Msemo huo wa wahenga unaakisiwa na taasisi za kutetea haki za wanawake, kwa kuwaandaa mapema watiania watakaogombea uongozi kwenye uchaguzi mkuu 2025.
Miongoni mwa taasisi wadau za Zanzibar kama Chama cha Wanahabari Wanawake (TAMWA) Jumuiya za Wanasheria Wanawake (ZAFELA) na ile ya Wanawake Wenyeulemavu (JUWAUZA).
Taasisi hizo zimeanza kuwapa elimu ya uongozi wanawake takribani 100 ikiwaandaa miaka miwili kabla ya uchaguzi mkuu wa 2025 ili kuongeza ushawishi na ushiriki wa kinamama majimboni na idadi ya wanawake ndani ya vyombo vya kutunga sheria.
Wanaonolewa ni kutoka vyama mbalimbali vya siasa vilivyosajiliwa ili ifikapo mwaka 2025 kuvishinda vikwazo vinavyoweza kujitokeza wakisaka nafasi za uongozi wa kisiasa.
WANACHOFUNZWA
Rushwa ni miongoni mwa wanayofunzwa ,Ofisa Uhusiano wa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) Mwanaidi Suleiman Ali, anasisitiza :”Msikubali kushawishika kwa kupokea hongo zinazotolewa na wanaume ili kuwaachia nafasi.”
Anasema uzoefu unaonyesha kuwa wakati wa uchaguzi huo, wanawake majasiri hukabiliwa na nguvu kubwa ya wanaume wenye fedha nyingi kuwarubuni ili wajitoe na kuwaachia wanapoona wapinzani hao wanakubalika na ni tishio kwao.
Aidha, anaeleza kuwa wapo wanaume wagombea hutumia makundi ya vijana wakiwamo pia wanawake kuwapa mlungula au rushwa, fedha na zawadi kuwaondoa kijanja.
Hata hivyo, kwa upande mwingine anawaomba wanawake waamke na kukataa rushwa ya ngono wanapodaiwa na wanaume wenye maamuzi katika vikao vya kupitisha majina ya wagombea wa nafasi za uongozi katika vyama vyao.
Mwanaidi, anasema ni vyema wanapoona dalili za vishawishi kama hivyo wavikatae mapema na kuripoti ZAECA ili kuwawekea mtego wanaohusika na rushwa zote ikiwamo ya ngono kwa ahadi ya kupitishwa majina yao.
“Ukitakiwa rushwa ya ngono, tumia akili ukusanye ushahidi baadae ripoti ZAECA. Iwapo utajirahisisha kwa tamaa ya kupata uteuzi na kama hukupewa ndio uje ulalamike kwetu, hatutakuwa na namna ya kukupigania maana tunachunguza mchakato mzima ikiwamo mawasiliano ya simu,” anabainisha.
“Umefika wakati wanawake wabadilike na kukwepa mitego ya wanaume wenye uchu, kwani uongozi na cheo hupangwa na Mungu, si kujidhalilisha bali ujasiri na kupambania haki yao.” Anawaambia.
“Kwa mujibu wa sensa ya Tanzania mwaka jana wanawake tupo asilimia 51.Ni jeshi kubwa na tunaweza kuongoza na kushika nafasi za maamuzi kwa njia za haki bila kushusha utu na heshima yetu.,” anasisitiza Mwanaidi.
Baadhi ya washiriki wa warsha hiyo walikiri kuwepo ugumu katika kupata nafasi za kugombea, wingine wakidai mfumo dume ni tatizo hata ndani ya vyama vyao.
Amina Rashid Salum, kutoka Chama cha Wananchi CUF Zanzibar, akizungumzia kuhusu rushwa, anashukuru ZAECA kuwaonyesha njia ya kupata haki, ingawa kuna wasiwasi wa kuwepo muhali hasa kadhia hizo zinapowahusu wenye madaraka.
Amina katika uchaguzi wa 2020 aligombea uwakilishi jimbo la Shaurimoyo, lakini hakupata nafasi, anasema vigogo wanaotuhumiwa na rushwa hakuna hatua zinazochukuliwa hata wanaposhikwa na ushahidi.
Aidha, anaitaka ZAECA kuingia hadi ndani ya chaguzi za vyama vya siasa ambako anadai rushwa imeota mizizi na hata wanapotaja ushahidi, kesi hizo hufumbiwa macho.
