Wanawake wa kada mbalimbali wanapaza sauti zao wakieleza namna ambavyo teknolojia ikitumika kikamilifu inaweza kumkwamua mwanamke na jamii kwenye umaskini.
Pamoja na mengi yanayozungumzwa kuhusu teknolojia, wanawake Tanzania wanamwangalia mwanamama, mkuu wa nchi, Rais Samia Suluhu Hassan, kwa namna ya kipekee.
Anaanza, mwanaharakati wa Haki za Binadamu Dk. Helen Kijo-Bisimba, anayemtaja Rais Samia kama mwanamke wa shoka na wa kuigwa, akisema utendaji wake umedhihirisha utofauti wa namna ya kushughulikia mambo kati ya kiongozi mwanaume na mwanamke.
Anasema wakati wa uchaguzi mkuu wa vyama vingi mwaka 1995, mfumo huo ulichukuliwa kama ni uadui, dhana ambayo anasema awamu ya Rais Samia inaifuta.
“Hatua ya mkuu wa nchi na Mwenyekiti wa CCM inayoongoza dola kujumuika kwenye jukwaa la wanawake wa chama cha upinzani CHADEMA, imeongeza maana kubwa zaidi kwa ustawi wa nchi na utengamano kati ya siasa na maridhiano nchini.
Itakumbukwa kwamba, Jumatano iliyopita, Rais Samia alijumuika na kuwa mgeni rasmi kwenye mkutano wa Baraza la Wanawake wa CHADEMA (BAWACHA), mkoani Kilimanjaro, ambako alialikwa kwenye maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani.
Anasema pamoja na kwamba mfumo wa vyama vingi vya siasa ni suala la kikatiba, katika hali ya utendaji mambo ni tofauti kwani umekuwa kama uadui.
“Nimemsikia anasema anataka kujenga nchi iliyo pamoja, na ndivyo inavyotakiwa. Taifa gani unaishi unaogopa kuingia kwenye vyama hasa upinzani?”Anahoji.
TOFAUTI KIUONGOZI
Dokta Hellen anamsifu Rais kuwa ni kiongozi wa raia wote hivyo anawajibika kuwakumbatia wote bila kujali itikadi za vyama, dini wala makabila.
“Anachofanya Rais nimemfurahia na nikasema ametuonyesha tofauti ya uongozi kati ya mwanamke na mwanaume na hii inaweza kumjengea msingi madhubuti, umahiri na heshima kubwa sana,” anasema mwanasheria huyo aliyeongoza Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu.
Anagusia kufufua mchakato wa katiba akieleza kuwa anatamani Rais Samia aongoze ajenda hiyo na kuihitimisha kwa manufaa ya nchi akisema:
“Ningetamani aliongoze hilo ili aweke alama ya Rais mwanamke kwamba ameweza kufanya kitu kama hiki. Atuletee jambo la kitofauti, mbadala na vitu ambavyo vimewahi kutokea.”
MIAKA 2 UONGOZINI
Anazungumzia miaka miwili ya Rais Samia madarakani akisema anaingia kuongoza nchi wakati muafaka, tena katika kipindi kigumu na kwamba kile ambacho wananchi walikihitaji amekifanya.
“Kwa ile hali ambayo tulikuwa tumefikia, nadhani alikuwa ni mtu muafaka mwenye kuleta suluhu na kusawazisha ili hali iwe bora” anasema.
Anaongeza kuwa Rais Samia amefanikiwa kuachia baadhi ya watu ambao walikuwa wamefungwa na kurudisha akaunti za fedha zilizokuwa zimefungwa jambo ambalo anaeleza kuwa ni zuri na ni haki ya watu.
Hata hivyo, anasema wananchi wana mambo ambayo wangetamani yafanyike haraka na kwamba ni kwa kuwa wameyadai kwa muda mrefu.
“Suala kama la katiba na sheria mbaya ziondolewe. Tunatamani kama anaweza afanye sasa maana akija mwingine tunaweza tukarudi kule kule. Kwa hii miaka miwili tumekuwa na uhuru fulani mzuri sana,” anasema.
