Inavyoelekea uhaba ni karibu katika mikoa yote na ukweli ni kwamba wanafunzi wana matatizo ya sehemu salama za kujisaidia wakiwa shuleni.
Ni jambo ambalo sasa linatakiwa lifike mwisho kwa vile moja ya mahitaji muhimu ya binadamu wanapokuwa kwenye mkusanyiko iwe ni shuleni, nyumba za ibada, shuleni na hata kazini ni pamoja na chakula, maji na choo.
Inavyoelekea karibu asilimia zaidi ya 50 ya shule nchini huenda hazina vyoo na hiyo ni changamoto kwa wanafunzi wakiwamo wasio na mahitaji maalumu na wanaoishi na ulemavu.
Kinachoonekana sasa ni walimu, wazazi na walezi na viongozi wa kamati za shule kwa zile za msingi na bodi kwa sekondari na viongozi wa halmashauri kufanya utafiti pamoja na kuamua jinsi ya kuwashirikisha wanafunzi na jamii kuchimba mashimo ya vyoo na kukabiliana na ukosefu huo.
Wakati mwingine inaweza kuwa rahisi kujenga vyoo kama kutakuwapo na mashimo yaliyochimbwa kama ambavyo zama hizi wananchi wanajenga maboma na serikali inayakamilisha kwa kuyaezeka, kuweka milango, madirisha, rangi na kumalizia kwa samani na hapa shule imekamilika.
Kushindwa kuwapatia watoto huduma ya choo bora ambayo ni muhimu kwa afya inasababisha watoto hao kuchukia au hata kutoroka shule kwa kuona kuwa ni kero, kwa upande wa mabinti nao ni tatizo, hasa wanapokuwa kwenye mzunguko wa kila mwezi.
Ikumbukwe uhaba wa vyoo umechangia baadhi ya wanafunzi kupata maradhi kama ya tumbo na maambukizi ya njia ya mkojo (UTI) na hata kuwakwamisha kitaaluma kutokana na utoro wa mara kwa mara wapo wanaomaliza darasa la saba hawajui kusoma na kuandika.
Ni vyema serikali za wilaya ziandae utaratibu wa kujengwa vyoo vikiwamo vya wanafunzi wenye changamoto za ulemavu zinazowarudisha nyuma wakati wa kujifunza kwa vile ukosefu wa choo au kuwapo na vyoo vibovu, vichafu visivyo na viwango vya mahitaji ya kundi hilo, kunawaumiza zaidi wanaoishi na ulemavu.Ukiacha madai kuwa jamii haina shule wala mabweni ni lazima pia kuzungumzia umuhimu wa walimu, wazazi na walezi kushirikiana na kujenga vyoo kwani hata wao wana nafasi kubwa ya kuchangia tatizo hili la kukosa vyoo listokee.
Zipo changamoto nyingi zinazomrudisha nyuma mtoto katika kujifunza si shuleni pekee hata nyumbani, ikiwamo kukoseshwa raha na mazingira anayosomea na kuchukuliwa na wanafunzi wengine kama ana tatizo na hata kutengwa na kunyanyapaliwa kutokana na hali unayoweza kuwa nayo.
Eneo hili linawahusu wasichana na wenye ulemavu ambao kutokana na hali ya kimaumbile wanalazimika kuhitaji huduma hiyo zaidi kuliko wengine.
Lakini mtoto hasa binti anashindwa kuzitolea taarifa changamoto anazokutana nazo wakati wa hedhi kutokana na kukosekana maji na vyoo shuleni.
Kwa sababu ya kukosekana mazingira rafiki kati yake na mzazi, mlezi au mwalimu ikiwamo ukali uliopitiliza anaamua kuvumilia lakini akishindwa kujifunza na kurudi nyuma kimasomo na kitaaluma.
Kuna haja ya wazazi na walezi kuongeza ukaribu na walimu watoto wao shuleni ili kutatua mambo yoyote yanayowakwamisha ukiwapo uhaba wa vyoo na kuwasababishia kuichukia shule na kuiona kama sehemu yenye kinyaa, yenye harufu mbaya, inzi na hata inayokera kukaa.
Lakini wazazi na walezi ni wakati wa kutenga muda wa kutembelea shule na kushirikiana na walimu, viongozi wa serikali na watoto wenu ili kutambua changamoto wanazopitia.
Suala la kumsaidia mtoto kielimu linahusisha pia kugundua changamoto zinazokabili katika kujifunza na kuzitafutia ufumbuzi na hilo ni jukumu la mzazi, walimu na mlezi.
Kwa maana hiyo ikiwa wazazi na walezi mmetambua changamoto saidieneni na walimu kuzimaliza ili kuwasaidia watoto wawe darasani kwa furaha na kupenda masomo.
Wazazi wengi na walezi wana dhana ya kuwa suala la elimu ni jukumu la serikali jambo ambalo sio kweli kwa sababu ujenzi wa choo wakati mwingine ni kazi ya serikali lakini hata wazazi pia.
Ni wakati wa wazazi na walezi kuamka na kubeba jukumu hili muhimu la kumsaidia mtoto kupambana na changamoto zinazomrudisha nyuma kimasomo ili kutokomeza tatizo la watoto kujifunza kwenye mazingira machafu yanayopambwa na kinyesi.