Amri aliibuka mshindi kwa kuandika Diwani iliyokuwa mfumo wa simulizi iliyoipa jina la ‘Mtale wa Ngariba’ ikihusu ukeketaji na madhila ya unyanyasaji yanayowakumba watoto wa jamii ya kimasai.
Kutokana na lugha aliyoitumia na wazo la kipekee kwenye kuwasilisha kazi hiyo, serikali kupitia Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Adolf Mkenda, inalazimika kuichukua na kuisambaza maeneo mbalimbali ikiwamo shuleni, maktaba na vyuoni.
Akizungumza katika ofisi za Nipashe hivi karibuni, mshindi huyo anasimulia ameamua kuandika muswada huo, kwa kuwa ni kisa cha kweli na yeye ni shuhuda, hata akaamua kuhamishia kwenye andiko.
“Mtale wa Ngariba, maana yake ni kisu cha Ngariba. Mtale ni neno la Kiswahili lenye maana ya kisu, lakini watu wengi hawautumii msamiati huu, ndio maana nimeutumia ili watu waujue.
“Mimi niliamua kuja na hadithi kwenye miswada yangu na kuipeleka kwenye mashindano, baada ya kukutana na binti wa Kimasai mwaka 2010, aliyekuwa miongoni mwa waliopitia changamoto ya ukeketaji na kulazimishwa kuolewa akiwa na umri mdogo,”anarejea mkasa uliommsukuma kwenye wazo la kuandika hoja hiyo, akiongeza:
‘Nilipomuhoji kwenye simulizi yake, aliniambia baadaye alipata ujauzito, lakini hakuna aliyekuwa anajali, kwa sababu alitoroka nyumbani kukwepa kuolewa kilazima, akajifungulia porini kwa kuwa hakuna aliyekuwa anamjali.
Amri anasema, baada ya hapo akamchukua na kumpeleka kwa mama yake mdogo, wakawa wanaishi pamoja. Anasema, kitendo hicho kilimuumiza sana na alipoona imetokea nafasi ya kuandika ushairi kwa ajili mashindano, akaamua kutumia kisa hicho ili kupeleka ujumbe kwa jamii” anaeleza Amri, ni mzaliwa wa Kilimanjaro, ambaye sasa ni mwalimu wa Shule ya Sekondari Baobab, iliyoko Mapinga, Bagamoyo.
Amri, anafafanua kuhusu kisa cha binti huyo wa kimasai (jina tunalo), pia imejikita katika azma ya kumkomboa mwanamke dhidi ya ukatili wa kijinsia, kijamii, kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni na kifikra.
Mbali na serikali kuchukua jukumu la kukisambaza kitabu hicho kwenye taasisi za elimu, bado Amri anasema ataendelea kunufaika na malipo kutokana na manunuzi kwa wahitaji wa ununuzi wa vitabu hivyo.
“Nina furaha kushinda tuzo hii, ukizingatia ndio mara ya kwanza tangu imeanza hii ni tuzo kubwa Tanzania. Ni heshima kuipata kwa sababu washiriki walikuwa wengi, lakini imekuja kwangu.
“Pia, ninawashukuru majaji wa tuzo hizi wakiongozwa na Jaji Mkuu, Profesa Fiken Senkolo, wamefanya kazi kubwa sana na ndani ya muswada wangu, nimeelezea namna kisu cha ngariba kilivyosababisha kuharibika kwa mfumo mzima wa maisha kwa binti wa kimasai,” anasema
AIPONGEZA SERIKALI
Amri anasema shilingi milioni 10 aliyoipata kama zawadi siku hiyo, inamnufaniha kwa mambo yake mengi ya msingi, huku akiimwagia sifa serikali kwa ubunifu wa kuandaa tuzo hizo.
“Serikali imefungua milango mipya, kwa sababu inawapa wabunifu nafasi ya kuonyesha kile walicho nacho na kuhamasisha wengine kupenda kuandika na kusoma vitabu.
“Jambo zuri zaidi tokea kuanzishwa kwa tuzo hizi, muitikio ulikuwa mkubwa sana, zilipokewa kazi 283, kati yake 79 zilionekana hazijakidhi vigezo kabisa, zikabaki 204 kwenye hizo tena moja ikaonekana haifai ikaondolewa.
