Uwekezaji zaidi unahitajika  Simba Queens kutisha CAF

14Nov 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Uwekezaji zaidi unahitajika  Simba Queens kutisha CAF

MSIMU wa Ligi ya Mabingwa Afrika 2022/23 kwa Wanawake ulifikia tamati mwishoni mwa wiki baada ya fainali iliyowakutanisha mabingwa watetezi, Mamelodi Sundowns Ladies ya Afrika Kusini dhidi ya wenyeji wa michuano hiyo, ASFAR FC ya Morocco, kupigwa jana.

Katika michuano hiyo iliyokuwa ikifanyika Morocco, ilijumuisha mabingwa wa Kanda Nane za Afrika, ambapo kwa Afrika Mashariki na Kati, iliwakilishwa vema na Simba Queens iliyomaliza nafasi ya nne baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Bayelsa Queens FC ya Nigeria katika mechi ya kuwania mshindi wa tatu juzi usiku.

Kwa ujumla ilikuwa ni michuano migumu na ya ushindani mkubwa kwani timu zilizoshiriki mbali na kwamba ni mabingwa wa nchi zao, lakini pia ndizo mabingwa wa kanda zao.

Kwa upande wa Simba Queens ambayo ilikuwa Kundi A lililokuwa likiundwa na Green Buffaloes ya Zambia, Determine Girls ya Liberia na wenyeji ASFAR FC, hadi inashika nafasi ya nne ilishinda jumla ya mechi mbili na kupoteza tatu kwa mbinde.

Simba Queens ilianza kwa kupoteza kwa bao 1-0 katika mechi ya ufunguzi dhidi ya ASFAR FC kisha ikashinda 2-0 dhidi ya Determine Girls kabla ya kuichapa Green Buffaloes 2-0 na kutinga nusu fainali.

Nusu fainali Simba Queens ilikutana na bingwa mtetezi, Mamelodi Sundowns Ladies na kutolewa kwa tabu baada ya kufungwa bao 1-0, hivyo kuangukia kuwania nafasi ya tatu ambapo ilipokea kipigo kingine kama hicho kutoka kwa Bayelsa Queens FC .

Hata hivyo, kwa namna Simba Queens ilivyoonyesha uwezo mkubwa katika michuano hiyo, tunaamini kama uongozi wa klabu hiyo utafanya uwekezaji mkubwa inaweza kuutwaa ubingwa huo msimu ujao.

Katika hili, tunashawishika kusema kwamba umefika wakati kwa klabu zetu kuweka nguvu kubwa na kutoa kipaumbele kwa timu za wanawake kama ilivyo kwa zile za wanaume kwani hilo likifanyika Tanzania inaweza kuanza kuimbwa kwa ubora wa soka la wanawake ndani ya kipindi kifupi.

Ni wazi kwa kipindi hiki ambacho soka la wanawake linashika kasi kwa haraka barani Afrika, Tanzania inapaswa kukimbia kwani kuna vipaji vingi na kilichobaki ni kuhamasisha mchezo huo na kuwekeza zaidi ili kupata mafanikio mapema.

Hilo tumeliona pia kwa uwezo ulionyeshwa kwenye kikosi cha Timu ya Taifa ya Wanawake chini ya miaka 17, Serengeti Girls, ilipofanya maajabu kwenye Kombe la Dunia mwaka huu kwa kutinga robo fainali huku ikizifunga timu ngumu za Canada na Ufaransa.

Hilo linatufanya tuamini pia kwa uwezo ulioonyeshwa na kikosi cha Simba Queens kwenye michuano ya CAF, kinahitaji maboresho kidogo tu ili kwenda kufanya makubwa msimu ujao wa mashindano hayo, hivyo ni wakati sasa kwa klabu hiyo kuanza kuijenga kwa ajili ya msimu ujao.

Lakini wadau wa soka hawana budi kujitokeza kwa wingi kuwekeza kwenye Ligi Kuu ya Wanawake nchini kwa kutoa udhamini hadi kwenye klabu shiriki ili kuongeza ushindani zaidi jambo ambalo litasaidia kupata mwakilishi bora wa Tanzania kimataifa katika mashindano yajayo.