Magonjwa yasiyo ya kuambukiza ni yale ambayo hayasambazwi kwa mtu mwingine kwa kuwa hakuna vimelea mwilini vinavyohusiana na magonjwa hayo. Magonjwa hayo ni moyo, shinikizo la damu, figo, saratani, kifua sugu, kisukari, magonjwa ya akili, magonjwa ya kinywa na meno na mengine ya kurithi kama vile ugonjwa wa selimundu.
Tanzania, katika mpango wa upimaji wa afya kwa magonjwa yasiyoambukiza jijini Dar es Salaam, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umebaini kuwa idadi kubwa ya wanaume wanapatwa na magonjwa hayo kuliko wanawake.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mfuko wa Bima ya Afya, athari ya magonjwa yasiyoambukiza ni mara nne zaidi ya watu waliopo mijini kuliko vijijini, huku asilimia 12.8 ya wanaougua wakiwa wako mijini na asilimia 3.1 wako vijijini kutokana na mfumo wa maisha.
Magonjwa yasiyo ya kuambukiza yanaelezwa kusababishwa na ulaji usiofaa na mtindo usio bora wa maisha kwa kutumia vyakula vyenye chumvi nyingi, mafuta mengi au vinywaji vyenye sukari nyingi ikiwa ni miongoni mwa viashiria hatarishi vya kupata magonjwa yasiyoambukiza.
Kulingana na utafiti mbalimbali uliofanywa, unaonesha kuwa kuna ongezeko kubwa la watu wenye uzito uliozidi pamoja unene uliokithiri na kuwaweka watu kwenye hatari ya kupata tatizo la magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama kisukari, saratani pamoja na magonjwa ya moyo na shinikizo la damu.
Mtindo usio bora wa maisha ni kutofanya mazoezi, matumizi ya sigara na tumbaku pamoja na unywaji wa pombe ambavyo husababisha mtu kupata magonjwa hayo.
Magonjwa hayo yana athari kubwa katika maendeleo ya taifa, lakini yanawezekana kudhibitiwa endapo elimu kwa jamii itatolewa kwa kuandika taarifa sahihi ili watu waweze kufuata taratibu za ulaji unaofaa na mtindo bora wa maisha.
Kwa mujibu wa Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa la Usalama, John Ashe, mwelekeo wa kufa kwa magonjwa hayo ni asilimia 10 kwenye nchi zilizoendelea na asilimia 60 kwenye nchi zinazoendelea. Tofauti hiyo kubwa inakumbusha kwamba suluhu la jumla linaomba ushirikiano wa wadau wote kupambana na magonjwa hayo ili watu wasiendelee kuathiriwa.
Ili kudhibiti magonjwa hayo yasishambulie zaidi, watu wanashauriwa kula mlo ulio bora na kuzingatia mazoezi.
Inashauriwa watu wapunguze vyakula vyenye mafuta mengi, chumvi na sukari nyingi na kupunguza kula vyakula vyenye wanga ambavyo husababisha uzito kuongezeka.
Ufanyaji mazoezi unashauriwa ufanyike kila siku kwa muda usiopungua nusu saa ili mishipa ya damu iweze kufanyakazi yake vizuri na viungo vya mwili viweze kujiendesha vizuri.
Watu wajiepushe kupenda kukaa sehemu moja muda mrefu na badala yake watembee ili kunyoosha viungo viweze kufanyakazi vizuri.
Pia inashauriwa muda wa jioni watu wale vyakula laini badala ya vizito na chakula kiliwe mapema muda wa saa 12 jioni hadi saa moja usiku ili kiweze kusagika vizuri tumboni.