Makosa ya kibinadamu kwa waamuzi sasa yabaki historia

05Dec 2022
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Makosa ya kibinadamu kwa waamuzi sasa yabaki historia

KUTOKANA na malalamiko ya wadau wengi wa michezo nchini, pamoja na kinachoonekana kukua kwa teknolojia hasa kwenye mchezo wa soka, hususan Kombe la Dunia linaloendelea nchini Qatar, Bodi ya Ligi imeonekana kuanzisha juhudi za makusudi ili kuondoka na kutegemea maamuzi ya waamuzi kwa asilimia 100.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Almasi Kasongo, amesema eneo la waamuzi ni muhimu sana na kwa sasa wameanza kulifanyia kazi hasa kwenye masuala ya teknolojia.

Ni ukweli usiopingika kuwa kwa soka la sasa duniani, watu wameacha kutegemea macho ya waamuzi, badala yake wametengeneza vyombo vya teknolojia ambavyo vitakuwa vinamsaidia mwamuzi kulirejea tukio kwa uhakika zaidi tofauti na alivyoliangalia hapo awali na baadaye yeye mwenyewe kutoa maamuzi ya mwisho, yawe yale yale au kubadilisha.

"Dunia ilipo waamuzi sasa wanasaidiwa na vyombo vya teknolojia kuliko kutegemea binadamu kwa asilimia 100, kila siku wanabuni vyombo vipya vya kuwarahisishia kazi na kuwafanya watoe maamuzi ya haki zaidi. Tunaona hata huko kwenye Kombe la Dunia masuala ya teknolojia yalivyopiga hatua, ni sisi ndiyo tumebaki kutegemea waamuzi kwa asilimia 100, lakini juhudi zimeshaanza ili kuhakikisha siku za usoni tu inabaki kuwa historia kwa sababu Bodi ya Ligi imeliona hilo, Shirikisho la Soka nchini (TFF) na serikali wote kwa pamoja juhudi za makusudi zimeanza ili siku za usoni tuondokane na changamoto hii.

Nakumbuka Februari mwaka huu, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, aliandika kwenye mtandao wake wa kijamii kuwa atakaa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa, ili waongee uwezekano wa kutenga bajeti ya kununua chombo cha teknolojia cha kumsaidia mwamuzi, VAR.

Mpaka sasa hatujapewa mrejesho kuwa imefikia wapi, lakini maneno yale yasiwe tu yametamkwa kwa sababu ya timu anayoipenda ilikuwa imenyimwa haki, yawe ya kweli kwani inaonekana kwa sasa VAR ni muhimu zaidi kuliko hata wakati ule aliokuwa akisema.

Kila muda unavyozidi kwenda ambapo wenzetu wanazidi kunufaika na VAR ndiyo hapa nchini waamuzi wanavyozidi kuvurunda na kuonekana kukifanya chombo hicho kionekane kinahitajika zaidi kuliko muda uliowekwa.

Hivi sasa waamuzi kupelekwa kwenye kamati yao siyo jambo la ajabu tena, waamuzi tena wale waliokuwa wanaaminiwa, wakiwa na beji za FIFA wamekuwa wakifanya makosa ambayo wakati mwingine ni ya kawaida sana na yalitakiwa kufanywa na wale ambao ni wageni kwenye fani hiyo.

Ukiiangalia Ligi Kuu Tanzania Bara tangu msimu uliopita, timu zimeonekana kujipanga kisawasawa kwenye usajili, zikileta 'vyuma' kutoka nje ya nchi na wamekuwa wakipambana sana uwanjani, lakini wakati mwingine zinakatishwa tamaa na refa ambaye maamuzi yake yanabadilisha kila kitu, matokeo na hata morali ya wachezaji na makocha.

Waliotengeneza na kukubali teknolojia hii itumike ni watu waliokaa wakafikiri inawezakana vipi makocha wapewe mamilioni ya pesa kuzifundisha timu mifumo mbalimbali ya kwenda kukabiliana na timu pinzani, halafu kila kitu kinakwenda sawa, lakini kosa moja la mwamuzi linabadilisha kila kitu?

Ni kwamba imefika wakati sasa hapa nchini maamuzi yanayofanyika uwanjani yote yawe sahihi, kama lilikuwa bao halali likakataliwa na mwamuzi, watu walio kwenye VAR watamwita kwenda kuangalia na atatoa haki. Iwe hata kinyume chake sawa tu, ili mradi haki imetendeka.

Mfano hapa nchini timu ndogo zimekuwa zikitesema mno. Kwanza wachezaji wake mishahara midogo, kambi duni, chakula cha kuungaunga, usafiri matatizo, halafu zinafika uwanjani zinapambana kwa kadri zinavyoweza, lakini anatokea mwamuzi mmoja tu, anawanyonga na kuwakatisha tamaa.

Ukweli ni kwamba, serikali, TFF na Bodi ya Ligi wanatakiwa kufanya mchakato huo haraka ili haki itendeke na ionekane kweli imetendeka.

Vyovyote iwavyo, kama waamuzi wanafanya hivyo kwa sababu za kibinadamu au kwa makusudi haitakiwi tena. Dunia imeshaanza kutoka huko. Na klabu za Tanzania nazo zianze kujiandaa kisaikolojia, si muda mrefu VAR itaanza kutumika.

Kama kulikuwa na michezo michafu inachezwa, huu ni wakati wa kuacha na kuanza kucheza soka, vinginevyo VAR itawapa tabu sana na kuonekana kama kuna uonevu, kumbe kuna timu zilizoea vya kunyonga na si kuchinja.  Siku zote ogopa kwanza Mungu kisha teknolojia.