Kauli yake ya kitaalamu inasimamia, ni vema wanawake wa Kitanzania wakazitumia teknolojia mpya zilizopo, huku wakibuni na kuanzisha vitu vingi vyenye tija vya kuonekana na kutumika katika ulimwengu mzima.
Dk. Lusako anasema wanawake ni lazima waonyeshe uthubutu katika kutekeleza vitu vingi vilivyopo, sambamba na teknolojia inayokuja kwa kasi, hata ikawafanya wasiwe na hofu ya kufanya mambo makubwa, kwa sababu licha ya kukua teknolojia, bado wapo wanawake wenye woga wa kufanya mambo hayo, hata kuwafanya wawe nyuma kimaendeleo.
Anasema, licha ya baadhi yao wana uwezo kuendesha magari ya kisasa, bodaboda, mabasi ya abiria, meli na hata ndege, sambamba na uthubutu wa kufanya biashara kubwa kama kwenda nchi kama za Uturuki, China na Japan kuchukua bidhaa kwa ajili ya kusogeza mbele gurudumu la maendeleo, lakini wapo ukiwauliza wanasema hawajui hata wafanye biashara gani.
“Ni vema wanawake wengi wakabadilika na kuwa na mitazamo sahihi hasa kwenye masuala a maendeleo, utamkuta mwanamke amekaa nyumbani kuanzia asubuhi hadi jioni bila ya kufanya shughuli yoyote ya kumuongezea kipato, hadi lini mwanamke utaitwa golikipa, ni wakati sasa mwanamke afanye biashara hata tatu au nne ili kuwa na kipato cha uhakika” anasema Dk. Lusako.
Hapo anafafanua kwa mfano binafsi kwamba, yeye akiwa ametunukiwa shahada ya usomi ngazi ya udaktari, bado anaendesha shughuli za kumuongezea maendeleo, zikiwamo za kutoa huduma za kibenki, akiwa ni wakaka wa benki zaidi ya nane, ikiendana na kampuni kadhaa za simu,
Rai yake kwa kinamamama, waingie katuijka anachokiita ‘mioyo ya kuamka’, kutenda na kubuni wanachomudu, kwa sababu biashara ziko nyingi, lakini tatizo kubwa lililopo ni wanawake au kinamama ni kuchagua biashara huku wakiwa hawana mitaji ya uhakika.
Dk. Lusako anawaomba wanawake kujenga tabia ya kuwafundisha watoto wao wa kike shughuli za maendeleo, ili waweze kufanya miradi ya maendeleo kama wao na kusimama katika misingi mizuri ya maendeleo kwa kutumia teknolojia zilizopo.
Anasema, mwanamke jasiri lazima ahakikishe binti yake anakuwa jasiri hata kumzidi yeye katika kutenda kwa kutumia teknolojia zilizopo.
“Usiogope kazi ya mtoto wa kiume kumwambia mwanao wa kike aifanye, mfundishe aifanye na ataweza kuifanya kwa kutumia teknolojia kwani itamrahisishia na kuwa mahiri sana, tusiwape kazi laini laini watende kama tunavyopenda na wafanye kama tunavyofanya.
“Sijawahi kuona kuna kazi inanishinda, labda ya kuoa tu, kwa kuwa sio stahiki yetu. Tunatakiwa tuwe chini ya himaya ya mwanaume, pia tuwe watii lakini hatukatazwi kuwasaidia wanaume zetu ili kujenga familia zetu” anasema.
Hata hivyo, anawataka wanawake kuondoa hofu ya kushindwa, bali wafungue viwanda vidogo na vikubwa na kufanya kazi ya kumsaidia Rais Dk. Samia kusimamia majukumu ya kulijenga Taifa.
Aidha, mkurugenzi huyo wa ujasiriamali anaeleza anachoamini kwamba wakitokea wanawake wengine walio tayari kusimama kwa uadilifu na kujituma katika kutumia vyema teknolojia zilizopo kimaendeleo, Rais Dk. Samia atazidi kuwekeza mikopo kwao, pia akiboresha iliyopo kwenye halmashauri nchini.
“Pesa zipo, kila halmashauri na hazina wakopaji. Ukiwakumbusha wanawake kukopa, wanasema hawawezi kuunda vikundi sababu hawaaminiani, jamani tunachelewa wapi?”anang’aka mama huyo.
Anaendelea kunyoosha kidole kuwa: “Adui wa mwanamke ni mwanamke mwenziwe! Hebu wanawake tuwe timu moja, mwenzio akitenda, wewe mbariki na wewe ukitenda yeye atakubariki, hauwezi kutembelea nyota ya mtu hata siku moja.”
Hivyo, anawaasa wanawake kupitia teknolojia na usawa wa kijinsia, wasimame kuona kama wataweza kufanya hata yasiyowezekana, lakini yanayofaa kwa jamii na Taifa kwa ujumla.
Dk. Lusako anawataka wanawake kutambua kuwa wanaume ni vichwa ndani ya nyumba hawawezi kushindana nao ila washindane nao kwa fursa na weledi katika kutenda kwa sababu anasema mume mwema akiona mke wake anapambana atashukuru na kuona anaisaidia familia yake kuinuka naye atapata nguvu zaidi.