Tunafanya hivyo, bila hata kufungwafungwa. Mazingira hayo yamewekwa na Rais wa Sita, Dk Samia Suluhu Hassan a.k.a Chifu Hangaya, kwa anachoamini katika uhuru wa kujieleza, uhuru wa kutoa na kupata habari.
Chifu Hangaya ndiye aliyeamua vyombo vya habari vikiwamo vijitivii vilivyokuwa kifungoni, kuachwa bila masharti na viendelee kufanya kazi zao kama kawaida, lakini vikijichunga katika kufuata sheria.
Hata hivyo,tunaonekana nasi kujisahau na kudhani kuwa ukishapewa uhuru, basi hutafuatiliwa tena na kujikuta tukifanya mambo mengine ambayo hata hayana msingi. Tukifuatilia mengine na kuyarusha huku tukijua hayana mashiko kwa jamii.
Angalia hivi karibuni, kaibuka binti mmoja hivi mbele ya tivii moja, akihanikiza kuwa alikuwa ziarani mbinguni alikokutana na Mungu na kushuhudia maghorofa yaliyojengwa huko yakiwa marefu na ya dhahabu tupu.
Nasi bila kutambua, bila kujua tunafanya nini, tukampa muda kwenye vijitivii kuuhadaa umma tena wa dunia nzima, kwamba ni mtu wa kwanza kuonana na Mungu na kukaa naye meza moja, sijui alikula naye nini?
Wapo walioshabikia video ile, lakini wengi bila shaka waliiponda na kuhisi pengine kuna tatizo la afya ya akili kwa anayesimulia mambo ambayo hayawezekani kabisa. Sina uhakika kama alieleza alitumia usafiri gani kufika mbinguni!
Kwa wale tuliokereka na mahojiano hayo, tunaiunga mkono Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa onyo ililotoa kwa vyombo vya habari, kuhusu kurusha maudhui kama hayo kwa jamii ambayo kwa kweli hayana staha.
Hayana staha kwa sababu yanaingilia imani za kidini, kweli tuaminishwe kuwa fulani anaweza kwenda Mbinguni akakutana na Mungu na kukaa naye meza moja jamani? Wakristo na Waislamu tunaamini Mungu mmoja, hii si kashfa kwetu?
Hivi kwa kujiita nanihii ndipo atupande vichwani na imani zetu na sisi kumpa wasaa wa kuidanganya Dunia? Tunawashukuru TCRA kwa kuingilia kati na kuonya, ili wasiibuke mitume wengine bandia kama hawa wakapewa fursa ya kutuvuruga.
Kwa kuwa TCRA wamekemea dhidi ya mawazo haya fikirika yanayogusa imani za kidini, sisi wenye vyombo hivi vinavyosambaza habari na taarifa haraka kwa jamii, tujiangalie tusikaribishe watu tusiowajua kiimani na kiakili na kuwapa fursa ya kututukanisha na Mungu.
Hilo lisiishie hapo, bali pia majumba ya ibada ambayo hivi sasa yanaibuka kama uyoga nchini yafuatiliwe, kwani nayo yanamiliki vijitivii vya aina hiyo na kurusha mawazo fikirika yakiwamo ya uponyaji ambao ni bandia.
Tuna makanisa-si misikiti, yanayohubiri uponyaji, huku mengine viongozi wao wakijiita maaskofu, wakijimwambafai kufufua wafu na kuendelea kuwapora waumini wao fedha, kwa kinachoitwa sadaka, huku wakiwauzia pia maji, mafuta na chumvi kwa bei mbaya.
Kwa upungufu wa uelewa wa baadhi yetu, tumekuwa tukipoteza raslimali zetu na hata maisha kwenye majumba hayo kwa imani za kuongoka na kuponywa, lakini tukiendelea kubaki na matatizo yetu bila unafuu wowote, huku maaskofu hao wakitegeshea walemavu bandia na kudai kuwaponya.
Tanzania tunaweza kujifunza kwa mataifa mengine ambayo zamani yalikuwa nyuma na leo yako mbele na kuyatumia kama mifano, hasa linapokuja suala la kusimamia jamii. Kuna mataifa jirani tu yanaonekana kutuongoza hivi sasa, kwa mambo mengi na kulazimika kujifunza kwao!
Nakumbuka miaka mitano iliyopita, nchi jirani ilifunga nyumba za ibada idadi ya mamia katika mji mkuu wao, kwa walioshindwa kufuata masharti ya usafi na usalama, tunashindwa nini kufuatilia pale tunagundua au kuthibitisha upotoshaji wa aina yoyote?
Tuhakikishe tunaepukana na mawazo hayo ya kuonana na Mungu, au mengine yasiyo na uhakika au yenye mwelekeo wa kupotosha. Wanahabari nasi kabla ya kurusha mambo haya, ni vema kuchungulia nyuma ya pazia kuna nini na kuwa na uhakika. Tusipotoshwe na wapotoshaji hawa. Alamsiki!