“Kwa hiyo, katika kazi 203 zilizobaki 159 zilikuwa za ushairi na riwaya zilikuwa 44. Haya ni mapinduzi na mafanikio makubwa sana kwenye tasnia ya elimu na nchi kiujumla,” anasema.
Anafafanua kuwa anasema kazi yake ya ushairi ina beti 314, akisifu ni hadithi tamu inayoburudisha, ambayo mtu anapoanza kuisoma hatotamani kuishia njiani.
Anafafanua uzoefu wake kwenye mashindano ya aina hiyo, akikumbushia aliwahi kushiriki kwenye mashindano ya ‘Safal Cornel’ yaliyokuwa ya mfumo huo, lakini hakufanikiwa kushinda.
DHAMIRA IJAYO
Anachoamini, muswada huo umetoa elimu na kuwaasa wazazi umakini kwenye malezi na maadili ya watoto, jamii kuacha kukumbatia mila na desturi zilizopita na wakati, mfano ukeketeji ambao ndio sababu ya binti kuharibikia, kama alivyoisimulia kwenye andiko lake.
Dhamira nyingine anaitaja ni kuwataka wanawake wasijibeze na kwamba wanaweza kufanya shughuli yoyote, kama ilivyo kwa wanaume, kikubwa ni wazazi kuwa makini kwenye malezi ya watoto na watu wa karibu, haki ya mtoto kupata elimu na muhimu ni penye elimu ya jinsia na maadili, kuanzia ngazi ya msingi.
Mshindi huyo anawasihi wadau wengine kujitokeza kushiriki tuzo hizo kwa mwaka ujao, kwa kuwa hazina mipaka na hazichagui watu wa kuwania.
“Milango ya kushiriki ipo wazi kwa mtu yeyote, japo kwa mwakani walisema wataongeza baadhi ya vipengele, sio riwaya na ushairi pekee kama ilivyokuwa mwaka huu, itakuwapo pia tamthilia, hadithi fupi, fasihi ya watoto na tafsiri,” anaeleza mtaalamu huyo wa ushairi.
Anashauri kwa yeyote anayeweza kuandika, wakati ni sasa kwa kuwa lugha ya kiswahili imeenea zaidi nchi jirani na serikali ipo kwenye mpango wa kuifikisha mbali zaidi lugha hiyo.
Anasema kwa mtu, anayetaka kushiriki kwaajili ya tuzo ahakikishe anafuata maelekezo yaliyotolewa na tume ya tuzo, pia andiko lake liguse masuala ya kijamii na liwe makini kwenye ubunifu wa hali ya juu na lugha rafiki itakayo mshawishi msomaji kusoma na kumaliza kitabu kizima.
SIRI YA MAFANIKIO
Pamoja na uzuri wa kazi yake,Abdala anataja siri ya mafanikio yake Kwamba wapo waliomshika mkono na kushirikiana nao mpaka kuibuka mshindi tuzo hiyo.
Anataja mafanikio yake, ni zao la kumtanguliza Mungu mbele na ushirikiano alioupata kutoka kwa walimu wenzake na familia yake kwa ujumla.
“Ninaishukuru serikali, ya Rais Samia Suluhu Hassani kwa kukubali kutoa fedha kiasi cha bilioni moja na zaidi, kwaajili ya tuzo hizi, pia Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) iliyopewa jukumu la kusimamia tuzo hizo kupitia Mkurugenzi wake, Aneth Komba.
“Pia uratibu mzuri uliofanywa na kamati ya tuzo chini ya Prof Penina Mlama, ambaye ndiye alikuwa Mwenyekiti wa Tuzo hizo, pamoja na majaji,” anasema.
Vilevile, anarejesha shukurani kwa walimu wenzake, kwa kumpa moyo wakati wote, akiwamo Mkuu wao wa shule, Venance Hongoa, ambaye huwa anawasihi walimu kuchangamkia fursa zinapojitokeza, pamoja na walimu wenzake Salum Kaneme na Songoi Kwalu.