimu na ufahamu wake ni mzuri kuliko kwa wale wasio na ulemavu.
Anasema alijifunza lugha ya alama kutokana na msukumo wa mwanafunzi Abdul-Azizi na alipoijua lugha hiyo, akamshawishi tena akaombe shuleni anakosoma, ili kuwasaidia wanafunzi viziwi w Shule ya Dk. Magufuli.
“Nashukuru nilipoenda kuomba kujitolea shuleni hapo, niliruhusiwa nikawa nawasaidia wanafunzi viziwi katika masomo yao kwa muda wa miaka mitatu tokea mwaka 2020 hadi 2022 baada ya serikali kupitia wizara ya elimu kusitisha vijana wanaojitolea ambao hawajaajiriwa,” anasema.
Anafafanua kuwa, nje ya Shule Abdul-Azizi alianza kumfundisha lugha ya Kiingereza na yupo vizuri katika lugha hiyo ambayo imemuwezesha kufanya vizuri katika mitihani yake.
Pia, anafafanu kwamba, ingawa hayakuwa matarajio yake mwanafunzi wake kupata daraja la pili la ufaulu, akitarajia daraja la kwanza, hata anayatathmini ni matokeo ambayo yamemfiji sana.
Sasa anashauri kiseriali, elimu mjumuisho iboreshwe zaidi ili watu wenye ulemavu kuwekewa miundombinu rafiki katika kupata elimu.
Swafinia Ali Salum, ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Dk. Magufuli ambae anashughulikia wanafunzi wenye mahitaji maalum ambapo shule hiyo kwa sasa inawanafunzi saba wenye ulemavu wakiwemo viziwi na waviungo.
Anasema shule hiyo inafuata muongozo wa elimu mjumuisho ambapo wanafunzi wote wenye ulemavu na wasio na ulemavu kuchanganywa darasa moja kwa kupata elimu.
MWALIMU SHULENI
Mwalimu huyo anamuelezea mwanafunzi wake Abdul-Azizi licha ya kwamba ana ulemavu lakini ni mwanafunzi hodari anayependa kujifunza na hufanya vizuri kuliko wanafunzi wasio na ulemavu, akifafanua shule hiyo hutoa elimu kwa wanafunzi wasio na ulemavu na hakuna tabia ya kuwanyanyapaa, bali wanapewa ushirikiano.
Akizungumzia kuhusu vifaa au visaidizi kwa watu wenye ulemavu, anasema kwa upande wa viziwi, hakuwa na visaidizi vya aina yoyote, ila kwa kwa walemavu wa viungo, shule hiyo ina miundombinu rafiki, ikiwamo katika majengo yke ya ghorofa.
Anasema shuleni hapo kuna changamoto kubwa ya wakalimani kwa wanafunzi viziwi hasa baada ya kuondoka kwa walimu wa kujitolea ambao waliokuwa wakiwasadia wanafunzi viziwi katika lugha ya alama.
“Mimi nawashughulikia wanafunzi wote wenye ulemavu na wasio na ulemavu na mimi nasomesha somo la Kiswahili na historia sasa ninapofundisha huwa natumia sauti na ishara yaani lugha ya alama ili wanafunzi viziwi nao kufaidika ingawa mimi sijasomea lugha ya alama lakini nimejifunza kutoka kwa wanafunzi viziwi”anasema.
Anasema matarajio yake ni kwenda kusomea lugha ya alama ili kuwaondoshea vikwazo katika shule hiyo kwa wanafunzi viziwi kupata elimu.
Aidha anasema amefarajika sana ufaulu wa mwanafunzi wao Kiziwi hivyo wanafunzi wenye ulemavu wakiwekewa mazingira mazuri wanauwezo wa kufaulu vizuri katika masomo yao.
WIZARA ELIMU
Kwa mujibu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, kuna wanafunzi 26,169 walifanya mitihani ya kidato cha nne Zanzibar mwaka jana, kati yao 14 ni wenye ulemavu kutoka shule za serikali za Unguja, akiwemo Abdul-Azizi.
Juma Salum Ali, ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Elimu Mjumuisho na Stadi za Maisha, anasema kabla ya mwaka 2004 kuanza mfumo huo wa elimu mjumuisho, wanafunzi wenye ulemavu walikuwa wanasoma katika mazingira magumu zaidi.
