Kupanda bei kwa vyakula katika maeneo mbalimbali nchini, ingekuwa ni vyema kama kungedhibitiwa, kwani vinginevyo mfumuko huo, unaweza kusababisha baadhi kushindwa kumudu milo mitatu kwa siku.
Upandaji bei huo umesababisha mchele kuuzwa shilingi 2,800 hadi 3,000 kwa kilo, huku unga wa mahindi ukiuzwa kati ya shilingi 1,600 hadi 1,800 kwa kilo na maharage shilingi 1,800 hadi 3,000 kwa kilo.
Sio kipindi kirefu miezi ya nyuma, kilo moja ya mchele ilianzia shilingi 1,600 hadi shilingi 2,000 huku unga wa mahindi ukiuzwa shilingi 1,200 kwa kilo, maharage shilingi 2,200 hadi 2,400 kwa kilo.
Bei ni hiyo ninayoielezea kwa baadhi ya maeneo ya jiji la Dar es Salaam, ikiwamo Mbezi Luis, lakini imepanda, hali inayotishia milo ya watu, hasa kutokana na ukweli kwamba wengi wao ni wale wa maisha ya kawaida.
Ingekuwa ni vyema kama Serikali ingefanya jitihada zaidi kwa ajili ya kudhibiti mfumuko huo wa bei, ili kuwapa Watanzania unafuu wa maisha, ni takriban kila kona ya nchi wanalalamikia upandaji huo wa bei ya vyakula.
Ninajua zipo sababu mbalimbali zinazotajwa kuchangia mfumuko huo, ikiwamo mabadiliko ya tabianchi, pia baadhi ya wafanyabiashara wa nje ya nchi kuja kununua vyakula na kwenda kuuza kwao.
Kwa mfano, hivi karibuni wananchi mjini Bukoba, mkoani Kagera, walikaririwa na vyombo vya habari wakidai kuwa kuna wafanyabiashara kutoka nchi jirani wanaingia mkoani humo na kununua mazao yote.
Wakadai kuwa kuingia wafanyabiashara hao kutoka nje ya nchi, kumesababisha bei ya vyakula kuwa juu na kuwafanya wawe na wakati mgumu, kwa kuwa hawana uwezo wa kumudu gharama mpya.
Hatua hiyo pia imesababisha hata mamalishe na baadhi ya migahawa kupanda bei ya vyakula, hali ambayo kwa ujumla inaweza kufanya baadhi ya watu kujibana na kula mlo mmoja kwa siku.
Katika mazingira hayo, bado hakujawa na dalili ya bei kushuka, hivyo ingekuwa vyema kama chanzo cha mfumuko huo kingedhibitiwa na kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu, ili Watanzania waondokane na adha hii.
Mtaalamu mmoja wa uchumi anasema, mfumuko wa bei kama huo ambao unaonekana mwiba kwa wananchi, njia inayoweza kutumika haraka kuondoa makali yake ni kuongeza uwezo wa ununuaji wa mtu wa kawaida.
Kwamba hakuna njia ya mkato kwenye mfumuko wa bei, bali ni lazima watu wawe na kipato, kwa kuwa bila kipato, ni vigumu kwa mtu kuweza kununua bidhaa, hasa pale inapopanda bei.
Pia kunaelezwa kwamba, kuna haja kwa serikali kupunguza au uondoaji wa kodi kwenye bidhaa zote muhimu zilizoathirika na bei, hususani ngano, mafuta ya kula na sukari, ili kuwapa unafuu wananchi.
Lingine, Serikali inashauriwa kubana matumizi yake ili kufidia kufutwa kwa kodi au punguzo la kodi katika vyakula, kwa kuwa ni vigumu wananchi kukabiliana na mfumuko wa bei kama hakuna mbinu za kuwanusuru.
Upandaji bei umehusisha pia bidhaa zinazotokana na mazao ya chakula na vinywaji, na bidhaa za viwandani, ambazo siyo chakula. Hivyo kila upande ungetafutiwa ufumbuzi wake, ili kuwapa wananchi unafuu wa maisha.