Uwepo msukumo kujua  Kiswahili, Kiingereza

10Jan 2023
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Uwepo msukumo kujua  Kiswahili, Kiingereza

BARAZA la Mitihani (NECTA) hivi karibuni limetangaza matokeo ya mtihani wa darasa la nne na kidato cha pili likieleza kuwa mambo si mazuri kwenye Kiingereza na Kiswahili.

NECTA inaeleza wanafunzi wamedorora kwenye lugha hasa Kiswahili na kimombo, kwa hiyo uelewa wa lugha unaporomoka ikiashiria kuwa hata shule ambazo zinatumia Kiingereza kufundishia tofauti na za umma ufaulu haupendezi.

Zipo sababu nyingi zinazoweza kutajwa kuzungumzia upungufu huo. Wako watakaosema tatizo ni walimu wa Kiswahili na Kiingereza licha ya kwamba Kiswahili kimepigiwa chapuo kuwa lugha ya kimataifa ikiwamo Afrika Kusini kutangaza mkakati wa kukifundisha shuleni na vyuo vikuu, hivyo wengi wanaoina inakubalika zaidi na walitakiwa kuweka msukumo zaidi.

Kadhalika Kiingereza ni lugha ya kimataifa na kwamba zama hizi kina mashiko na kinahitajika zaidi kwa ajili ya kufanyakazi za kikanda na kimataifa.

Aidha, Kiswahili ni muhimu huzungumzwa kwenye mikutano ya Umoja wa Afrika na huenda hata hapa nchini kinapewa kipaumbele zaidi huku Kiingereza kikiendelea kupewa nguvu mpya na hata baadhi ya shule za serikali kuanza shule za msingi zinazofundisha lugha hiyo.

Inawezekana ufundishaji duni na ukosefu wa wataalamu wa kufundisha Kiswahili na Kiingereza kikamilifu unaweza kuwa sababu ya wanafunzi kushindwa lugha hizo.

Kwa upande wa Kiingereza sababu inaweza kuwa ni kukosa wapenzi na wazungumzaji na kusababisha wanafunzi kuichukia na hata kushindwa mitihani kama inavyotokea kwa darasa la nne na kidato cha pili.

Lakini, kwa sababu hakuna utafiti uliofanyika kujua kiini na sababu ya watoto kushindwa Kiingereza na Kiswahili na ufaulu duni hakutakuwa na majibu sahihi ya maswali hayo.

Pamoja na changamoto zilizoko ni vizuri kama taifa  kukazania wanafunzi  kujua zaidi Kiingereza na Kiswahili kuliko zaidi na ikibidi kuwekeza kwenye ufundishaji na matumizi yake kutokana na umuhimu wake kiuchumi, kisayansi na kibiashara duniani.

Kama nchi inayoendelea haiwezekani kupuuza lugha iwe Kiingereza au Kiswahili hili linapaswa kupewa kipaumbele na kuwa na umuhimu wa matumizi yake kimataifa, hakuna anayeupinga uhitaji huo kwa kuwa hata katika nchi zilizoendelea ambazo Kiingereza si lugha yao ya asili, bado kinahimizwa na kinatumika.

Ni wazi kuwa hata mataifa yaliyoendelea kiteknolojia, kiuchumi na ugunduzi wa hali ya juu kuanzia tiba, kilimo na uzalishaji viwandani, wanaendelea kutumia Kiingereza ni wazi lugha hiyo ina umuhimu mkubwa na wa kipekee na si ya kupuuza kwa vile imeshakuwa na mizizi katika sekta muhimu duniani za kiuchumi, teknolojia na maendeleo.

Serikali itoke msukumo kwa walimu wa lugha hasa Kiingereza, Kifaransa na hata Kichina pamoja na Kiswahili na kuwalipa vizuri walimu wa lugha hizo ili nchi iwe na watu wanaoelewa  lugha.

Kwa mfano kuna maelezo kuwa Japan, Ufaransa, Ubelgiji na Italia mwalimu anayefundisha Kiingereza analipwa vizuri zaidi na hilo ni vyema Tanzania kulitazama ili kuwa na walimu bora wa lugha hapa nchini.

Ukweli ni kwamba Kiswahili kina umuhimu lakini Kiingereza ni lugha ya uwekezaji, biashara, uchumi, teknolojia na kwamba ndiyo inayobeba mawasiliano ya kila mradi wa maendeleo ndani na nje ya nchi na hata kama ni mikataba ya kibiashara, masoko na huduma inafanyika kwa lugha hiyo, si vyema kuipuuza.

Kwa Tanzania ipende isipende Kiingereza ndiyo lugha ya biashara na teknolojia duniani, watu, kampuni za kimataifa zinazungumza Kiingereza na hakuna, biashara au teknolojia masuala ya tiba ya kimataifa bila lugha hii.

Hata magonjwa kama COVID-19, corona, ‘hay fever’ SARS yote mawasiliano yake ni Kiingereza, hata kama Waswahili watayatafsiri na kusema UVIKO 19, homa ya mgunda, yote hayo ni matokeo ya kukitumia kwanza Kiingereza ili kukifasili kwenye Kiswahili kwa hiyo suala la kutupia macho lugha hizi na kuzifundisha ipasavyo hazina mbadala.