Taarifa zinaeleza kuwa kuna mashauri mengine matano yakiendelea kufanyiwa kazi kwa sababu hizo hizo.
Kati ya mashauri hayo manne yanadaiwa kutoka katika Halmashauri ya Chalinze na moja Bagamoyo ambayo yanahusisha tuhuma mbalimbali zikiwamo za kujihusisha na mapenzi na wanafunzi pamoja na ulevi uliokithiri.
Walimu ni tegemeo kubwa la kulea watoto na kuwafundisha tabia njema, baada ya wazazi walimu hao huwa ni walezi wa pili wanaotegemewa kuwalea watoto hao katika maadili mema.
Lakini kutokana na taarifa zilizotolewa na walimu waliopatwa na mkasa huo wanahusishwa na utoro, ulevi na kujihusisha kimapenzi na wanafunzi.
Kama shuleni ndiko wazazi wanaamini ni mahala salama pa watoto wao kufundishwa masomo na tabia njema, halafu watu wanaoaminiwa ndio wanao waharibu, sasa wapelekwe wapi?
Imeelezwa kuwa walimu hao wanadaiwa kufukuzwa katika kipindi cha miaka miwili kuanzia 2020 hadi Septemba 2022.
Taarifa hizo za kufukuzwa kwa walimu hao zilitolewa mjini Bagamoyo na Katibu wa Tume ya Utumishi wilayani humo, Fedinand Ndomba, alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa wa Chama Cha Walimu.
Alisema, tabia hiyo ya utoro kwa baadhi ya walimu inachangia kushuka kwa kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi
Uamuzi wa kuwafuta kazi walimu hao umefanyika ili iwe fundisho kwa watumishi wengine wenye tabia kama hizo ambao wanasababisha kushuka kwa elimu.
Haishangazi kuona watoto wanasoma kutoka darasa la kwanza mpaka wanapomaliza darasa la saba baadhi yao hawajui kusoma wala kuandika.
Hiyo inatokana na watoto hao kushindwa kufuatiliwa na walimu wao na hata wazazi pia ni wa kulaumiwa kwa kushindwa kufuatilia nyendo za watoto wao na badala yake kuwaachia jukumu hilo walimu peke yao.
Katibu huyo alisema, kuna baadhi ya walimu pia hususani wa kiume wamekuwa wakijihusisha na mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi, watoto ambao wamepewa dhamana ya kuwalea, kuwatunza, lakini wamebadilika na kuwaharibia maisha na ndoto zao.
Licha ya Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Wilaya ya Bagamoyo, Hamis Kimeze, kuelezea vikwazo vinavyowakabili walimu ikiwamo kucheleweshwa kwa fedha za uhamisho pamoja na malipo kwa wastaafu, lakini kisiwe kigezo cha wao kufanya mambo yasiyofaa katika jamii na kuonyesha mifano mibaya.
Hata hivyo, Katibu Tawala Wilaya ya Bagamoyo Kasilda Mgeni, aliyemwakilisha Mkuu wa wilaya alikemea vitendo viovu vinavyofanywa na walimu na kusema kamwe hatovifumbia macho.
Akizungumzia tuhuma za baadhi ya walimu kujiingiza kwenye mapenzi na wanafunzi, alisema zitafanyiwa kazi na hatua zitachukuliwa kukomesha tabia hiyo.
Kauli aliyoitoa Katibu Tawala inatia matumaini ili kudhibiti vitendo viovu vinavyofanywa na baadhi ya walimu wasio na maadili ya kazi zao.
Vitendo vya udhalilishaji na ukatili dhidi ya watoto vinapigwa vita kila siku na walimu wanatakiwa kuwa mfano bora kwa watoto waliokabidhwa kuwalea badala ya kuwafundisha vitendo vibaya.










