Hatua hiyo, ni habari njema kwa wanafunzi waliokuwa tayari wamekata tamaa ya kuanza masomo. Pia ni ya kuungwa mkono kutokana na serikali kuona umuhimu wa kufadhili wanafunzi hao.
Kilio hicho cha wanafunzi kimesikika, baada ya wiki iliyopita Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alipoahirisha Mkutano wa Tisa wa Bunge la 12, hadi Januari 31, 2023 akitoa kauli ya kuwapatia wanafunzi hao mikopo.
Sakata hilo la wanafunzi hao, liliibuliwa na wabunge akiongozwa na Mbunge wa Biharamulo (CCM), Ezra Chilewesa, alipoomba bunge kuahirisha shughuli zilizopangwa kwa muda, ili kujadili tatizo la wanafunzi kukosa mikopo ya elimu ya juu.
Hoja hiyo iliungwa mkono na wabunge na Spika, Dk. Tulia Ackson, akitoa nafasi ijadiliwe na hatimaye bunge liliazimia wanafunzi hao wawezeshwe fedha za kujikimu ili kuendelea na masomo.
Wabunge hapa wametimiza vyema majukumu ya kuisimamia serikali, kama ambavyo katiba inawataka kufanya hivyo.
Wabunge walijadili hoja hiyo, iliyotokana na maazimio ya bunge ya taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali iliyowasilishwa tarehe 5, mwezi huu kuhusu kuifanyia ukaguzi wa kina Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu katika mchakato mzima wa ugharamiaji, upangaji, utoaji na urejeshaji mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu nchini.
Tayari bodi hiyo imekwishatoa tangazo la kuridhia kauli ya serikali ya kuwapatia mikopo wanafunzi 28,000 wenye sifa za kupata mikopo, lakini hawakupokewa vyuoni na kusajiliwa ili kuendelea na masomo.
Kupitia Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, Abdul-Razaq Badru, bodi pia imefungua dirisha la rufani ili kutoa fursa kwa wanafunzi ambao hawakuridhika na viwango vya mikopo walivyopangiwa, kuwasilisha taarifa za uthibitisho ili kuongezewa viwango vya mikopo ikilinganishwa na uhitaji wao.
Kwa sasa, kuna jumla ya wanafunzi watakaotakiwa kuzingatia taratibu za uwasilishaji wa rufani hizo, kwa njia ya mtandao, ambazo ziko katika tovuti ya bodi. Lengo la bodi ni kuwapatia mikopo wanafunzi wapya 71,000 katika mwaka wa masomo uliokwishaanza.
Ni jambo la kuipongeza serikali kwa hatua hiyo ya kuwapatia wanafunzi wenye sifa za kupata mikopo, kwa sababu ni fedha ambazo wataanza kuzirejesha baada ya kuhitimu masomo yao ya elimu ya juu.
Faida ambayo wanafunzi watapata kutokana na mikopo hiyo, ni pamoja na fedha za kujikumu, gharama za chakula na malazi, ada ya mafunzo, vitabu na nyenzo za kuandiki, mahitaji maalum ya vitivo na idara, utafiti pamoja na mafunzo kwa vitendo.
Mikopo hiyo, pia inasaidia kuondoa mzigo kwa wazazi ama walezi wa wanafunzi hao, kwa sababu kwa kiwango kikubwa wanatoka katika familia duni na wanaotegemea kilimo na ufugaji kama njia ya kupata fedha za kuendesha maisha.
Suala hilo la kuwapa mikopo wanafunzi, naamini litaondoa kabisa msongo wa mawazo wawapo vyuoni na kuwa na umakini zaidi, kwa kile wanachofundishwa darasani, maana tayari watakuwa na uhakika wa fedha. Ni hatua moja ya kisafari kumpata mtaalamu sahihi na mwenye weledi.
Vilevile, kwa wanafunzi itakuwa ni vigumu kwao kujiingiza katika vitendo visivyofaa kama ukahaba, rushwa ya ngono na hata matumizi ya vilevi ambavyo mara nyingi wanapata kwa walio nacho na hawajali kuwa mwanafunzi anatakiwa kusoma na maisha ya kujichunga.
Changamoto kubwa ambayo wanafunzi watakabiliana nayo hasa wanaoishi mkoa wa Dar es Salaam, ni tatizo kubwa la uhaba wa maji, ambao unatokana na mabadiliko ya tabianchi. Hata hivyo ni habari njema sasa serikali inajitahidi kulitatua, kama tunavyotaarifiwa kwa namna mbalimbali.