Ali anadems, mfumo umesaidia wanafunzi wengi wenye mahitaji maalum, fursa ya kupata elimu na sasa, kuna wanafunzi 7,314 wenye ulemavu mbalimbali katika shule za serikali, kuanzia ngazi ya maandalizi, msingi na sekondari na wanafanya vizuri katika mitihani, mchangio kmkuu ni msaada wanaopata.
Pia, anataja mkakati wanaotumia katika kupunguza changamoto hiyo, ni kuwafundisha walimu lugha ya alama nai elimu hiyo haishii kwa walimu pekee, hata kwa wanafunzi wasio na uziwi, ili wawasaidie wenzao wahitaji wa msaada.
Katika vifaa visaidizi kwa wanafunzi wenyeulemavu, mkuu wa kitengo hicho, anasema serikali imejitahidi kuwanunulia wanafunzi hao vifaa, hata anakiri havitoshelezi mahitaji, ikiiwamo kwa wenye shida ya kusikia.
“Wizara imenunua vifaa vingi kwa wanafunzi wenye ulemavu kwa Shule za Unguja na Pemba ambapo gharama ya vifaa hivyo ni zaidi ya shilingi milioni 400,” anadems, hukia kirejea upande wa pili, kwa sasa wazazi wengi wanahamasika kuwapeleka shule watoto wao wenye ulemavu.
WADAU WANAOWASAIDIA
Mwenyekiti wa Umoja wa watu wenye Ulemavu Zanzibar, Salma Saadati, anasema elimu kada hiyo kwa sasa inatoa matokeo chanya, ikilinganishwa na nyuma wanafunzi hao walikosa haki.
Anasemas, Wizara ya Elimu, ina jukumu la kuajiri wakalimani, kuwasaidia wanafunzi viziwi kupata elimu na kufaulu mitihani yao vizuri.
Mwadawa Khamis, Mwenyekiti wa Shirikisho la Jumuiya za Watu Wenye Ulemavu Zanzibar (SHIJUWAZA), anasema wanafunzi wenye uziwi, wanahitaji jitihada za ziada kuwapatia elimu na kwenye lugha ya alama, iwe somo la lazima kwa wanafunzi wote.
Anasema, wanafunzi wengi viziwi huvunjika moyo, hata kuwafanya kutoroka shule kutokana na changamoto za kupata elimu, hasa kukosa mawasiliano yao.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Watu Wenye Ulemavu Zanzibar, Ussi Khamis Debe, anashauri Baraza la Mitihani Zanzibar, wanapotoa matokeo ya wanafunzi, waweke mahsusi ufaulu wa wenye ulemavu kwenye mitihani hiyo ya taifa.
Anasema hali ilikofika, jamii imeshapata mwamko kuona watu wenye ulemavu wana haki ya kupata elimu, ingawa kiwango chao cha ufaulu bado kidogo, kwani kuna changamoto nyingi kwao katika kujifunza.
“Idadi ya viziwi Zanzibar inaongezeka, hivyo ni vyema kuwa na wakalimani ambao watakidhi mahitaji katika kila sekta na si kwa sekta ya elimu pekee”anasema.
Anasema tayari Sheria mpya Namba Nane ya Mwaka 2022 ya Watu Wenye Ulemavu, imeshapitishwa na kutiwa saini na Rais, ikiopatia meno ya kusimamia majengo yote ya umma kuzingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu, akishauri kila mzazi anapaswa kusimamia masklahi ya watoto wao wenye ulemavu.
WAZIRI ELIMU
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Leila Muhammed Mussa, anasema wizara hiyo inaendelea kuboresha sekta ya elimu, ili watoto wote kupata elimu bora, ikitarajia kuajiri walimu mahsusi wa lugha ya alama shuleni, pia inamalizia ujenzi wa shule mbili za elimu mjumuisho, za Jendele, Unguja na Pujini, Pemba.
“Shule hizi zitakuwa na vifaa vya kisasa kwa watu wenye ulemavu katika kupata elimu lakini pia shule hizo zitakuwa na bweni ili wanafunzi wenye mahitaji maalum kupata mda wa ziada wa kufundishwa masomo yao”alisema Waziri huyo.










