Uhaba wa damu ulivyo na suluhisho linalotoka kwa kila kona ya jamii

12Jan 2023
Pankras Luoga
DAR ES SALAAM
Nipashe
Uhaba wa damu ulivyo na suluhisho linalotoka kwa kila kona ya jamii

“ALIYETOA pesa kuchangia ujenzi wa choo cha mahabusu asubuhi, jioni ya siku ile ile alikuwa mtuhumiwa wa kwanza kuingia kwenye ile mahabusu yenye choo kilichokarabatiwa,” ni sehemu ya usemi wenye vionjo wa kifasihi.

• Damu ikiwa benki. PICHA ZOTE: MAKATABA

Vivyo hivyo, hicho ndicho kinatumika katika upatikanaji na matumizi ya damu hospitalini, ikielezwa mtu anachangia damu leo na kesho huenda damu hiyo, ikatumika kuokoa maisha yake, mkewe, mtoto, dada, shangazi, mama au mwingine wa karibu yake.

Taarifa kutoka vituo vya afya katika ngazi mbalimbali nchini hasa hospitali za wilaya, mikoa, kanda na taifa, zinaonyesha kukabiliwa na upungufu wa damu. Kwa mfano, ni hivi karibuni kulikuwapo taarifa kwamba  Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Rukwa, inakabiliwa na upungufu wa uniti 50 za damu kila mwezi, kwani inakusanya uniti 150 kwa mwezi, wakati mahitaji halisi iliyo nayo ni uniti 200 kwa mwezi huohuo.

Ni uhaba unaoipunguzia uwezo  hospitali katika kutoa huduma bora za afya, hasa zile za dharura zenye kuhitaji huduma ya kuongezewa damu.

HALI YA UCHANGIAJI

Ingawaje kumeshuhudiwa wadau mbalimbali wakijitokeza kuchangia damu hasa katika matukio maalumu, kama vile kampeni za uchangiaji damu, siku za maadhimisho ya uchangiaji damu duniani au matamasha, pia  kupitia  taasisi husika za kijamii kama “Simba Day” na “Yanga Day”.

 

Hata hivyo. bado hali ya uchagiaji damu kwa sasa si ya kuridhisha, kwani hospitali nyingi zimekuwa zikitoa taarifa za kukabiliwa na upungufu wa damu katika akiba zao.

 

Pia, taasisi inayohusika na damu nayo (Benki ya Damu) imeonekana kutokuwa na akiba ya damu ya kutosha, licha ya juhudi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuendesha kampeni hizo za kutoa elimu kwa wananchi, kuhusu faida za uchangiaji damu na kuchangisha damu kutoka kwa wadau mbalimbali nchini.

 

Hivyo, ni hali isiyo sahihi hata kuinua mahitaji ya jamii tunahitaji kuunga mkono juhudi hizo, ukijitolea damu na kuwahamasisha wengine pia kufanya hivyo. Mara zote, damu inayotolewa huwa ni ya kuokoa maisha ya wajawazito na watoto wachanga, ambao ni ndugu kwa maana ya wawe wa karibu kama dada, wadogo, shangazi au watoto wetu.

 

Na zaidi ya ndugu wanaopata ajali na kuhitaji damu, hata kuongezewa damu na hilo halina mwenyewe, kwani yeyote katika jamii akipata ajali au madhara, hata akapoteza damu nyingi, moja kwa moja ni mhitaji wa kuokoa maisha, pale panapohitajika kuongezewa damu.

 

ATHARI ZIKOJE?

Athari za upungufu wa damu katika vituo vya afya ni kuongezeka vifo vya wahitaji kama vile wajawazito na watoto wachanga, wagonjwa wengineo na hasa wale wa ajali, wenye kuhitaji huduma ya kuongezewa damu.

 

Mfano, kwa siku za hivi karibuni kumekuwapo na ongezeko la ajali za barabarani nchini na kuchangia kuwapo majeruhi wengi wa hospitali jirani na ukanda wa ajali, wakihitaji nyongeza ya damu haraka.

