Kinamama waathirika wa biashara wanyamapori, waliogeuka walinzi

20Apr 2023
Jenifer Gilla
Nipashe
Kinamama waathirika wa biashara wanyamapori, waliogeuka walinzi
  • Wakaa jela, kuuguza watoto, kudhuriwa…

NI mwaka 2016, ambao Lydia Joseph, mkazi wa Kijiji cha Ngoley katika Halmashauri ya Wilaya ya Babati, hatousahau, kutokana na machungu aliyopitia yakileta mageuzi makubwa katika maisha na ukombozi dhidi ya biashara haramu ya wanyamapori kwa jamii yake.

Akisimulia mkasa uliomkuta mama huyo aliyekulia katika familia ya wawindaji, yalipo mapitio ya wanyama (shoroba) ya Kwakuchinja, anasema mnamo Aprili 6, mwaka huo, mwanawe aliyerithi mikoba ya uwindaji alimletea nyama ya pundamilia ale, huku akienda kuuza nyama iliyosalia.

Lydia anasema, biashara ya uwindaji pasipo kibali maalum na kuuza nyamapori ilishapigwa marufuku na kulikuwa na doria kali dhidi yake. Haikupita hata saa moja, polisi walifika mlangoni mwake kumkamata, ila akafanikiwa kutoroka kwenda mjini Arusha kwa mtoto wake mwingine kujificha.

“Arusha nilikaa kama wiki mbili hivi, wakaja kunikamatia huko huko, nikarudishwa Babati nikapelekwa Magereza ambalo nilikaa miezi minne. Ikabidi watoto wauze baadhi ya mashamba yangu ili ipatikane faini ya Sh. milioni 2.5 ndio nikatoka. Huo ndio ukawa mwisho wa mimi kula nyamapori na mwanangu kufanya hiyo biashara,” anasimulia Lydia.

Kwa mujibu wa Meneja Ufuatiliaji na Tathmini wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID), John Noronha, katika mradi wa Tuhifadhi Maliasili, inakadiriwa kuna vifo vya wanyama 1069 vimetokea kati yam waka 2012 hqdi 2019.

Aidha alisema katika kipindi hicho   watu 642 walijeruhiwa na kupata vilema vya kudumu, kutokana na migogoro kati ya wananchi na wanyama inayoendelea katika maeneo yanayounganisha hifadhi nchini (shoroba).

Anataja chanzo kikuu ni kufanyika kwa shughuli za kibinadamu katika maeneo wanayopita wanyama hao. Lingine ni uwindaji haramu, kinyume na Sheria ya Wanyamapori ya Mwaka 2009.

Lydia ambaye sasa ni mhamasishaji wa uhifadhi wa wanyamapori, anasema baada ya kutoka jela aligundua kuwa si mhanga pekee wa biashara haramu ya wanyamapori, kwa kuwa asilimia kubwa ya wanawake walioenda kumpa pole, walimhadithia matatizo wanayopitia kutokana na biashara hiyo wanazaofanya waume na watoto wao.

“Hapo ndio nikapata akili kuwa wanawake wengi tunaoishi katika mapitio ya wanyama ya Kwakuchinja, tunapitia matatizo mengi kutokana na biashara hii. Ndipo nikahamasisha wanawake wenzangu tukaunda kikundi chetu cha kukemea uwindaji wanyamapori haramu tukakiita Lamailama Group” anasema.

MWENYEKITI KIKUNDI

Mwenyekiti wa kikundi Lamailama, Petronila Gobbi anasema kilichomvutia kuingia kikundi hicho cha uhamasishaji ni ‘misukosuko’ ya ulezi wa familia wanayopitia, baada ya mume wake kukamatwa na kukaa jela miezi sita, alipokamatwa akiuza nyama ya digidigi aliyeiwinda bila kibali.

Mume wake alimwacha na watoto wadogo watatu maisha yalikuwa magumu, kwa kuwa alimtegemea kuleta mahitaji nyumbani, hali iliyomfanya kuuza baadhi ya mali zake apate pesa za kulea watoto.

Anasema baada ya kuunda kikundi mwaka 2018, walitembelewa na taasisi ya kijamii ijulikanayo Community Support Initiative Tanzania (COSITA) kwa kushirikiana na Polisi wa Usalama Barabarani waliopata fedha kutoka USAID na kuwapa mafunzo ya umuhimu wa kuhifadhi wanyamapori kwa jamii yao na taifa kwa ujumla.

Petronila anasema walipatiwa fedha Sh. milioni nne kwa ajili ya kutumisha mfuko wao wa vikoba na kununua kuku 100 wa nyama, huku kila mwanachama akikopa pesa kwa ajili ya kuanzisha mradi wake binafsi.