Anaeleza uzoefu wa rushwa kuwa wakati akigombea nafasi hiyo mpizani wake mmoja alimfuata kwa kutaka kumrubuni akiahidi kumpatia Shilingi milioni 100, alizozikataa.
“Baada ya kuniona ni tishio alitaka kunirubuni nikamwambia sirubuniwi kwa fedha wala zawadi kama doti za kanga na sabuni”anasema Amina.
Mratibu wa kuwawezesha wanawake katika uongozi (SWIL) unaofanikishwa na Norway, Mariam Ame Chum, anasema lengo lao ni kuwaamsha na kuwaandaa kimbinu wanawake wenye nia ya kugombea uwakilishi, ubunge na udiwani mwaka 2025 ili kuweka mazingira wezeshi ya kufikia 50/50 katika uongozi.
“SWIL imeandaa mafunzo haya ili kuwajengea uwezo wanawake na kuwaondoa hofu ili wajitambue, na tunatarajia wakati ukifika watakuwa wameiva sawasawa,” anasema kutoka TAMWA.
Anasema kutokana na jitihada za TAMWA inayosimama utetezi wa haki za wanawawake, hali katika vyombo vya maamuzi imeanza kubadilika, tofauti na ilivyokuwa miongo kadhaa iliyopita wakati Tanzania ikianza mfumo wa vyama vingi.
Mariam pia aliwataka wanaume kuachana na mitazamo hasi kwamba pahala pa mwanamke ni jikoni pekee, akisema katika dunia ya sayansi na teknolojia, wamejitokeza wanawake wingi wanaofanya makubwa kwa maslahi ya mataifa yao.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) Salim Suleiman Ali, anawataka wanawake wenye nia ya kugombea uongozi kutengeneza mazingira sasa ikiwa hasa kufanyakazi kwa karibu na jamii.
Anasema, maandalizi hutakiwa kuanza mapema, ili kujua mipango, mikakati, njia za kupita ili kuwafikia wapigakura.
Anasema haiwezekani mwanamke mgombea kutojishirikisha vyema ndani ya chama chake na kugonjea miezi miwili, kabla ya uchaguzi mkuu ndio ajitokeze.
Anazungumzia rushwa ya ngono au fedha akisema ni jambo mojawapo la kukwepa kwa mgombea wanamke, kwasababu humshushia heshima ndani ya chama na jamii.
WENYEULEMAVU
Wanawake wenye mahitaji maalumu hawakuachwa nyuma katika kuandaliwa kwa ajili ya kugombea nafasi za uongozi, JUWAUZA ikiwapa kipaumbele.
Yumna Manga ni miongoni mwa wanawake wenyeulemavu anasema ili kuimarisha hali za watu wenye ulemavu lazima kuwepo na ushiriki wa kutosha kwenye vyombo vya maamuzi hasa vya kutunga sera na sheria.
Aidha, anasema uwezo wa kifedha ni changamoto kwa wanawake wenyeulemavu kwenye ushiriki wa siasa kwa sababu kampeni zinahitaji gharama.
“Watu wenyeulemavu tumeachwa nyuma mara tatu zaidi ya mtu mwingine asiye na mahitaji maalumu wengi wetu tunachangamoto ya fedha hivyo tunatoa wito kwa wananchi watuamini kiuwezo ni sio hali zetu”anasema.
Yumna anasema katika uchaguzi wa mwaka 2020 aligombea ubunge viti maalum hivyo amejifunza vitu vingi ikiwamo jamii, inahitaji uelewa wa masuala ya watu wenye ulemavu kwa sababu inamuhukumu kutokana na hali yake na si uwezo wake.
“Hatutaki tu kupata nafasi ya viti maalum tunataka majimbo kuongoza wananchi watuamini tunahitaji kuyasemea mahitaji yetu sisi ndio pilipili inatuwasha”anakumbusha,
Mkurugenzi wa asasi za kiraia -AZAKI Zanzibar Ahmed Abdallah anazipongeza jumuiya za asasi za kiraia kwa elimu wanayotoa kwa wanawake kuhusu nafasi za uongozi ili kuhakikisha wenye ulemavu wanakuwa mstari wa mbele kushiriki uchaguzi mkuu.










