'Rice cooker' ilivyoua utamu wali uliopaliliwa na mkaa

14Jan 2023
Adam Fungamwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
'Rice cooker' ilivyoua utamu wali uliopaliliwa na mkaa

TEKNOLOJIA licha ya kwamba imeleta maendelea makubwa sana na kurahisisha maisha, lakini imekuja kuondoa baadhi ya vitu vya kitamaduni.

Huko nyuma tuliwahi kuelezea jinsi teknolojia ilivyorahisisha kizazi cha sasa kupata wapenzi na wake kwa urahisi, tofauti na zamani ambapo hakukuwa na simu za mkononi kiasi kwamba watu waliganda sana kwenye vituo vya basi, au sehemu walizoahidiana wapenzi, na kule vijijini ilikuwa tafrani tupu, kwani watu waligandishwa kwenye miti, vichaka, huku wakiwa hawana uhakika wa wapenzi wao kuja, kwa kuwa tu hakukuwa na mawasiliano.

Vile visa vilivyokuwa vikitokea kutokana na kutokuwa na teknolojia ilikuwa ni burudani tosha.

Leo tunaangalia teknolojia kwenye mapishi. Imekuja kurahisisha chakula kuiva kwa muda mfupi kwa kutumia jiko la gesi na umeme, bila mpishi kuhangaika sana au kuchafuka.

Zamani ili kupika chakula lazima kwanza vitafutwe vifuu kwa wakazi wa mikoa wa Pwani, ukanunuliwe mkaa, au liwashwe jiko la mchina, na jiko lililoonekana ni la kisasa zaidi na linaloivisha kwa haraka zaidi, stovu.

Hiyo ndiyo faida ya teknolojia, lakini bado kuna watu wanadai baadhi ya vyakula havinogi vikipikwa kisasa.

Wanakumbuka miaka  ya 1990 kurudi nyuma, wakati kinadada na kinamama walivyokuwa wakipika wali kwa kutumia mkaa, vifuu au kuni.

Halafu baada ya kuiva, sufuria la watu linafunikwa juu. Ule moto wa mkaa, kuni au vifuu unagawanywa. Nusu unabakishwa kwenye jiko au mafiga, halafu mwingine unawekwa juu ya mfuniko.

Kwa lugha rahisi iliyokuwa inatumika wakati ule na nadhani hata sasa ni kupalilia.

Baada ya hapo utaachwa hapo na nadhani baada ya masaa mawili hivi, utapakuliwa, tayari kwa ajili ya chakula cha familia.

Wali huo utiwe na nazi au mafuta ulikuwa unanukia vizuri, kwa sababu tayari juu wali unakuwa umeungua na kutengeneza kitu kama utandu hivi na jina lake linaitwa matandu, wengine huita mahaba, ili mradi kila mtu na jina lake.

Upishi wa aina hiyo ulitengeneza matandu, halafu chini ukatengeneza kitu kinaitwa ukoko.

Matandu na ukoko ulikuwa ndiyo vipenzi vya watoto wa zamani. Na wengi wao walipenda mno wali na maharage. Wenyewe waliita ubwabwa na maharage. Watoto wa zamani hawakuwa na makuu. Hakuhitaji wali kuku, wali nyama, wali samaki wala nini. Wao ni wali na maharage tu.

Sasa ndiyo ilkute wali ulioungwa na nazi umepaliliwa na maharage nayo yaungwe na nazi. Ni hatari tupu.

Sasa burudani inaanza pale akinamama wanapoanza kupika wali huo. Watoto siku hiyo hawaendi kucheza mbali. Ikumbukwe kuna miaka hasa mwishoni mwa 1970 hadi miwshoni mwa 1980 hadi mwanzoni mwa miaka ya 1990, mchele ilikuwa bidhaa adimu sana nchini Tanzania. Siku ikipikwa nyumbani, balaa lake linakuwa kubwa.

Wengine wanajifanya wanasinzia ili upakuliwe mapema, lakini akishakula wanaenda kucheza. Hakuna tena usingizi. Wengine hata wale ambao ni wabishi kuoga, siku hiyo bila fimbo wala kulazimishwa wanaoga mapema. Kisa siku hiyo unapikwa ubwabwa nyumbani.

Mama atapalilia na wakati wa kupakua, watoto wataanza kupewa matandu kwanza, kabla ya ubwabwa.

Halafu kesho yake asubuhi, watoto huamka mapema hata kama si siku za kwenda shule. Kisa ni kwamba wanakumbuka kuwa jana ulipikwa ubwabwa, lengo ni kutaka wapakuliwe ukoko ambao unamiminiwa na mchuzi mwingi wa maharage.

Hapo watoto wataanza kula ukoko kwanza, kabla ya kula ubwabwa na chai asubuhi.

Ukimuuliza mtoto yoyote wa miaka hiyo, atakwambia utamu wa matandu na ukoko, jinsi mapishi ya akinamama wa wakati huo kutokana na kupika kwa kutumia mkaa, kuni na hata vifuu.

Kutokana na kukua kwa teknolojia, hivi sasa kwa asilimia 90, hasa wakati za mijini hawatumii sana mkaa, vifuu wala kuni.

Angalau vijijini, ambako bado kuna kuni ambazo wanatumia. Lakini vile vile wanawake wengi kwa sasa wamekuwa hawatumii tena aina ya mapishi ya kupalilia wali, labda wale wa mikoa ya Pwani kama vile Tanga, Lindi na Pwani yenyewe hasa Bagamoyo.

Ni aghalabu sana leo kukuta wali unapaliliwa kutokana na teknolojia, kwani sasa wengi wanatumia 'rice cooker' na hata jiko la gesi kupika wali, hivyo haiwezekani.

Ukipika kwa njia hiyo huwezi kupata matandu wala ukoko chini. Ndiyo maana wengi waliozungumzia hili ambao ni watu wazima, walionekana kukumbuka sana matandu na ukoko, lakini kwa sasa wakadai hawawezi kuupata kwa sababu wake zao ni wa kisasa, na wanatumia majiko ya kisasa.

Wengi walikuwa wanakula matandu na ukoko kwa mapishi waliokuwa wakipika mama zao enzi hizo. Kwa sasa wanabaki na kumbukumbu tu na kusimulia tu, lakini ni nadra sana kuupata wali wa kupaliliwa, ambao ulikuwa mtamu na wenye kunukia.

Watoto wa kizazi cha sasa wao ndiyo kabisa. Wao ni wali wao ni kwenye 'rice cooker' na jiko la gesi tu.

Ukiwasimulia mambo ya wali wa kupaliliwa, matandu na ukoko, watakushangaa tu.

Tuma meseji 0716 350534