Mkidanganya mitihani mnaiangamiza Tanzania

15Nov 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mkidanganya mitihani mnaiangamiza Tanzania

OKTOBA ulikuwa mwanzo wa kipindi cha miezi miwili cha mitihani ya darasa la nne, la saba, kidato cha pili na sasa kidato cha nne.

Jukumu hilo linazihusu shule za msingi na sekondari na sasa mtihani ni ya kumaliza elimu ya sekondari.

Hata hivyo, moja ya tatizo kubwa sekta ya elimu ni udanganyifu wa mitihani. Ni kawaida kusikia Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) likitangaza kuwatuhumu walimu, wakuu wa shule, wanafunzi na wasimamizi pamoja na kufuta matokeo ya shule au vituo kadhaa kwa sababu za udanganyifu na utovu wa nidhamu katika mitihani ya sekondari na msingi.

Tunaona kuwa shinikizo la kutaka watoto wafanye vizuri hata kama hawana uwezo linawaweka walimu, wazazi, walezi na wasimamizi wa shule mara kadhaa kwenye kuhusishwa na udanganyifu wa mitihani kwa wanafunzi wao.

Hitaji hilo au shinikizo kutoka kwa wazazi, walimu kwa watoto kupata alama bora za juu na kuleta sifa kwa shule limekuwa jambo muhimu katika kuchochea tabia mbaya za wizi na udanganyifu wa mitihani.

Aidha, hatukosoi lakini tunazifahamu na kuzifuatilia juhudi za kurekebisha mitaala ndipo tunapopata uthubutu wa kusema kuwa mfumo wa sasa wa elimu unaonekana kusisitiza madaraja kwa kutizama (kufaulu kwa mitihani) ukichukuliwa kama jambo la sifa badala ya kutoa maarifa.

Tunajua kuwa zipo shule zinazolenga kupata alama nzuri za juu tena kuwa bora ili kuvutia wanafunzi zaidi na kujipatia fedha kutokana na utitiri wa watakaojiunga nazo na hivyo kupata mapato ya ziada.

Lakini, tunazidi kusisitiza kuwa mitihani ya udanganyifu inabakia kuwa tabia mbaya yenye madhara ya muda mrefu kwa watu binafsi na nchi, ni kuzalisha mbumbumbu na kujidanganya kuwa wewe ni bora wakati ukweli ni huna uwezo.

Tanzania inakabiliwa na changamoto za watumishi wa umma na wafanyakazi wanaotokana na maadili mabovu, wasio na uadilifu na pia mafisadi yote hayo ni matokeo ya kuwa na mienendo ya kukosa uaminifu kuanzia kwenye mitihani na uongo kwenye mitindo ya maisha.

Ukweli ni kwamba huwezi kuwa raia mwadilifu kama unatokana na kuanza kudanganya mitihani ukiwa mwanafunzi wa shule ya msingi, ukazidi kuharibu ukiwa kidato cha nne, sita na hata vyuo vikuu. Wewe si raia mwema wala mwadilifu.

Tunawakumbusha wazazi, walezi, walimu, wamiliki wa shule na wasimamizi kuwa ufike kipindi waache tabia mbaya ya wizi kwa vile mwizi au mharibifu, hatarajiwi baadaye maishani abadilike na kuachana na mienendo hiyo mibovu ambayo ndiyo msingi wa maisha yake.

Tunaona kuwa kuanza kudanganya mitihani ili upate fedha kwa wazazi na walezi na shule yako ionekane kidedea ni kupanda mbegu mbaya kwa Watanzania, ambayo inaharibu ustawi wa taifa kwa miongo mingi.

Tunaikumbusha NECTA, serikali, shule binafsi na za umma, walimu, wasimamizi, watahiniwa, walezi, wazazi, walimu na wasimamizi kuwa njia mbaya siku zote huishia katika matokeo mabaya.

Kama tunaandaa wasomi ili wawe rasilimali watu kwa njia mbaya za wizi, hawatakuwa waaminifu wala watiifu na nchi haiwezi kuendelea kwa sababu masuala ya kutokuwa na taaluma bora zilizotokana na rushwa yataangusha juhudi zote chanya ambazo taifa linawekeza ili kufikia maendeleo endelevu.

Ni wakati wa kuwa na taasisi ya kupambana, kuchunguza, kukomesha rushwa kwenye mitihani ili Tanzania iondoke kwenye shimo la maangamizo linalotokana na kuwa na wasomi, viongozi na nguvukazi iliyozalishwa kwa njia ya wizi na udanganyifu wa mitihani.