“Maisha yangu yamebadilika. Hiki kikundi kimeboresha maisha yangu, kutoka kuwa mama wa nyumbani na sasa nina mifugo na biashara ndogo ndogo. Hata nilipomwambia mume wangu sasa biashara ya wanyamapori basi, alinielewa kwa sababu anaona naleta pesa ya kusaidia chakula wakati yeye akihamia kwenye kilimo,” anasema.

SIMULIZI ZA MADHARA

Mwanachama, Matilda Daniel, anasema alipata hekaheka ya kuuguza mtoto wake aliyevimba mdomo  kuwa mwekundu, baada ya kula nyamapori ambayo hakuweza kuifahamu, ambayo ililetwa kwao imeshachunwa.

“Baada ya kupeleka mtoto hospitali nikaambiwa amekula kitu ambacho kimemdhuru, wakaniuliza alikuwa nyama gani? Nikashindwa kusema, kwa sababu hata mimi sikuijua. Kwa hiyo tatizo jingine ni kama hilo, tunaletewa nyama ambayo hata hatuijui ni ipi matokeo yake inatudhuru,” anasema.

Matilda anaeleza kuwa, tangu amejiunga na vikoba maisha yake yamebadilika, kwa kuwa kila mwaka anakopa pesa inayomsaidia kukuza ndoto yake ya kuwa mfugaji na sasa ana kuku takribani 30 waliotokana na pesa za mkopo.

Mkurugenzi wa USAID, John Noronha, anasema tayari Dola za Marekani milioni 37.5 sawa na Sh. bilioni 86.25, zimetengwa kwa ajili ya kuboresha mapitio ya wanyama ‘shoroba’ ikiwamo kutoa elimu juu ya uhifadhi na kuwapa wanavijiji mitaji, ili kuachana na shughuli ya uwindaji haramu.

SURA YA MAFANIKIO

Lydia Joseph, ambaye ni mhamasishaji mkuu wa kikundi hicho, anasema tangu wameanza kutoa elimu kwa jamii inayozunguka rasilimali hiyo, kadhia yenye madhara kwa wanyama imepungua kwa kiasi kikubwa.

Anaeleza kuwa elimu walioitoa imebadilisha mawazo ya jamii na kufikia hatua baadhi yao wanaanika njia mpya zinazotumiwa na wauzaji nyama hizo haramu, ikiwamo kutangaza kuwa wanauza mboga za majani, huku chini wakificha nyamapori.

Chifu wa kitongoji wa Eluway, Leteiva Loburu, anasema moja ya mambo yanayochangia kushamiri uwindaji haramu katika eneo hilo, ni imani potofu iliyoenea kuwa baadhi ya nyama kama vile punda inaponeshaa magonjwa ikiwamo kifua, miguu na kusafisha figo.

“Sasa unakuta kundi linaoingia katika mtego huo ni wanawake, kwa sababu ni watu wa kuamini vitu kwa haraka. Wao wakiambiwa tu ‘hii ni dawa ya kitu fulani’ na ukiangalia ndani ana mgonjwa atakuwa ananunua kila siku,” anasimulia kiongozi huyo.

Sasa anashukuru elimu iliyotolewa na misaada ya kimaendeleo waliopewa na mashirika mbalimbali, ikiwamo Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Burunge (JUHIBU), kuwa imepunguza migogoro kati ya wanyama na binadamu, sasa wanaweza kukaa eneo moja bila ya kuleteana madhara.

Katibu wa Hifadhi ya Wanyamapori ya Burunge (BWMA), Benson Mwaise, anasema wanashirikiana na wadau wengine wa uhifadhi, ikiwamo TAWA (Tanzania Wildlife Management Authority) na USAID kuhakikisha wanamaliza tatizo uwindaji haramu katika eneo la Kwakuchinja kwa manufaa ya wanakijiji na wanyama.

Anasema, baadhi ya mikakati yao ni kutoa elimu za uhifadhi kwa wanakijji na kutoa gawio linalotokana na shughuli za utalii katika Hifadhi ya Wanyamapori ya  Tarangire kila mwaka kwa wanakijiji, wanayoitumia kwenye miradi ya maendeleo, ikiwamo ujenzi  na ukarabati wa shule pamoja na kutunisha mifuko ya vikundi cha kinamama ya vikoba.

“Kupitia njia hizi jamii imeelewa imeona umuhimu wa kuhifadhi maliasili hii muhimu kwa utalii nchini, sasa hivi na wenyewe wanashiriki kuitunza, hata wakiona swala amepotea au ameumia watatoa taarifa au kumleta hapa ofisini, kwa kweli tunashukuru wadau ikiwamo USAID wanaotuunga mkono mafanikio ni makubwa,” anasema.

Habari hii imefanikishwa kwa ufadhiri wa mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili unaotekelezwa na Chama cha Waandishi Habari za Mazingira (JET).