Kutapakaa machimbo Butiama kunavyoharibu mazingira

20Apr 2023
Marco Maduhu
aliyekuwa BUTIAMA
Nipashe
Kutapakaa machimbo Butiama kunavyoharibu mazingira

SEKTA ya Madini inadumu chini ya usimamizi wa Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na marekebisho yake 2017.

Muonekano wa machimbo katika Mgodi wa Madini ya Dhahabu, Sirorisimba, uliopo wilaya ya Butiama mkoani Mara, ukionekana jinsi ulivyokatwa miti. PICHA: MARCO MADUHU.

 

 

Upande wa pili, kazi zao zimekuwa na athari ya mazingira kuondoa uoto wa asili, kutokana na ukataji miti hovyo, kwa ajili ya kupata magogo ya kwenye mashimo (maduara) ambayo hutumia kuingia chini ya ardhi kwa ajili ya kupasua miamba yenye madini.

Baadhi ya migodi iliyotembelewa na Nipashe iliyopo Halmashauri ya wilaya ya Butiama ni Mgodi wa Sirorisimba, Magunga, Nyamikoma kuona namna uoto wa asili, unavyoathrika kwenye maeneo hayo ya machimbo, kutokana na ukataji miti hovyo.

Hilo linachukua sura  huku Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004, inaongoza ili kuondoa uharibifu wa athari za mazingira katika Migodi, ni lazima sheria husika zizingatiwe. Pamoja na kuhakikisha kuwapo mipango, madhubuti itakayowapa wachimbaji wadogo hisa za kiuchumi, ili wawe na njia mbadala na kufanya uchimbaji kwa kuzingatia sheria za uhifadhi wa mazingira.

Ofisa Usimamizi wa Taka na Mazingira, Halmashauri ya Wilaya ya Butiama, Karani Ruhumbika, anasema machimbo ya madini wilayani humo yameharibu mazingira, akinena: “Uoto wa asili ambao ulikuwapo kwenye milima ambayo inachimbwa madini haupo tena maeneo yamebaki kuwa jangwa,”

Anasema, wao kama serikali wamekuwa wakitoa elimu ya utunzaji mazingira, pamoja na kupanda miti ili kurudisha uoto wa asili kwenye milima inakochimbwa madini, lakini muitikio wake umekuwa mdogo.

Ruhumbika anasema, mipango ya serikali ni kuendelea kuhamasisha upandaji miti kwa kushirikiana na wadau, wakiwamo Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), ili kurudisha uoto wa asili uliopotea.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Sirorisimba katika Halmashauri ya Wilaya ya Butiama Ibrahim Mniko, anasema katika milima ya uchimbaji madini kwenye Mgodi wa Sirorisimba, uoto wa asili ulishapotea na wanachokifanya kwa sasa, wachimbaji ni kununua miti (mirunda) kwenye maeneo mengine na kuimarisha mashimo ya uchimbaji madini.

“Milima yote ambayo inachimbwa madini kwenye mgodi huu wa Sirorisimba, uoto wa asili ulishapotea miti yote ilishakatwa,” anasema Mniko.

Msimamizi wa Machimbo ya Majengo yaliyopo kijiji cha Nyamikoma wilayani Butiama, Lucas Wasinyo, anasema wachimbaji wadogo wanachimba madini kienyeji, hivyo suala la ukataji miti ni lazima, kwa sababu ya kuiweka kwenye mashimo na hawana njia nyingine mbadala zaidi ya miti.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Nyamikoma, Halmashauri ya Wilaya ya Butiama, Godluck Makaja, anasema wachimbaji wanakata miti sana, lakini kuhusu suala upandaji miti, anasema ni ngumu kwao sababu wao ni watu wa kuhamahama, wakifuata mahali madini yapo.

Meneja wa Mgodi wa Irasanilo, uliopo Magunga wilayani Butiama Robert Lucas, anasema katika Mgodi huo matumizi ya miti siyo makubwa sababu baadhi ya miamba haitumii miti (Matimba).

Karani wa Mgodi wa Irasanilo, Mugare Kitoki, anasema maeneo yote nchini yanayofanya shughuli za uchimbaji mdogo wa madini, suala la uharibifu wa mazingira kwa ukataji miti halikwepeki na kusema, kama kuna njia mbadala ya uchimbaji bila ukataji miti, wanaomba kupatiwa elimu hiyo.

