Eneo la kwanza, inaishangaa namna Tanzania ilivyohimili misukosuko ya uchumi duniani, hali kadhalika ikitoa baadhi ya majibu ya siasa ya uchumi kitaifa yanayohojiwa nchini, kwa baadhi ya mambo yanayoshika uchumi nchini.
Toleo hilo la wiki hii linaloitwa Ripoti ya Kiuchumi ya Tanzania; Upatikanaji wa Majisafi kwa Maisha Bora na Umuhimu wa Kupatikana Mfumo wa Maisha Bora, ina ufafanuzi namna Tanzania ilivyomudu magumu ya kiuchumi kimataifa, kuanzia mwaka 2021.
Kimsingi, ni kipindi tangu Rais Dk. Samia Suluhu Hassan anaingia madarakani, dunia ikiwa katika misukosuko mingi, ikiwamo janga la ugonjwa Covid - 19, mahsusi ripoti ikielekeza angalizo kwa nchi za Kusini mwa Janga la Sahara.
Ripoti hiyo inafafanua kwamba wakati nchi jirani na Tanzania barani Afrika, uchumi wake ukishuka kwa wastani asilimia mbili za pato lao la taifa, hali ilikuwa kinyume Tanzania ikishuhudiwa uchumi wake unapanda kwa wastani wa asilimia mbili.
Hapo kuna juhudi za kiongozi mkuu wa nchi kupandisha uchumi wa nchi zimeushangaza utafiti wa Benki ya Dunia, hadi mwishoni mwa mwaka huo 2021 penye misukosuko, uchumi wa Tanzania ukaongezeka kufika wastani asilimia 4.3 na mwaka unaofuata 4.8, ilhali kukiwapo makadirio kufika mwaka huu, wastani huo utapanda kufika asilimia 5.3.
Benki ya Dunia inarejea hata penye mlipuko wa maradhi UVIKO-19 barani Afrika, baadaye kukutwa na vita baina ya Russia na Ukraine, inayotikisa uchumi wa dunia yote, Tanzania bado imekuwa katika nafasi nzuri barani Afrika.
Itakumbukwa hata athari za mlipko wa maradhi Uviko 19, umekuwa wa chini sana, kulinganisha na ilivyo kwa hata baadhi ya nchi jirani katika Afrika Mashariki.
Benki ya Dunia, inasifu hatua za serikali nchini katika ufanisi kwenye uchumi, biashara na huduma, mahsusi ikitaja maboresho katika shughuli za utalii, kufunguliwa mipaka ya biashara na mafanikio kwenye chanjo dhidi ya UVIKO 19, hata nchi haikuathirika sana.
Katika mbinu zake kukuza uchumi, Rais Dk. Samia mara baada ya kuingia madarakani, Machi 2021, alifanya ziara za kibiashara zinazofungua tija na milango ya biashara kitaifa katika nchi jirani na mbali, sasa zikitajwa kuwa na tija kubwa ka uchumi na biashara nchini.
Ziara jirani zenye tija kubwa katika biashara ya nchi, zinajumuisha katika mataifa kama; Kenya, Uganda, Malawi na Rwanda.
Itakumbukwa, katika Sekta ya Utalii, Rais Dk. Samia katika moja ya mikakati yake ya mwanzo kukuza Sekta ya Utalii, alishiriki sinema ya Royal Tour, ambayo inaonyesha mapinduzi makubwa katika sekta hiyo ya Utalii.
Sekta ya Utalii, ni moja ya maeneo makubwa katika mchango kwa uchumi wa taifa, ajira, na kuingiza fedha za kigeni.
Benki ya Dunia, katika ripoti yake hiyo inayozama kwenye maisha bora, kupitia huduma za maji na nyendo bora za kiuchumi, inafafanua kwamba kuwapo na misingi imara ya kiuchumi, ndiyo imekuwa siri kuu ya mafanikio ya nchi.
Hata kurejea hoja za ukinzani kisiasa unajitokeza, ikiwamo bungeni kuhusu kasi ya kupanda kwa bei ya vyakula na bidhaa za kilimo, Benki ya Dunia, imerejea ilichokiita ‘vikwazo vya nje’.
