Miaka ya 1990 kurudi nyuma ilikuwa ni jambo la kawaida tu kukuta mama, msichana mmoja au wawili au zaidi wakiwa amekaa wanasuka ukili, huku wakipiga stori za kila siku zile za hapa na pale, huku watoto wao wakicheza pembeni.
Nakumbuka mama yangu naye alikuwa mmoja kati ya kinamama hao. Alikuwa akienda sokoni kununua ukindu.
Ukindu ni majani au kitembe ambayo hupatikana sehemu mbalimbali, hususan kwenye mito au zenye kupitiwa maji mara kwa mara. Majani yake hutumika kusukia kili za kushonea vikapu, mikeka au vitanga.
Baada ya hapo atarudi nyumbani na kuanza kuchana ukindu kwa namna ambayo anahitaji ili kusuka ukili.
Nilikuwa nikimwona mama yangu akisuka ukili karibuni kila siku anapopata nafasi. Mara nyingi huwa baada ya chakula cha mchana au jioni kabla ya kupika chakula cha jioni, ingawa kuna wakati pia alikuwa anapumzika kufanya kazi hiyo.
Hata majirani zake nao walikuwa wanafanya hivyo hivyo. Wakati mwingine wanakusanyika pamoja kupiga stori huku akisuka.
Nilichokuwa nakiona ni kwamba kila siku ukili ulikuwa unakuwa mrefu na kukunjwa mithili ya nyoka aliyejikunja.
Anaporidhika kwa mahesabu ya macho, nilichokuwa nikikiona alikuwa anapima kwa kutumia urefu wake na mkono kuunyoosha juu akiwa ameshika ukili. Atafanya hivyo mara kadhaa akihesabu hadi pale atakaporidhika au hesabu ya urefu anaoutaka utakapopatikana. Hadi mama yangu mzazi anafariki sijawahi hata siku moja kumuuliza huwa wanahesabu hivyo mara ngapi.
Tulichokuwa tunaona na kuburudika kuwaona pale tulipokuwa watoto ni kuona tu wanavyosuka na kushona tu, si kuuliza maswali.
Halafu sasa mama yangu alikuwa mmoja wa wale kinamama aliyekuwa akianza kusuka, anaimba anaimba. Ataimba nyimbo za muziki wa dansi wa Tanzania. Akichoka ataimba nyimbo za mapambio, akimaliza anaimba nyimbo za kiasili za nyumbani kwao alizaliwa.
Kwetu sisi ilikuwa ni burudani tu. Kwanza ile kumuona anasuka ukili ilikuwa tunapenda kumuona. Halafu kama dakika 10 zikipita tunamkumbusha, "mama leo mbona huimbi?" Hajibu kitu, muda si mrefu ataanza kuimba. Sisi watoto wake tunakaa kimya kumsikiliza na kupata burudani ya nyimbo hadi atakapochoka kusuka, au muda wa kuanza kuandaa chakula.
Baada ya kupata mikanda kadhaa ya ukili ambayo nilisema ni kama nyoka aliyejikunja. Siku moja atakwenda sokoni kununua rangi mbalimbali ambazo kuna atazichemsha kwa kuchanganya maji. Baada ya hapo atatumbukiza ukili aliousuka kwenye maji yaliyochezwa na rangi. Kila ukili utakuwa utatumbukizwa kwenye maji ya rangi inayotakiwa. Mmoja utawekwa kwenye rangi nyekundu, mwingine bluu na mwingine kijani. Halafu kuna ukili mmoja au miwili haitawekwa popote. Utabaki na rangi yake ya asili.
Siku chache baadaye utaanza kuona mama anaanza kushona yale maburungutu ya mduara ya ukili wenye rangi tofauti.
Nilikuwa namuona mama yangu akishona kwa kutumia sindano kubwa na ndefu. Uzi aliokuwa akitumia mara nyingi ni wa nailoni.
Ushonaji huo nao utakuwa kwa muda wa zaidi ya wiki moja au zaidi kutegemea na kazi zake zingine. Halafu siku isiyo na jina unaona anataka kwa kisu mviringo wa mshono ule na kuwa mkeka. Na urefu au ukubwa wake unategemea na saizi aliyokuwa akiihitaji tangu awali.
Mkeka huo unakuwa na rangi mchanganyiko ambazo alikuwa wakichovya ukili wake kwenye yale maji yaliyocheshwa na kuchanyikana na rangi.
Kinamama wengine huuza mikeka huyo, mingine hutumika kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya familia yake na wageni tu nyumbani.
Huu ni usanii wa hali juu ambao kinamama wa wakati huo hasa wa maeneo ya Pwani, waliozaliwa, kukulia, au kuishi walikuwa nayo.
Anapoanza kusuka ukili unaweza kuona kama anajichosha au kupoteza muda, lakini mwisho wa siku hata sisi wenyewe watoto tulikuwa tunashangaa mwisho wa yote unaibuka mkeka.
Cha kusikitisha ni kwamba siku hizi unaweza kutembea na kuimaliza Dar es Salaam yote, tena siku hizi ni kubwa sana kuliko zamani na usimkute mama anasuka ukili au kushona mkeka.
Utamaduni au sanaa hii ambayo ilitakiwa kuendelezwa vizazi kwa vizazi imeanza kupotea kama si kupotea kabisa. Sidhani kama kinamama walikuwa wamewarithisha mabinti zao. Au kama walirithishwa wanaona umuhimu huo kwa sasa?