 

Upungufu wa damu katika vituo vya afya, huzaa usumbufu mkubwa kwa ndugu wa wagonjwa, kwani wanahitajika kuanza kutafuta mtu wa kutoa damu pindi mgonjwa wao atakapogundulika anahitaji huduma ya kuongezewa damu.

 

HATUA STAHIKI

Ni jukumu la asili, kwamba kila mmoja katika jamii anahitajika kujitolea damu na kuwaelimisha wengine kuhusu umuhimu wa kujitolea damu, hivyo awahamasishe wengine.

Pia, taasisi zinazohusika na hasa hospitali kupitia taasisi ya benki ya damu, zinapaswa kutoa ujumbe wa kuhimiza jamii ishiriki katika kujitolea damu.

 

Hapo, wataalamu wa afya nchini wanapaswa kujikita katika kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa uchangiaji damu na kuieleza jamii faida za kila mwananchi kushiriki katika hilo, waokoe maisha ya wajawazito na watoto wachanga na wagonjwa wengine wenye mahitaji ya damu na mchangiaji mwenyewe.

 

Hapo kuna rejea nyingine, kwamba kila mmoja anapaswa kutambua yu mgonjwa mtarajiwa mwenye kuhitaji kuongezewa damu, ili kuokoa maisha yake.

 

Zaidi wataalamu wa sekta nyingine kama ulinzi, elimu, maji, nishati, miundombinu, kilimo, utalii, mifugo na nyingine  wana nafasi muhimu ya kushiriki kuelimisha wafanyakazi wao na wote katika makundi yao, kama vile wanafunzi na jamii kwa ujumla waendane na umuhimu wa kushiriki uchangiaji damu.

 

Mara nyingi operesheni na kampeni za uchangiaji damu, hubebwa na mitazamo ya baadhi ya wanajamii katika eneo husika,  hivyo inaibua wajibu  wa wanajamii kusaidiana kuondoa mitazamo hasi katika kila dhana ya uchangiaji damu.

 

Bado  kuna kundi muhimu ndani ya jamii kama vile viongozi wa dini, kwani wako mstari wa mbele, wameanza na wanaendelea kuwahimiza waumini wao kushiriki zoezi uchangiaji wa damu na wanaonyeshe kwa vitendo kwamba, kuchangia damu sio kitu kibaya kwani maandiko ya kidini yanaendana nayo na kuipa baraka zote.

Mkoani Rukwa ambako kuna uhaba tajwa, viongozi wa dini ya Kiislamu waliamua kwenda na kuchangia damu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Rukwa, ikiwa ni ishara bora mbele ya waumini wao na jamii kwa jumla, kwamba hilo ni jambo muhimu kwa kila mmoja kuwa mstari wa mbele kushiriki.

 

FAIDA KWA JAMII

Kuna faida nyingi zinatajwa jamii inaposhiriki kuchangia damu, baadhi ni hizo za kupunguza vifo visivyo vya lazima vya wahitaji wa maradhi na matukio ya dharura.

 

Mengine yanatajwa, ni kusaidia kupanua tija katika huduma za afya zinazotolewa na vituo vya afya katika maeneo yao.

 

Kwa sasa, wanajamii wote wanawajibika kujitokeza kuchangia damu pasipo kusubiri siku au matukio maalumu, kwani wahitaji wapo kupitia kiashiria cha upungufu tajwa; wajawazito, watoto wachanga na mgonjwa wodini ambao mara zote huangukia msamaha maalum ni wenye sababu maalumu za kiafya au kitabibu kutotoa damu, japo nao nafasi yao inahamia katika kuchangia kuhamasisha na  kutoa elimu ya umuhimu huo.

Pia, wataalamu toka sekta ya afya pamoja na sekta nyinginezo kama maji, elimu na ulinzi wanapaswa kusaidia kutoa elimu kwa wafanyakazi na jamii zao.