Fikra kubwa za uwekezaji mkubwa zitalivusha taifa mgawo maji, umeme

05Jan 2023
Christina Mwakangale
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Fikra kubwa za uwekezaji mkubwa zitalivusha taifa mgawo maji, umeme

MARA zote katika mafanikio yeyote huanza ndoto, mtazamo na hata kutazama na kujifunza kutoka kwa wengine. Ndipo linapokuja suala la uwekezaji.

Uwekezaji, aidha wa muda mfupi, kati na mrefu hufanyika popote hata kwa mataifa ambayo sasa yameendelea, kwa kuwa vipaumbele katika jamii kwanza ni huduma zao, ikiwamo maji na nishati.

Embu fikiria, ni nchi ngapi zilizo kwenye orodha ya neema ya kuzungukwa na vyanzo vya maji. Jiografia ya nchi iliyo na rasilimali ya asili kama maziwa, mito na bahari ni hazina kubwa kwao. Mabadiliko ya tabianchi yanavyokua kwa kasi duniani, ni wakati waliomo kwenye jiografia hiyo kutumia fursa.

Tanzania, imo kwenye orodha ya hazina hizo, kwa kujaliwa miongoni mwa nchi duniani hususan barani Afrika, ambazo zimezungukwa na vyanzo vya asili vya maji, yaani Maziwa Makuu, achilia mbali Bahari ya Hindi na mito mikubwa kama Msimbazi, Ruaha na Rufiji.

Maziwa hayo ni Ziwa Victoria, Nyasa na Tanganyika ambayo kijiografia yamekaa kikanda, kwa maana Kaskazini, Magharibi na Kusini huku Mashariki chanzo kikuu kikiwa Bahari ya Hindi.

Mito ndio usiseme iliyopo kwenye mikoa, wilaya yenye ukubwa wa kutosha, ikiwamo Ruaha, Msimbazi, Rufiji, Ruvu na mingine mingi midogo iliyojaaliwa maji karibu msimu wote wa mwaka.

Ziwa Tanganyika, lenye urefu kilomita za mraba 32,900 ipo Kanda ya Ziwa,  pia Ziwa Nyasa lina kilomita za mraba 29,600, hali kadhalika  Ziwa Rukwa lenye ukubwa wa kilomita za mraba 5,760.

Kwa mujibu wa takwimu za Wikipedia, Ziwa Natron, Manyara, Burigi zote kwa ujumla, zinakadiriwa kuwa na kilomita za mraba za kutosha.

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa), pamoja na shirika la umeme nchini – Tanesco, mwezi uliopita walitangaza mgawo wa maji kwa maeneo mengi ya mji wa Dar es Salaam na hata Pwani wanaotegemea chanzo cha maji cha Ruvu Juu na chini na umeme pia nchi nzima.

Mfano, nchi ya Libya iliyoongozwa na Muamar Gadaffi, ilitengeneza mto bandia ‘Great Man Made River’ na kufuta taswira ya uhaba wa maji kwenye nchi hiyo ambayo ipo Kaskazini mwa bara la Afrika.

Nchi hiyo kwa kiwango kikubwa, imetawaliwa na Jangwa la Sahara, kwa makadirio mto huo bandia, ndio mradi mkubwa zaidi wa uhandisi kuwapo duniani.

Mradi umetawaliwa na mfumo mkubwa wa mabomba na mifereji ya maji, ambayo pia inajumuisha visima zaidi ya 1,300 na kina cha zaidi ya mita 500, hutoa huduma miji ya Tripoli, Benghazi, Sirte na mingine, kusambaza mita za ujazo 6,500,000 kwa siku moja.

Pia, mto huo umo kwenye ‘Ajabu la Nane Duniani’ na mwaka 2008, kitabu cha kumbukumbu cha Guinness kiliutambua mto huo, kama mradi mkubwa zaidi wa umwagiliaji duniani.

Mnamo Septemba Mosi mwaka 2010, ni tarehe ya kumbukumbu ya kufunguliwa  sehemu kuu ya mto huo bandia wa Libya na mradi huo unazidi miradi mikubwa ya ujenzi, gharama yake ni dola bilioni 25.

Wapo watakaodhani kwamba hatua hiyo utekelezaji wake ni mgumu mahali pengine, hiyo si sawa kwa kuwa utaratibu na vipaumbele  muhimu ni kutatua changamoto kwenye jamii na suluhisho la kudumu.

Hata ipite miaka kadhaa ya utekelezaji ni bora, kwa kuwa suluhisho litakuwa la kudumu. Yaani vyanzo vya maji viwepo kusiwepo na ndoto ya aina hii, kipi bora, mikakati ya muda mrefu ya mgawo wa maji ambao athari zipo wazi, kwanza, kushuka uchumi miongoni mwa jamii na mlipuko wa maradhi.

Pia, ikumbukwe ripoti mpya iliyochapishwa na Shirika la Afya Dunian (WHO) mwaka 2017, kwa niaba ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Maji, inaonya nchi nyingi ambazo hazijaongeza kasi ya kutosha kwa kutenga fedha kutumika ili kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), kwa matumizi ya maji safi.

Ripoti hiyo inasisitiza kwamba nchi zinapaswa kuongeza jitihada za kutambua vyanzo vipya vya fedha ili kuhakikisha upatikanaji wa maji safi ya kunywa na kudhibiti magonjwa ambayo yanasababishwa na watu kunywa maji machafu.

WHO kupitia Idara ya Afya ya Umma, Mazingira na masuala ya kijamii, ikasema karibu watu bilioni mbili wako hatarini kuambukizwa kipindupindu, kuhara damu, kupata homa ya matumbo na polio kutokana na kunywa maji machafu ambayo yanaweza kuwa na mchanganyiko wa kinyesi.

Shirika hilo linasema, maji machafu ya kunywa yanakadiriwa kusababisha vifo vya zaidi ya watu laki 500,000 kila mwaka.

WHO inasema kuwa nchi nyingi zinazoendelea, zina malengo ya kuhakikisha upatikanaji wa miundombinu ya msingi, ambayo itatoa huduma salama ya maji na ya kuaminika ili kufikia malengo ya maendeleo endelevu ifikapo mwaka 2030.

Katika ripoti hiyo, Benki ya Dunia inakadiria kwamba uwekezaji katika miundombinu wapaswa kuongezwa na hivyo kutahitajika dola za Marekani bilioni 114 kwa mwaka.