Kuhusu maendeleo, Dk. Hellen anasema miradi mikubwa inaendelea kutekelezwa jambo ambalo linadhihirisha kwamba mwanamke anaweza kufanyakazi kwa ukamilifu na utimilifu.
Anaeleza kuwa pamoja na kwamba baadhi ya watu wanalalamikia mikopo inayochukuliwa na serikali, utekelezaji wa miradi mikubwa unaonyesha fedha hizo zinakopelekwa na si mikopo kwa hasara.
“Tukiweza kupata umeme nchi nzima kitakuwa ni kitu kizuri kama ambavyo tunaona mtandao mkubwa wa barabara za lami. Tulikuwa tunaambiwa tutatoka Mtwara kwa barabara hadi Bukoba tukawa tunashangaa lakini vitu kama hivyo vinawezekana,” anasema.
Mkurugenzi wa Shirika la Wanawake katika jitihada za Kimaendeleo (WAJIKI), Janeth Mawenza, anampongeza Rais Samia kwa kuongea na wanawake kupitia jukwaa la BAWACHA, akisema ni chachu ya kuleta mabadiliko ya uongozi ndani ya jamii.
Anasema kitendo hicho kinajenga mahusiano bora miongoni mwa wananchi na kwamba kitaamsha nguvu ya mashauriano na kuwaleta Watanzania pamoja na kwamba amekwenda kuimarisha ustawi wa vyama vya siasa nchini na amekuja kuimarisha mahusiano yanayojengeka katika misingi ya uongozi bora katika nyanja zote.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wanawake Wakiislam Tanzania, Shamim Khan, anapongeza hatua hiyo ya Rais Samia akieleza kwamba amefanya kitendo cha kidemokrasia ambacho ni cha kudumu.
“Ndiyo demokrasia; yeye kachaguliwa na wanawake wote bila ya kujali chama.Ni mwanamke hodari. Malumbano yapo katika mawazo na hii ndiyo demokrasia,” anasema Shamim, akimwelezea Dk. Samia kama mwanamke anayefanya mambo mengi kwa manufaa ya makundi yote .
“Ni mwanamke shupavu, hana majivuno na mimi nasema mwaka 2025 tusimwache. Na ametuonyesha njia wanawake wengine kwamba tuthubutu. Elimu anayo, uwezo anao na ni mwanamke,” anasema.
Anasema kwa utendaji wa Dk. Samia, hana wasiwasi kwamba mwaka 2025 ‘njia ni nyeupe’ kwake kwa kuwa ameonyesha uwezo mkubwa.
Anasema serikali ya awamu ya sita imegusa sekta zote akitolea mfano wa afya, miundombinu, maji na nishati hivyo anawataka wanawake na wanaume wenye umri wa kushiriki uchaguzi wasimwache Rais Samia.
Mwanamke mbobevu wa Hisabati, Profesa Veridiana Masanja, anamwelezea Dk. Samia kama kiongozi wa mfano akitolea historia ya Chama Cha Demokraisa na Maendeleo (CHADEMA) namna ambavyo maandamano yake yalivyogharimu maisha ya wananchi.
Anasema maandamano yalizorotesha ustawi wa mambo mengi na kwamba awamu ya tano kuzuia mikutano ya hadhara ilileta butwaa kwa vyama vya upinzani jambo ambalo lilisababisha ufa kati ya wananchi na serikali.
Anatoa mfano kwamba jimbo la Arumeru Mashariki ambalo lilishikiliwa na upinzani liliathirika na maandamano ya CHADEMA na hawakupata maendeleo kutokana na chama hicho kususia vikao mbalimbali vya serikali.
“Nampongeza sana Rais Samia kwa kukubali mwaliko wa BAWACHA…hatuwezi kusema sisi ni nchi ya amani kama hatuko tayari kusikiliza reconciliation (maridhiano), hata ndugu wa tumbo moja huwa wanagombana lakini mazungumzo huwaleta pamoja,” anasema.
Anasema alichokifanya Rais Samia ni hatua muhimu ambayo itaboresha mambo mengi nchini.










