Huduma za mawasiliano ni za msingi katika maisha ya wananchi kwa vile zinagusa nyanja za kijamii, kiuchumi na kisiasa. Pia, mawasiliano yanawezesha kuhimili sekta mbalimbali ikiwamo afya, elimu, kilimo, uwekezaji, biashara na ajira.
Maeneo mengine ni benki na utalii, ambako kunaongezewa ufanisi wa kiutendaji sambamba na kutoa mchango mkubwa katika uchumi wa moja kwa moja kupitia sekta hizo.
Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Kundo Mathew, ametamka hayo akiwa katika ziara yake ya kukagua miradi ya mawasiliano, ubora na upatikanaji wa huduma za mawasiliano, na usikivu wa redio na uhakiki wa anwani za makazi wilayani Mafia, Pwani.
Anasema Wizara yake inabeba miundombinu yote ya mawasiliano nchini na sasa imeongezewa bajeti, kuakisi uhalisia wa kazi adhimu inayotakiwa kufanyika katika masuala ya TEHAMA nchini.
“ Bajeti ya wizara hii ilikuwa Sh.bilioni nane kwa mwaka lakini Rais Samia alivyoingia madarakani aliipatia Sh.bilioni 230,” anasema Kundo na kuongeza:
“Shilingi bilioni 230 maana yake ni miradi mingi zaidi ya ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano, ajira za moja kwa moja na miundombinu inapoimarika zaidi huduma za mawasiliano zinazidi kupatikana kwa urahisi na gharama zake zitaendelea kuwa nafuu.”
Kundo anasema, katika jitihada zinazofanywa na serikali katika uwekezaji ni kwenye miundombinu ya TEHAMA, katika bajeti ya mwaka 2022/23 serikali imetoa Sh.bilioni 145 kwa ajili ya ujenzi wa mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.
Anasema, hadi sasa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano umeunganishwa na nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo(DRC), ili kusaidia kutoa huduma pamoja na maeneo mengine ya mpakani.
Pia, anaongeza kuwa, mnamo Juni 26, 2021, serikali kupitia aliyekuwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk. Dorothy Gwajima, ilizindua Mpango Mkakati wa Sekta ya Afya wa Awamu wa Tano katika mkutano ulioshirikisha wadau wa sekta hiyo, alieleza mpango mkakati umejielekeza kuleta matokeo katika maeneo matano ya kimkakati.
Anataja malengo hayo ni kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya kwa kuendelea kujenga miundombinu, kuongeza watumishi, vifaa tiba, dawa na vitendanishi, kuimarisha utayari wa kujiandaa na kukabiliana na magonjwa ya mlipuko na dharura kwa kuboresha mfumo wa kutoa taarifa ya viashiria hatarishi, ushirikishwaji wa jamii, usafi wa mazingira.
Pamoja na udhibiti wa taka hatarishi, upatikanaji wa fedha, mabadiliko chanya ya tabia na ushirikishwaji wa sekta nyingine.
Eneo jingine ambalo serikali imejielekeza ni kuendelea na jitihada za kuboresha kitita cha huduma za afya katika ngazi ya msingi na huduma za rufaa, huduma za utengamano, huduma shufaa,za tiba asili na tiba mbadala.
MIKAKATI TEHAMA
Kuhusu utekelezaji wa mikakati hiyo ya TEHAMA katika Sekta ya Afya, Mratibu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Kanda ya Pwani, Baraka Eliezer anasema kuwa mfuko huo unatekeleza mradi muhimu wa tiba mtandao, inayogusa hospitali katika mtandao mmoja.
Anasema, dhamira ni kuhakikisha hospitali zenye huduma bora zaidi zinasaidia zile ambazo hazina wataalamu wa kutibu magonjwa bobezi na vifaa vya kisasa kwa njia ya mtandao, bila kumlazimu daktari aliyekuwapo kwenye hospitali za taifa za rufaa kwenda kwenye hospitali za mikoa au wilaya.
Anasema hivi karibuni serikali imetumia takribani Sh.bilioni mbili kujenga miundombinu ya kuziunganisha hospitali za mikoa na za rufani, kiwa ni azma yake ya kuboresha sekta ya afya nchini kwa kutumia TEHAMA.
‘‘Kupitia TEHAMA daktari bingwa mbobezi wa kutibu masuala ya neva kutoka Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) anaweza kutoa huduma katika hospitali zilizopo mikoani bila mgonjwa kusafirishwa kwenda MOI, Dar es Salaam. Mradi huu tulianza kuutekeleza miaka miwili iliyopita na tuliona hili ni eneo muhimu sana na linaenda sambamba na lengo letu la kuhakikisha jamii inanufaika na TEHAMA,’’anasema Eliezer.
Aidha, Mhandisi huyo ameishukuru serikali ya sasa, kuhakikisha kwamba UCSAF inaendelea kupata fedha zinazowezesha kuwa na miundombinu ya Tiba Mtandao katika hospitali mbalimbali nchini.
Katika upande wa Zanzibar, Eliezer anasema tayari serikali kupitia UCSAF inatekeleza mradi mkubwa wa Tiba Mtandao ili kutatua changamoto za kutoa huduma za kibingwa kwa kuziunganisha Hospitali za Abdallah Mzee iliyopo Pemba na Mnazi Mmoja iliyopo Unguja, pamoja na Hospitali za MOI na Jakaya Kikwete za Dar es Salaam .
Anasema, mradi huo unategemewa kukamilika kabla ya mwezi Juni mwaka huu na kwamba kukamilika kwake kutasaidia kuleta mapinduzi makubwa katika Sekta ya Afya kwa upande wa Zanzibar.
Naibu Waziri anasema kuwa, mfumo wa afya uliopo sasa unailazimu serikali ya Mapinduzi Zanzibar kutumia gharama kubwa kwa mgonjwa anapotoka Zanzibar kwenda kupata huduma za rufaa Tanzania Bara na hivyo UCSAF itahakikisha huduma zote za rufaa zinapatikana pia katika Hospitali hizo za Abdallah Mzee na Mnazi Mmoja zilizopo Zanzibar.