Hongera waliojitosa kuokoa maisha Bukoba

16Nov 2022
Golden Kisapile, TUDARCo
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Hongera waliojitosa kuokoa maisha Bukoba

HONGERA Watanzania kwa kuthubutu kuwaokoa wenzetu katika mazingira hatarishi bila kujali kama kuna kuumia hata kufa.

Wakati yanapotokea majanga hasa ajali, moto kulipuka, majengo na miundombinu kubomoka hata mafuriko, inaweza kuwa vigumu kujitosa kusaidia waathirika.

Lakini, ukweli unabaki kuwa kuwasaidia walio katika hatari ndiyo njia ya kuokoa maisha na kupunguza madhara yanayoweza kuwafika binadamu.

Wataalamu wa majanga na kukabiliana na kiwewe, shoki na mfadhaiko (trauma) wanasema msaada wa haraka ndiyo wa muhimu kuliko chochote na unatakiwa kupatikana ndani ya dakika 60 au saa moja baada ya ajali.

Nikumbushe kuwa mnamo Novemba 6, mwaka huu ilitokea ajali ya ndege katika Ziwa Victoria na kusababisha abiria wa ndege 19 kupoteza maisha na wengine 24 wakiokolewa na wavuvi wasamaria wema akiwamo Jackson Majaliwa, aliyefanyakazi ya ziada kuwasaidia.

Ni pongezi kwa kila mmoja aliyekuwapo wakati ajali inatokea na kutoa msaada huo bila kujali kuwa ilikuwa ni ndani ya maji.

Zipo ajali za moto, za barabarani, mafuriko na hata kuangukiwa na majengo ambazo zilitokea na baadhi kusabaisha maafa kwenye jamii.

Lakini wapo Watanzania waliopambana kuwaokoa na kuwasaidia wengine kwenye ajali mbalimbali bila kujali hatima zao.

Ni wazi kuwa kuwanusuru na kuwaokoa waathirika kunapunguza vifo vya wazee, wagonjwa, watoto, vijana na kunusuru nguvu kazi inayohitajika mno katika jamii tunayoishi.

Kunusuru watu kunapunguza idadi ya walemavu na wategemezi katika jamii wakiwamo ombaomba ambao wanakosa walezi au wahitaji.

Tukumbuke kuwa kuwa waathirika wa ajali kuanzia za barabarani na nyinginezo wasiposaidiwa na kuokolewa kwa haraka pamoja kupoteza maisha wengine hupoteza viungo kama vile mikono, miguu na kuwa walemavu wa kudumu na hupelekea kuwa tegemezi kwa ndugu, jamaa na marafiki.

Ni kuwa endapo msaada utatokea wahusika kama kwenye ajali za moto, au za barabarani watanusurika na idadi ya walemavu katika jamii wanaotokana na ajali inapungua pia.

Ajali ni mwiba inakwamisha watu kufikia malengo yao ya kimaisha kwa ujumla, mfano kama baba au mama akipata ajali atakaye athirika ni watoto na wategemezi wao.

Inaweza kukwamisha masoma ina maana atakatisha masomo, ataacha shule, ataondoka bweni au mengine mengi yanayokwamisha.

Ni wazi kuwa kama aliyeumia au kupoteza viungo kwenye ajali anafanya biashara atasitisha kufanya ndoto yake na hatimaye kupelekea kutofikia malengo fulani, kwa hiyo endapo angeokolewa inakuwa na tija pamoja na hao wanaowategemea.

Ni wazi kuwa mfululizo wa ajali una athari kichumi ambao unashuka, kama mtu amepatwa na ajali na asipookolewa kwa wakati kama atanusurika itapelekea awe mlemavu na kushindwa kufanya shughuli zake za kila siku kama vile uzalishaji yote hayo huweka uchumi pabaya.

Matokeo yake ni kukosa pato lake la kila siku na hushindwa kuchangia tozo na kodi katika mfuko wa serikali, hatimaye uchumi wa taifa huweza kushuka kutokana na ajali za mara kwa mara.

Kwa hiyo kuwaokoa wengine wakati wa ajali ni jambo jema na la muhimu ili waweze kufanya shughuli zao za kila siku hususan zile za kiuchumi, maendeleo ya jamii na taifa.

Kuokoa ni suala jingine, lakini zipo zinazozuilika, ningetoa rai watu wote kuwa wakati mwingine ni kujitahidi kujaribu kila linalowezekana kuzuia ajali zisitokee.

Kama taifa si kila mmoja anaweza kukimbilia kuokoa kuna kamati zinazohusika na maafa ni vyema serikali izioongezee nguvu ya kuokoa watu wakati ajali zinapotokea.

Isifike wakati watu wakaumia lakini wakakosa msaada na kuumia hata kupoteza maisha. Uwezesha uangalie miundombinu, nguvu kazi na maslahi kwa wahusika.