Ila ameanzia mbali kwa kuwataja mashabiki wa timu yake ya Simba kuwa wengi wamekuwa hawana tabia ya kwenda kuangalia mechi ambazo timu yao inacheza kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
"Nimefungua mjadala kwa nini watu hawaji uwanjani mechi za Dar. Nimepata majibu mengi, lakini sijaridhishwa nayo na nimeona ya kawaida tu ambayo hayaendani na uhalisia. Nimewasema mashabiki wa klabu yangu ya Simba, wakaniambia eti timu haicheze vizuri msimu huu ndiyo maana, hapana.
Kwanza mimi ninavyoona mashabiki hupenda timu yao kwa shida na raha, ndiyo maana utaona kwa wenzetu hata timu inataka kushuka daraja, lakini mashabiki bado wamejazana," alisema Ahmed.
Nimwongezee tu hapo, ni kwamba mashabiki nchi za nje hasa Ulaya, hata timu yao ikicheza mechi ya mwisho tena na timu kubwa wanajazana na wakifungwa mabao, dakika chache kabla mechi kumalizika wanatoa mabango ambayo naona wanakuwa wameyatayarisha kabla ya mechi wakikubali matokeo na kusema wanashukuru, lakini msimu ujao watarejea kwa kishindo, wakiendelea pia kushangilia. Hao ndiyo mashabiki mashujaa wafia timu.
Ahmed akawauliza, mbona hata wakati ule Simba ilipokuwa inacheza soka biriani, ile ya kina Clatous Chama, huku Meddie Kagere, kule Luis Miquissone bado mashabiki wa Simba Dar walionekana kuwa idadi ndogo wanaokwenda viwanjani kuliko hata wa Yanga ambao walikuwa 'tiamaji tiamaji?'
Ni kweli mashabiki wa Simba walionekana kujazana tu Dar pale timu yao ilipokuwa ikicheza mechi za kimataifa, Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.
Ingawa Ahmed ameitaja timu yake na inaonekana ni kama inazidiwa mashabiki na wenzao Yanga, lakini hata hao wanaozidi ni wachache. Kifupi tu ni kwamba mashabiki wa soka Dar hasa wa Klabu za Simba na Yanga uhudhuriaji wao uwanjani umekuwa wa mashaka.
Unaweza kusema sababu ya televisheni, wengi wao wanaangalia huko, lakini mikoani nako zipo, ila huko ndiko timu hizo zinapojaza mashabiki.
Sitaki kwenda mbali sana, nataka nieleze baadhi ya sababu ambazo kama wataalamu watafanya uchunguzi, basi wanaweza kuanzia hapo pia.
Kwanza kabisa tuelezane ukweli ni kwamba mifumo ya kielektroniki irekebishwe na iwe rafiki kwa mashabiki. Pia wengi hawana Ncard. Hapa tu peke yake unaweza kuona kuwa kuna baadhi ya watu wameachwa na wanapata changamoto sana kwenye hili na ndiyo maana utaona hata wanaoingia uwanjani mara nyingi ni wale wale tu. Wengine wakipata changamoto kidogo tu, wanakata tamaa.
Mikoani hakuna changamoto hizo kwa sababu wao nao wana mifumo yao ya kuingia.
Kingine ni kwamba mashabiki wa soka wanachukuliwa kama watu wanaokwenda kudowea chakula cha watu kwenye shughuli na si wateja.
Mara nyingi hawachukuliwi kama wateja, ndiyo maana wanaanza kukutana na changamoto tangu mlangoni, kuingia, hakuna mifumo rafiki ya kuingia, unaweza kudhani mtu anaingia gerezani. Hadi anaingia yupo hoi na amenusurika virungu, kuumwa na mbwa, kufukuzwa huku na huko.
Wanapokaa tatizo, usalama wao mdogo, na hata vyoo pia changamoto, kutoka nako ni tabu, unaweza kukuta geti moja tu limefunguliwa.
Mikoani wanaweza kuvumilia kwa sababu ya kuziona klabu hizo na wachezaji wake ni nadra sana, ndiyo maana wanajaa, lakini wa Dar es Salaam hawawezi kuvumilia hilo.
Huwa tunaona mashabiki wanapigwa mitama na maaskari, virungu, hii yote inasababisha mashabiki hasa Dar kuamua kubaki majumbani na kuangalia kwenye vibanda umiza au kwenye mabaa.
Usalama wa mashabiki mara tu wanapotoka viwanjani Dar nao ni mdogo na mara nyingi kumeripotiwa uporaji mita chache tu kutoka Uwanja wa Benjamin Mkapa, iweje kipindi hiki ambacho kumeripotiwa kuwa na Panya Road sehemu mbalimbali?
Kwa sasa asilimia 90 za mechi za Dar zinachezwa usiku, mji kwa sasa umepanuka sana, kuna watu wanaishi Boko, Kisemvule, Goba, Chanika na sehemu nyingi ambazo ni nje ya mji na wakifika huko, wanaingia tena ndani zaidi kwa usafiri wa bodaboda kwa gharama kubwa, lakini unaweza kukuta sehemu zingine kwa muda huo usiku hakuna usafiri tena, hivyo kuwaogopesha wengi kwenda viwanjani. Nadhani kuna baadhi ya mechi za ligi ziendelee kuchezwa jioni Benjamin Mkapa.
Sababu hizo, zingine na kuendelea kutowafanya Watazamaji kama wateja, pamoja na ndani ya uwanja kutokuwa na huduma zozote za kijamii ambazo zinaweza kuwavutia mashabiki, zinasababisha mashabiki wa soka kupungua.
Mjadala uendelee na uchunguzi ufanyike ili kujua sababu zingine zaidi ziunganishwe na hizi chache nilizoziainisha ili ufumbuzi upatikane kwani gharama kubwa zinatumika kuziendesha timu na uhudhuriaji viwanjani kwa wingi ni sehemu kubwa ya mapato.