DED BUTIAMA

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama, Revocatus Rutunda, anakiri machimbo madogo ya madini wilayani humo yameathiri mazingira, pamoja na kupoteza uoto wa asili kwenye milima inakochimbwa madini, miti ikiteketea.

Anasema Halmashauri ya Wilaya ya Butiama, sasa kuna migodi mingi inayochipukia na wachimbaji hawana elimu ya kulinda mazingira, ndiyo sababu ya uharibifu wa mazingira na ukataji miti, umekuwa mkubwa hata kupoteza uhalisia wa uoto wa asili.

“Halmashauri tumekuwa tukijitahidi kupanda miche na kuisambaza ili ipandwe na kurudisha uoto wa asili na takwimu za mwaka jana tulipanda miti milioni 1.6, lakini suala la upandaji miti na ukuaji ni kitu kingine, tulipoifuatilia miti hiyo baadhi tulikuta imelishwa na mifugo,” anasema Rutunda.

Pia, anataja sasa wamepata wafadhili kutoka asasi ya Global Resource Alliance, wanaopanda miti katika milima miwili ya Kigoro na Mwikoro, ili kurudisha uoto wa asili, huku na wao kama serikali wakiendelea kuhamasisha upandaji miti, kupitia pia maadhimisho ya sikukuu ya mkoa, Mara Day, ya utunzaji mazingira kwa kupanda miti.

“Elimu bado inahitajika sana ya utunzaji wa mazingira na kuzuia mabadiliko ya tabianchi, kwa historia ya zamani katika wilaya hii ya Butiama, milima yote ilikuwa imefunikwa na miti, lakini baada ya kuanza shughuli za uchimbaji madini milima yote ipo wazi,”anaongeza Rutunda.

Anataja mikakati mingine ya serikali katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira, ni kutunga Sheria ndogo kwa kila kijiji na akibainisha kuwa, tayari kuna vijiji viwili vya Kamgendi na Lyamisanga, ambavyo tayari wameshatunga sheria ndogo, mara baada ya kuona uharibifu wa mazingira unakuwa mkubwa.

KUTOKA TFS

Meneja Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Halmashauri ya Wilaya ya Butiama, Hafidh Saidi, anasema katika maeneo ya machimbo wilayani humo, miti mingi na uoto wa asili umeshapotea, kutokana na ukataji miti.

Anasema, TFS tayari wameshaanza programu kwa kushirikiana na serikali kupanda miti ili kurudisha uoto wa asili na mwezi Aprili, mwaka huu watafika kwenye maeneo yote ya machimbo wilayani Butiama, ili kutoa elimu kwa wachimbaji ya upandaji miti.

“Suala la upandaji miti ni jingine na kuikuza ni suala jingine, kabla ya kuanza kupanda miti kwenye maeneo ya machimbo, lazima tufike kwanza kutoa elimu kwa wachimbaji na baada ya hapo ndipo tupande ili itunzwe na kukua,” anasema Said.

OFISA MIRADI

Ofisa Miradi kutoka Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT), Clay Mwaifani, anasema tatizo lipo kwenye maeneo mengi ya machimbo, madogo juu ya uharibifu wa mazingira ni ukosefu wa sheria ndogo ngazi ya vijijini.

Anasema kuwapo sheria hizo ndogo kutakuwapo na uwajibishaji hasa kwa watu ambao wanaharibu mazingira, pia muitiko wa upandaji miti utakuwa mkubwa sababu ya adhabu.

Mwaifani anasema pia sheria zipo zinasema ‘kata mti panda mti’na kutoa ushauri katika maeneo ya machimbo, sheria hiyo inapaswa iongezewe makali kidogo, ukikata mti mmoja panda miti 30 ndiyo italeta tija na kuzuia uharibifu wa mazingira.

Mwisho.

 

Picha;

  • Muonekano wa machimbo katika Mgodi wa Madini ya Dhahabu, Sirorisimba, uliopo wilaya ya Butiama mkoani Mara, ukionekana jinsi ulivyokatwa miti. PICHA: MARCO MADUHU.

Top of Form

Bottom of Form

Top of Form

Bottom of Form