Mtoto wa kike alindwe, asikatishwe ndoto zake

12Oct 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mtoto wa kike alindwe, asikatishwe ndoto zake

MAADHIMISHO ya Siku ya Mtoto wa Kike Duniani na kaulimbiu yake ya ‘Sauti Yangu, ni Usawa wa Baadaye’ ni muhimu katika kumthamini na kumwezesha kufikia malengo aliyojiwekea katika maisha yake.

Changamoto kubwa wanayokabiliana nayo watoto wa kike ni vikwazo vya safari yao ya kuelekea utu uzima, huku mimba na ndoa za utotoni zikiwalazimisha kuacha shule na kukatisha ndoto zao za elimu.

Hivyo ni jukumu la kila mtu kuchukua hatua na kuwapa fursa watoto wa kike kutimiza ndoto zao na kuimarisha maisha yao.

Kitu kibaya kinachosikitisha ni kuona watoto wengi wa kike hukatishwa ndoto zao na watu wa karibu tena kutoka ndani ya familia.

Takwimu kwa upande wa Tanzania Visiwani zinaonesha kwamba jumla ya matukio 1,222 ya udhalilishaji yaliyoripotiwa kwa mwaka 2021 kati ya hayo 846 ni wasichana sawa na asilimia 79.2.

Kwa mwaka huu wa 2022 kuanzia Januari hadi Agosti jumla ya matukio 695 ya udhalilishaji yameripotiwa, kati ya hayo 481 ni wasichana.

Kiwango hicho ni kikubwa ikilinganishwa na idadi ya watu waliomo visiwani humo na hiyo ni miongoni mwa changamoto zinazokwamisha mwelekeo wa ndoto za watoto.

Udhalilishaji wa watoto wa kike hujitokeza kwa wingi visiwani humo kutokana na ripoti za matukio yanayoripotiwa mara kwa mara kwenye vyombo vya habari na hata kesi zinazowasilishwa mahakamani.

Watoto wa kike wanakabiliwa na vipingamizi vingi ndani na nje ya familia kwa kufanyiwa vitendo vinavyowasababisha washindwe kufikia ndoto zao za malengo waliyojiwekea.

Katika baadhi ya familia mtoto wa kike hutumika kama kitega uchumi cha kuiletea familia fedha. Mfano mzazi anaweza kuamuru mtoto huyo asiende shule ili aolewe kwa kutegemea mahari ambayo wakati mwingine huwa mifugo au fedha.

Mtoto huyo hupatiwa mume ambaye kiumri hupishana sana na kusababisha mtoto huyo kupata madhara hasa anapopata ujauzito kutokana na viungo vyake kutokomaa.

Wazazi hao wanashindwa kuelewa kuwa mtoto wa kike anapopatiwa fursa ya kuendelea kielimu anakuwa mkombozi mkubwa si kwa familia pekee bali hata kwa jamii inayomzunguka.

Kuna mifano tosha inayoonekana katika jamii mbalimbali watoto wa kike waliopewa fursa ya kuendelea kielimu wanavyoweza kuikomboa familia na vile vile kusaidia wengine kufikia ndoto zao.

Mtoto wa kike akijengewa uwezo ni mlezi mkubwa wa familia na mifano ipo ya kutosha katika baadhi ya familia, watoto wa kike ndio wanaotunza wazazi wao kwa asilimia kubwa.

Mtoto wa kike ameumbwa kuwa na huruma hata anapokuwa na familia yake ni lazima atakumbuka jukumu la kuwatunza wazazi wake.

Dunia sasa hivi inashuhudia watoto wa kike waliowezeshwa wanavyoweza kufanya maajabu na kuwapita hata wenzao wa kiume. Sasa hivi kuna marais wanawake jambo ambalo hapo zamani lilikuwa gumu kutokana na mfumo dume uliojengeka.

Mtoto wa kike ni lazima athaminiwe na kuwezeshwa kutimiza ndoto yake.