Shida kubwa inaelezwa ni kwa wauguzi na wakunga hao kushindwa kuzingatia maadili, wakijiegemeza katika vitendo viovu vya kujali maslahi yao, kuliko anachopaswa kutumikia mgonjwa.
Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania (TNMC), nalo katika hilo halijabaki kimya, limeamua kuchukua hatua dhidi ya malalamiko hayo, kwa kufuatilia kinachotokea ikichukua hatua dhidi ya watendaji mabaya, kadri inavyobidi.
Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania (TNMC), Agness Mtawa, anasema vitendo vya uvunjifu wa maadili, pamoja na kuwapo wauguzi na wakunga ‘vishoka’ wanaojiingiza katika taaluma hiyo, bado ni kikwazo cha tija katika sekta ya afya nchini.
Agness ameiambia hadhira iliyohudhuria mahafali ya saba, katika utoaji wa vyeti vya usajili na leseni kwa wauguzi na wakunga zaidi ya 1,000 waliofaulu kwenye mitihani ulioandaliwa na baraza hilo, jijini hapa.
“Pamoja na mafanikio tuliyoyapa, bado zipo changamoto mbalimbali, ikiwamo vitendo vya uvunjifu wa maadili kwa wauguzi na wakunga. Pia lipo tatizo la watu ambao siyo wanataaluma kuingilia taaluma yetu,” anasema.
Hapo anasisitiza kwamba wauguzi na wakunga wanapaswa kuzingatia maadili, ili kuondoa malalamiko ambayo yamekuwa yakijitokeza katika maeneo mbalimbali, ili kuisaidia serikali kupunguza vifo vya mama na mtoto.
“Sisi tutaendelea kuchukua hatua kwa muuguzi au mkunga yeyote ambaye atabainika kuwa amekiuka maadili kwa kumfuta kwenye usajili wetu,” anatahadharisha.
WALIOVUNJA MAADILI
Vilevile, anasema tangu mwaka 2016, wauguzi na wakunga 50 walibainika kuvunja maadili ya utumishi wa umma, kati yao wanne walifutiwa usajili na kupokonywa leseni, huku wengine wakipewa karipio kali.
Pia anataja kuwapo kero ya wauguzi na wakunga ‘vishoka’ wanaotumikia fani, akifafanua: “Bado wapo wananchi ambao wanajifanya wanataaluma hii na kutoa huduma bila ya kuwa na vigezo. Hili ni kosa la jinai!
“Ambao tumekuwa tukiwabaini tumewachukulia hatua za kuwapeleka mahakamani na wengine tayari wameshafungwa vifungo mbalimbali,” anasisitiza Agness.
Kuhusu hatua za ziada kukabili hali hiyo, mkurugenzi huyo wa uuguzi anafafanua kwamba, hadi sasa baraza lao limeshaandaa mfumo wenye namna unaowawezesha waajiri wote kuhakiki usajili wa wauguzi na wakunga wote nchini.
“Mfumo huu unao uwezo wa kubaini muuguzi au mkunga aliyesajiliwa na asiyesajiliwa, hivyo nitoe wito kwa waajiri kufanya uhakiki kupitia mfumo huu mara kwa mara, ili kukabili changamoto ya wasio wanataaluma kujipenyeza,” anasema.
Anataja hadi sasa kuna wauguzi na wakunga 55,000 waliosajiliwa nchini na wenye leseni hai wako 42,000, wakitoa huduma katika vituo mbalimbali vya serikali na binafsi.
Kiongozi huyo wa wauguzi anataja changamoto nyingine, ni wauguzi wengi kushindwa kuhuisha leseni zao kwa wakati kinyume na miongozi ya baraza hilo.
MAMLAKA YA UUGUZI
Mkurugenzi wa Uuguzi na Ukunga Wizara ya Afya, Ziada Sellah, anawataka wauguzi na wakunga nchini kuacha tabia ya kuchagua maeneo ya kufanya kazi, akiwaasa wanapaswa kufahamu wahitaji wa huduma zao wako nchi nzima, hivyo hawana wasiishie kuchagua maeneo ya mijini pekee, kuwa pa kufanyia kazi.
Mwenyekiti wa Baraza hilo, Prof. Lilian Mselle anaahidi wataendelea kuchukua hatua kwa mtumishi yeyote atakayeoneka kuitia doa taaluma hiyo, kwa kuchangia uvunjifu wa maadili.
Prof. Mselle anasema: “Lengo la Baraza la Uuguzi na Ukunga kuanzishwa mwaka 1953 ilikuwa kusimamia maadili kwa kada hii, ili wananchi wapate huduma bora za afya.”
Anasema, baraza hilo limeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kinidhamu kwa wauguzi na wakunga, ikiwamo kuwafutia leseni na kuwafuta kwenye daftari la usajili waliobainika kuwa na hatia.
NAIBU WAZIRI AFYA
Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel, anasema katika mwaka wa fedha 2023, serikali imetenga Sh. bilioni nane kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kufanya kazi kwa wauguzi na wakunga nchini, Ikiwa ni pamoja na kuwasomesha kuwaongezea ujuzi.
Anasema, serikali inatambua umuhimu wa wauguzi na wakunga katika sekta ya afya, hivyo kuna haja ya kuwekwa mazingira mazuri ya ufanyaji kazi ili kuendelea kutoa huduma bora za afya katika maeneo mbalimbali.
“Takribani asilimia 60 ya watumishi waliopo katika sekta ya afya ni wauguzi na wakunga, hivyo hatuna budi kuweka mazingira mazuri kwa kuboresha mazingira ya kazi pamoja na kuboresha maslahi yao binafasi,” anasema Dk. Mollel.
Rai yake kwa wauguzi na wakunga nchini ni kufanyika kazi kwa kuzingatia maadili, miongozo, kanuni na sheria, ili wamudu kutoa huduma bora kwa wananchi, hata kwa kupunguza malalamiko yaliyopo.
“Pamoja na kuboresha mazingira ya kazi, wauguzi na wakunga mnapaswa kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma, ili kuisadia serikali kutoa huduma bora na kupunguza vifo vya mama na mtoto,” anaeleza.
Naibu Waziri Mollel, anawataka madaktari kufanya kazi kwa ushirikiano na watumishi wa kada ya uuguzi na ukunga, ili kuleta tija, hata kuifikia azma ya serikali kutoa huduma bora za afya kwa wananchi wake.
“Sisi madaktari tumekuwa watu wa kujiona ndiyo kila kitu, bila kujua kuwa bila wauguzi na wakunga hatuwezi, wauguzi wakikosea ndiyo sisi Wizara ya Afya, tutapiga hatua katika malengo tuliyojiwekea,” anasema.