Uchunguzi ufanywe, kulikoni matusi kwenye mtihani, kidato 2 kuporomoka

06Jan 2023
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Uchunguzi ufanywe, kulikoni matusi kwenye mtihani, kidato 2 kuporomoka

MOJA kati ya mambo yaliyotawala kwenye matokeo ya mitihani ya kidato cha pili na darasa la saba ni kushuka viwango ya ufaulu, kuwapo udanganyifu pamoja na matusi.

Kaimu Katibu Mkuu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa, Athumani Amasi, anasema kwamba wanafunzi 279 wamefutiwa matokeo, kati yao 82 ni wa darasa la saba na 213 wa kidato cha pili.

Akasema hao walifutiwa, baada ya kubainika kuwa wamefanya udanganyifu na 14 wa kidato cha pili waliandika matusi.

Pia, kwenye mtihani wa kidato cha pili, kunatajwa  ufaulu ulishuka na kuwa asilimia 82.6.7 dhidi ya asilimia 92.3.2 kwa msimu uliopita.

"Natoa wito kwa wazazi, walezi kuacha tabia ya kuwadanganya wanafunzi ambao ni watoto wao kwa mbinu tofauti ili wafaulu, waache wafanye mitihani kwa uwezo wao, wakiandaliwa vizuri watafaulu," alisema Amasi.

Nawapongeza wanafunzi wote wa kidato cha pili na darasa la nne waliofaulu. Hata ambao hawakufanikiwa, wasikate tamaa, kwani inawezekana hawakuwa kwenye hali nzuri wakati wa mitihani.

Inawezekana kabisa siku hiyo walikutana na changamoto mbalimbali. Huwezi kujua wanafunzi wanapitia mengi sana, inawezekana siku hiyo akatoka nyumbani kukiwa na ugomvi wa wazazi wake, au siku ameamka akiwa anaumwa, hata kufiwa.

Wanaweza kurudia tena Mungu akawasaidia.

Kuna wale ambao wanadanganya, tena kwa kusaidiwa na wazazi na walezi wao kama alivyosema Amasi.

Hii inatokana na dunia ya sasa kuhitaji zaidi vyeti kuliko uwezo halisi wa mtu. Ndiyo maana wazazi wanatumia sana kuwapa kile wanachokuona kama ni majibu ili wafaulu bila hata kujali kichwani mwa watoto wao kuna nini.

Hii ndiyo inatuzalishia wasomi 'feki' ambao waajiri wengi wanadai hawaajiriki, kwa  sababu wamefuzu kwenye makaratasi tu kwa uongo. Wale wenye uwezo wanaachwa. Halafu wazazi kama hawa wanawapa matokeo watoto wao, wakifaulu wanafanya bonge la sherehe.

Hawa wazazi hawana tofauti na timu inayonunua mechi, halafu ikipata ubingwa inafanya sherehe ya kuwa bingwa.

Mimi nadhani imefika wakati wataalamu wetu na wasomi, kuanza uchunguzi kujua ni kwa nini ufaulu msimu huu umepungua, pia kwanini miaka ya hivi karibuni kumekuwa na udanganyifu kwenye mitihani kiasi kwamba inafikia wakati watu wanabadilisha hata namba za watahiniwa na hata wale wanaoandika matusi.

Naweza kuonekana wa ajabu kidogo kwa sababu ya utamaduni wetu. Huwa si watu wa kufanya uchunguzi, lakini hili kwa wenzetu wangelifanya haraka sana, halafu wangekuja na majibu.

Hayo majibu huwa yanazisaidia serikali kujua nini cha kufanya. Nini cha kupunguza na nini cha kuongeza.

Tuna wasomi wengi nchini ambao wamekaa tu, huu sasa ni wakati wa kuwaingiza kwenye mtihani wa kufanya uchunguzi.

Ni kuwachukua hao wanafunzi, kukaa nao kirafiki tu, na kuwauliza ni nani anawapa mitihani na walielezwa nini, na hata wanaotukana wanafanya hivyo kwa sababu gani, na kipi huwa kinawasibu.

Hapa tunaweza kupata kitu tusichokijua tofauti na tunavyofikiria. Hadi sasa hatujajua ni kwa nini miaka kadhaa iliyopita kuna mwanafunzi alichora zombi kwenye mtihani.

Vitu kama hivi sisi tunaviona kama mzaha, lakini wenzetu huvichukulia kwa umakini na kupata somo ambalo linawafanya kurekebisha hali fulani ya kuokoa wanafunzi na kuwafanya warudi kwenye mstari wao na wazazi wao wanaotaka watoto wao wafaulu bila ya kuwa na uwezo kichwani.