Katika hilo, ripoti hiyo ya wiki hii inajumuisha kudorora kwa kilimo kunakotokana na ukame ulioikumba nchi, kupanda bei ya mafuta ya petroli kimataifa, kulikosababisha usafiri wa shida na kupanda bei za vyakula.
Itakumbukwa, serikali ilishatoa ufafanuzi, ikianza na kilimo katika msimu uliopo ambao uko katika hatua ya mavuno, ikishauri wakulima kupanda mazao yanayohimili ukame katika msimu uliopo, kutokana na hali mbaya ya hewa.
Pia, baada ya kuwapo vita baina ya Ukraine na Russia, mara moja bei ya mafuta ilipanda kimataifa na hatua nchini ikalazimika kupandishwa bei ya petroli kulikotangazwa na serikali.
MFUMUKO WA BEI
Ni siku chache tu zimepita serikali ilitangaza kuwapo kasi ya mfumuko wa bei, chakula kikitajwa chanzo kikuu, hata kuchukuliwa hatua na serikali ya kukaribisha tani 90,000 za mchele kutoka nje, ili kukabili makali hayo ya bei.
Hata hivyo inaporejewa sura ya pili ya ripoti hiyo kimataifa, Benki ya Dunia inauweka kwenye uzani wa kundi la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), kwamba ina nafuu kubwa.
Kutokana na misukosuko ya kiuchumi, nchi wanachama wa SADC zina mfumuko wa bei kiwango cha asilimia 10, ikitolewa mfano wa taifa la Zimbabwe, ambako kunatajwa ni wastani wa mara mbili na nusu zaidi kwa hali iliyoko nchini (asilimia 240).
Hata kwenye maeneo ya kisekta ambayo yanaiwezesha Tanzania kuangukia nafuu ya kiuchumi na kupata sifa, imo eneo la vyakula kukitajwa kuwapo maboresho makubwa.
Katika mpango wa taifa na bajeti ya kilimo mwaka huu, Rais Dk. Samia akafanya mageuzi makubwa zaidi, kukiwapo bajeti ya kilimo ikielekezwa Sh. 751,123,280,000 katika mwaka uliopo wa fedha, kutoka Sh. 294, 162,071,000 za mwaka wa fedha uliotangulia, 2021/23 sawa na ongezeko la asilimia 255.
Kwa mujibu wa mapedekezo yaliyowasilishwa na kupitishwa bungeni, yanajumuisha wakulima kupata ruzuku ya mbolea na kuendelezwa kwa skimu mbalimbali za umwagiliaji, kupisha janga la ukame kwenye kilimo na uhaba wa mazao.
Pia, Rais Dk. Samia ni hivi karibuni akiwa jijini Dakar Senegal kuhudhuria kikao cha maendeleo ya Afrika, ambako aliwasilisha mada na ajenda mojawapo muhimu ikiwa kilimo, alifanya faragha na baadhi ya wawekezaji kimataifa, kuanzisha viwanda vya mbolea nchini, kukiendana na kupata majibu chanya.
Ripoti ya Benki ya Dunia inataja maeneo yaliyofanya vizuri kuinua utawala wa Rais Dk. Samia, yanajumuisha pia maeneo ya huduma za bima, makazi, sekta za fedha na teknolojia ya mawasiliano.
Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, eneo lingine la mapato ambalo linaonyesha mabadiliko ya uchumi kukua katika zama za Serikali ya Awamu ya Sita, inaangazia kwenye mapato yasiyo ya kodi.
Hapo inafafanua kwamba, katika mwaka wa fedha 2020/ 21 ilikuwa wastani wa asilimia 2/1, lakini yakapanda hadi kuwa asilimia 2.7 katika mwaka wa fedha uliofuata, 2021/22.
MAUZO YA NJE
Tangu aingie madarakani mwaka 2021, Rais Dk. Samia, mauzo ya bidhaa zilizozalishwa nchini zilifanya vizuri, nusu yake zikitokana na bidhaa migodini.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, bidhaa zilizozalishwa ambazo huchukua asilimia 20 ya bidhaa zote, mauzo yake yalipanda kwa asilimia 36 katika mwaka wa fedha 2021/22 kutoka asilimia 36 za mwaka wa fedha 2020/21, ikiwa na ishara zote za ukuaji maradufu. Huduma za utalii nazo zikafanya makubwa nchini, kukaribisha pato la taifa na fedha za kigeni.










