Klabu hizi ziliundwa katikati ya miaka ya 1930 kwa minajiri ya kutoa burudani, kudumisha undugu na umoja, na baadaye zikawa chachu cha kuusaka Uhuru wa Tanzania.
Kuna dhana imejengeka kuwa ni klabu moja tu ndiyo iliyotumika kudai uhuru, lakini ukweli ni kwamba Chama cha TANU kilizitumia klabu zote mbili kudai uhuru na ukapatikana mwaka 1961.
Klabu ya Yanga ilianzishwa mwaka 1935 na Simba ikaanzishwa mwaka mmoja baadaye, na waanzilishi wengi wao walikuwa ni wale waliojiengua kutoka Yanga.
Ukitembelea kwa sasa kwenye mitandao ya kijamii na baadhi ya vijiwe vya soka, utaona kabisa athari za waliokuja baadaye kujiita wasemaji wa klabu walivyowafanya mashabiki wa timu hizi mbili kuwa maadui badala ya watani wa jadi.
Unakutana na matusi, kuvunjiana heshima, dharau, badala ya utani ule ambao umezoeleka huko nyuma.
Nina uhakika Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Abeid Amani Karume kama wangeona uhasamu wenyewe ndiyo kama huu wa sasa wangeweza kuzipiga marufuku klabu hizi.
Lakini, walizilea na kuzipa kila aina ya msaada kwa sababu pamoja na kuzitumia kukusanya watu, kuzitumia kisiasa, kudumisha amani na umoja, pamoja na kuwa na ushirikiano.
Mfano, mwanachama au shabiki wa Simba wa Morogoro, leo anaweza kwenda Mwanza, anaweza kuwa hana ndugu, lakini akakuta tawi la klabu yake, akajieleza akapewa msaada na kuhudumiwa kama vile ndugu yao au mtu wanayemfahamu. Kumbe tu wote ni mashabiki wa timu moja.
Mtu anaweza kuwa shabiki wa Yanga, halafu ndugu yake Simba, huku anaweza kumuacha kumpa msaada mdugu yake na kumsaidia mtu asiyemfahamu, kwa sababu tu ni Yanga mwenzake.
Hii hadi leo imeendelea kuifanya Tanzania kuwa moja. Utani wa jadi ninaoufahamu mimi tangu enzi zile ni kwamba Yanga ikiifunga Simba, mashabiki wa timu hiyo wanakuwa na furaha isiyo kifani, wanawanunulia chakula, soda na vitu mbalimbali wale wa Simba, wanawapa wale huku wakiwazodia kwa maneno ya utano. Kule Kigoma wanawanyoa nywele kabisa na wanaonyolewa hawapingi.
Na wa Simba nao wanafanya hivyo hivyo, watawakirimu kwa kuwaninilia vinywaji na chakula, huku wakiwacharura wenzao. Unakuna, unapakiwa na maneno.
Hata kwenye misiba, klabu hizi mbili zimekuwa zikishirikiana, watu wanazikana, kwenye msiba wa watu wa Yanga, wa Simba wanashughulika na ule utani kama wa makabila unaendelea kama kawaida.
Kwenye miaka ya karibuni mashabiki wamegeuka kabisa. Badala ya kuwa utani imekuwa uhasama. Watu badala kutaniana wanatukanana na kuvunjiana heshima. Kwa kiasi kikubwa imeletwa na watu wanaoitwa au kujiita wasemaji kwenye miaka ya hivi karibuni.
Nimemsikia Afisa Habari mpya wa Yanga, Ali Kamwe, mara baada ya kuchaguliwa amesema ataondokana na aina hiyo ya usemaji, badala yake anataka kuendelea utani tu.
"Katiba ya Yanga ibara ya 39 inasema kazi ya Afisa Habari ni kufanya mawasiliano yote ya klabu na kuwajibika kwa Mtendaji Mkuu, kwa hiyo mimi nahakikisha kuwa nahusika na mawasiliano ya klabu kwenda kwa mashabiki na wanachama kupitia tasnia ya habari, hili suala la kucharurana ni utamaduni uliojengeka, tunaheshimu utani wa jadi ndiyo mpira wetu ilipo, utani wa hapa na pale unaweza kuwepo, lakini sidhani kama mimi naweza kufika hatua ya kumvunjia mtu heshima, kumdhihaki, kumtusi, mimi nimelelewa kwenye familia yenye kutunza maadili ya Mwafrika," anasema Kamwe.
Hili ni jambo la kupongezwa na kuungwa mkono si na Wanayanga wenzake, na Maafisa Habari wenzake, bali hata Watanzania wote.
Tuondokane na ushahibiki ambao umewaondoa Watanzania kuwa wamoja na kuwagawanya pande mbili. Wanajiona ni maadui zaidi kuliko watani wa jadi.
Nakumbuka mwanachama mmoja wa Simba aliyekuwa na rafiki zake wanachama wa Yanga, alikutana na mashabiki wawili ambao alitaniana nao sana, na baadaye alipowazoea, aliwapeleka kwa rafiki zake ambao ni wanachama wa Yanga ili wakapate kadi ya uanachama. Huu ndiyo utani wa jadi unaotakiwa.
Unatakiana na mtani wako, halafu baadaye unapata faida ya kupata kadi, kazi, kuoa, kuolewa, kusafiri na siyo kuishia kutukanana, kukashifiana, ambapo mwisho wake ni ugomvi na kupigana.
"Afanye kazi kwa bidii na kwa kujituma, aheshimu kila shabiki, ili mradi wa klabu yake, haijalishi amechoka kiasi gani, ili mradi wa klabu yakeMimi namfahamu Kamwe, ni kijana mwenye nidhamu
Tambo zitaendelea na ni muhimu, hatuwezi kuishi kama tuko msibani, lazima tuishi kwa tambo, Simba na Yanga ndiyo maisha yetu, mashabiki wetu ndiyo wanapenda maisha ya kutunishiana misuli, kuzodoana lakini siyo kwa kuvuka mipaka, zitaendelea ila safari hii zitakuwa za kitaalamu kidogo na siyo za kuropoka," alisema Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally kwenye salamu zake za pongezi kwa Kamwe.
Mashabiki wa soka wanachohitaji kwa maafisa hao, ni kuwaondoa kwenye uhasama uliopo na kuwarudisha kwenye utani wa jadi.