Mashabiki Simba mwacheni kocha mpya afanye kazi yake

09Jan 2023
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Mashabiki Simba mwacheni kocha mpya afanye kazi yake

WAKATI Kocha Zolan Maki alipoingia Simba alibainisha wachezaji anaowakubali na wale ambao alisema hawapo kwenye mipango yake.

Tatizo lilikuja pale baadhi ya wachezaji waliotajwa kuwa hawaoni kama wanaweza kuiletea klabu hiyo tija ni vipenzi vya mashabiki wa klabu hiyo.

Sisemi kwamba ndiyo sababu iliyomfanya kuondoka, ila ilichangia mashabiki wengi wa klabu hiyo kutompenda. Baada ya nafasi yake kukaimiwa na Juma Mgunda, hatimaye ameshuka kocha mwingine, Robertinho Oliveira.

Kwa mara ya kwanza ameitazama mara mbili 'laivu' timu yake kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi. Ni mechi ambazo Simba ilichezesha wachezaji ambao hawapati sana namba kwenye kikosi cha kwanza. Kocha alikuwa jukwaani na akatazama uwezo wa vipaji vya wachezaji wake.

Wanachama na mashabiki wengi wa klabu hiyo hawakubaliani na uwezo wa wachezaji wengi wa kikosi hicho, kocha huyo yeye ameona tofauti.

Kuna baadhi ya wachezaji ambao anasema ni wazuri na kuwashangaza wengi, ila akasema wanakosa vitu vichache ambavyo wanahitaji kurekebishwa.

Kocha huyo akapendezwa na uwezo wa wachezaji wanne. Wa kwanza ni Kibu Denis ambaye wanachama na mashabiki wengi wa Simba kwa sasa hawamkubali. Wengine wanataka aondoke au atolewe kwa mkopo.

Taarifa zinasema viongozi wa Simba waliikatalia Geita Gold ambayo ilikuwa ikimtaka mchezaji huyo kwa mkopo. Nadhani viongozi wa klabu hiyo bado kuna kitu wanakiona kama ambavyo kocha huyo amekiona, ambapo hakionwi kwa jicho la tatu na mashabiki wa timu hiyo.

"Nimefurahi kwa umri wake unafaa, nitafanya kazi naye na kuhakikisha anakuwa bora," alisema kocha huyo.

Na waliokuwa naye alidai kuwa akauliza ni raia wa nchi gani, akaambiwa ni Mtanzania na akamsifu kutokana na uwezo wake wa kukaba, nguvu na kutumia miguu yote miwili.

Mchezaji mwingine aliyemtaja kuwa ni mzuri ingawa ana mapungufu kadhaa yanayohitaji kurejebishwa ni Jonas Mkude, akamsifu pia kijana Michael Joseph na beki Kennedy Juma.

Katika wachezaji wote wa Simba waliocheza kwenye Kombe la Mapinduzi inaonekana amevutiwa na wachezaji hao tu.

“Kennedy anakaba kwenye nafasi ni mchezaji ambaye hatumii nguvu anafanya kazi nzuri uwanjani ana umbo zuri na ni mrefu ana kila sifa ya kuitwa beki, napenda timu yenye wachezaji wa aina yake nitaendelea kuwaangalia zaidi nijue na mapungufu yao,” alisema kocha huyo.

Inaavyoonekana kocha huyu ni aina ya makocha ambao wana uwezo wa kutengeneza wachezaji na si kufundisha zaidi.

Kuna makocha ambao hutumia wachezaji ambao tayari wapo vizuri na wenye uwezo na viwango vikubwa, lakini hawana uwezo wa kuwatengeneza na kuwarekebisha kutokana na kasoro zao.

Robertinho anaonekana ni mmoja wa makocha ambao anaweza kurekebisha mapungufu ya mchezaji ambaye yeye anamuona ana kitu, ila kuna vitu anavikosa.

Hii inaweza kuwa ni faida kubwa kwa Klabu ya Simba kwani inaweza kusababisha baadhi ya wachezaji ambao walikuwa wanaonekana wamekwisha kuibuka tena.

Kinachotakiwa sasa ni wanachama na mashabiki wa klabu hiyo kuacha mihemko, kuchanganywa na kauli za wapinzani wao, badala yake wamuache kocha huyo afanye kazi yake.

Bahati nzuri tu ni kwamba Robertinho ni kocha maarufu kwenye ukanda huu na amepata mafanikio makubwa akiwa na Klabu ya Rayon Sports ya Rwanda na Vipers ya Uganda, vinginevyo kelele zingekuwa zimeshaanza.

Kama viongozi, wanachama na mashabiki wa Simba watamuacha kocha huyo kwa muda mrefu, anaweza kuwatengenezea kikosi cha kutisha chenye wachezaji bora, uwezo wa viwango vikubwa tena bila kutumia gharama kubwa.

Ni kocha ambaye anaonekana ana jicho la kujua wachezaji anaweza kusajiliwa hapa hapa Afrika wasio na majina makubwa, lakini wenye viwango vikubwa akatengeneza muunganiko wa hatari kama alivyofanya alikotoka ambako alikuwa na vikosi ambavyo havikuwa na gharama kubwa.

Kama huko alikuwa na wachezaji wa kawaida na akafanya kitu, Simba ambao ina uwezo wa kusajili wachezaji wa daraja la kati Afrika, anaweza kufanya makubwa. Kikubwa msimu ujao yeye ndiye awe na mamlaka ya kukata wachezaji wasiofaa na kuleta ambao anaamini atafanya nao kazi nzuri.