Shirikisho la Kimataifa la Historia na Takwimu za Mpira wa Miguu (IFFHS) limeitangaza Ligi Kuu Tanzania Bara ni ya tano kwa ubora barani Afrika na ya 39 duniani kwa mwaka 2022, na imepanda kutoka nafasi 10 Afrika na ya 62 duniani, nafasi iliyokuwapo mwaka uliopita.
Ofisa Mtendaji Mkuu, Almasi Kasongo, ameelezea kwa uchache tu ni kitu gani ambacho kimeonekana kwa shirikisho hilo la kimataifa hadi kuiweka Tanzania kwenye tano bora, ikizipiga kumbo Ligi Kuu Afrika Kusini, Angola, Tunisia, Nigeria na Zambia.
"Unapofanya jambo ni lazima ufanye utafiti, wataalamu walikaa na wakaja wa matokeo hayo.
Siri kubwa ya kuwa hapa ni utawala bora, uwazi na weledi, Bodi na Shirikisho tumekuwa tukipigania sana hilo, tangu Rais wa TFF, Wallace Karia, alipoingia madarakani unaweza ukaona ni kwa kiasi gani eneo la utawala bora limezidi kuimarika, unapokuwa na utawala bora ni lazima kutakuwa na uwazi na kukiwa na uwazi basi watu watafanya kazi kwa misingi ya weledi. Ukivichanganya vitu hivyo vitatu, mafanikio yake ndiyo haya tumeanza kuyaona," Kasongo alisema.
Niwapongeze TFF na Bodi ya Ligi kwa usimamizi mzuri na kutengeneza mazingira safi na rafiki kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo imesababisha kupaa Afrika, japo bado baadhi ya watu wamekuwa na maswali mengi juu ya ligi hii kuzidi kama zile za Afrika Kusini, Zambia, Angola na Tunisia.
Kwangu binfasi naweza kuainisha vitu ambavyo kwa kiasi kikubwa vinaweza kuwa ndiyo vimesababisha Ligi ya Bongo kupanda.
Kwanza kabisa, ninavyojua wachezaji wengi za Zambia awali walikuwa wakikimbilia Afrika Kusini kucheza soka la kulipwa, kuwepo nchini kwa nyota kama Clatous Chama, Moses Phiri wa Simba, Kennedy Musonda wa Yanga, inaonyesha kuwa ligi ya Tanzania kwa sasa imepanda sana.
Zamani wachezaji kama kina Chama na Phiri wangekuwa wako Sauzi tu.
Kumiminika kwa wachezaji kila pande wa Afrika mpaka kwa nchi ambazo Wabongo hawakuwahi kuona kama wanaweza kuja kucheza soka hapa, kunaonyesha jinsi gani ligi imepiga hatua.
Kuwepo ia kwa idadi kubwa ya wachezaji wanaoruhusiwa kusajiliwa pia kumesabisha hivyo licha ya kwamba hapo awali baadhi ya wahafidhina walikuwa wakipinga, wakitaka wapunguzwe.
Kwa sasa idadi ni wachezaji 12, na wapo wanaotaka msimu ujao waongezeke hadi 15 ili ligi izidi kupanda juu.
Klabu ya Simba kutinga hatua ya robo fainali ya michuano ya kimataifa mara tatu, na kusababisha ushiriki wa timu nne, huku msimu huu ikiwa imeingiza timu mbili za Simba na Yanga kwenye hatua za makundi kwenye michuano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika, CAF.
Kwa siku za karibuni Bodi ya Ligi pia imekuwa ikidili na waamuzi ambao walionekana hawafanyi vema kwenye mechi mbalimbali.
Waamuzi wengi wamefungiwa, na hawa ndiyo ambao mashabiki wengi wanadai kusababisha soka la Tanzania kudumaa.
Wapo vijana waliopandishwa ambao kwa sasa wanachezesha vyema sana na yale makosa ya kibinadamu ya waamuzi sasa yanafanywa na wachezaji uwanjani, siyo wao tena.
Hapa ndipo TFF na Bodi wanapaswa kushikilia bango. Ni eneo linalotakiwa kuwa endelevu na la kutazamwa, ikiwezekana kuazima hata baadhi ya waamuzi kutoka Zanzibar ambao wameonekana kuchezesha vema Kombe la Mapinduzi, nao waje kuongeza nguvu.
Pia eneo la viwanja pia TFF na Bodi kwa siku za karibuni wameonekana kulivalia njuga. Hili nalo linatakiwa kuwa endelevu kwani haitopendeza tena kuona ligi iliyo tano bora Afrika ikichezwa kwenye viwanja vibovu.
Mbali na hayo, yapo pia maeneo mengine kadhaa ambayo yanatakiwa kufanyiwa kazi kama TFF na Bodi wanahitaji ligi ya hapa nchini izidi kwenda juu na kushangaza wengi Afrika.