Watanzania zaidi 800 katika foleni ya kupandikizwa figo

16Mar 2023
Yasmine Protace
DAR ES SALAAM
Nipashe
Watanzania zaidi 800 katika foleni ya kupandikizwa figo

UGONJWA wa figo unatajwa kuwa wa hatari na hata kuchangia baadhi ya vifo, kwa wanaochelewa kupata matibabu.

Pia, ugonjwa huo unawafanya watu kutumia gharama kubwa kwa ajili ya matibabu.

Ni Shida inayochangiwa na baadhi ya watu kushuka kimapato, kutokana na kutumia gharama kubwa katika matibabu yake.

Ugonjwa wa figo unaanza kwa hatua mbalimbali na mpaka hatua ya mwisho, mgonjwa anakuwa katika hali mbaya. Hiyo ni pale figo inashindwa kufanya kazi yake inavyopaswa, ikishughulika polepole.

Kiafya inafafanuliwa, watu wengi huwa hawaonyeshi dalili za kupona ugonjwa huo, hadi pale figo zimeharibika sana, huku kibaiolijia, figo ina kazi nyingi, ikiwamo kutoa uchafu na maji mwilini, kuzuia shinikizo la damu, kusawazisha kemikali za mwili na kuzalisha chembe za damu nyekundu.

Serikali imekuwa ikielimisha jamii namna ya kujilinda na magonjwa ya figo, kunakuwa Siku ya Figo kimataifa, inayokuwa kila mwezi Machi. Hata hivyo, inaonekana baadhi ya jamii hazina uelewa wake sahihi. Inafafanuliwa na takwimu za kiserikali kwamba, kuna Watanzania zaidi ya 800, wanahitaji huduma za kupandikizwa figo.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, akiongea katika jengo la wagonjwa wanaosafisha figo, katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam, anasema tafiti zimebainisha takribani Watanzania kati ya 5,800 mpaka 8,500, wanahitaji kusafisha damu (dialysis) au huduma za kupandikizwa figo.

Akizungumzia katika maadhimisho ya Siku ya Figo Duniani anasema kuwa, hadi kufikia Januari 31 mwaka huu, kuna wagonjwa 3,250 wamepata huduma ya kusafishwa damu  na wagonjwa 335 wamepandikizwa figo.

“Kati ya wagonjwa waliopandikizwa figo, wagonjwa 103 wamepandikizwa nchini, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili imepandikiza wagonjwa 70 na Hospitali ya Benjamin Mkapa Dodoma imepandikiza wagonjwa 33,”anasema Ummy.

Anaongeza kuwa serikali imejipanga kuweka jitihada za kudhibiti na kuzuia ugonjwa wa figo na magonjwa yasiyoambukiza kwa ujumla, kwa kuimarisha afya za kinga kwa jamii.

“Naomba nikumbushe umuhimu wa kubadili mtindo wa maisha kwa kufanya mazoezi, kuepuka matumizi ya tumbaku na bidhaa zake, kupunguza matumizi ya vilevi na kuzingatia ulaji wa mlo kamili, wenye mbogamboga na matunda ya kutosha, ili kuimarisha kinga ya mwili dhidi ya magonjwa,”anasema.

Waziri Ummy anahimiza kupunguza matumizi ya chumvi, sukari na vyakula vyenye mafuta mengi na kuzingatia unywaji wa maji ya kutosha walau lita 2.5 kwa kila siku, huku kukiwapo uzingatiaji matumizi ya dawa ambazo hazijatolewa maelekezo ya kitaalamu na daktari.

Anaongeza kuwa, takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinabainisha asilimia 10 ya watu wote duniani wanaishi na ugonjwa sugu wa figo na zaidi ni kwa wenye umri zaidi ya miaka 75, wastani wa nusu yao wana tatizo hilo.

Kuhusu utekelezaji Sera ya Afya ya Mwaka 2007 na tatizo figo, Waziri Ummy anasema serikali imeanzisha huduma za uchujaji damu kwenye hospitali za mikoa minane, kwa kuzipatia mashine 49 maalum za kazi hiyo, pia kukarabati majengo kwa gharama ya Sh. bilioni 2.8.

Anakumbusha kuwa, Tanzania huungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Figo Duniani kila Alhamisi ya Wiki ya Pili ya mwezi Machi, Jumuiya ya Kimataifa ya Nefrolojia (ISN), kwa kushirikiana na Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Figo Duniani (IFKF), iliyoanzisha maadhimisho hayo yaliyofanyika kwa mara ya kwanza mwaka 2006.

Kaulimbiu ya mwaka huu ni ‘Afya ya Figo kwa Wote- Kujitayarisha kwa yale yasiyotarajiwa kusaidia walio hatarini,” ikilenga kuongeza ufahamu na elimu ya afya ya figo na kuhamasisha wananchi kujitokeza kupima afya zao.

 

 

Top of Form

Bottom of Form

Top of Form

Bottom of Form