Sababu ikijulikana, gonjwa la waamuzi nchini litatibika

24Sep 2022
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Sababu ikijulikana, gonjwa la waamuzi nchini litatibika

MJADALA uliopo kwa sasa mitaani na katika mitandao mbalimbali ya kijamii ni juu ya baadhi ya waamuzi kuboronga kwenye mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Hilo limesababisha Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara kuwapeleka kwenye Kamati ya Waamuzi, baadhi ya marefa na waamuzi wasaidizi kwa ajili ya kujadiliwa na ikiwezekana kupewa adhabu stahiki.

Waliopelekwa ni mwamuzi bora wa msimu uliopita, Ahmed Aragija na Amina Kyando, huku waamuzi wasaidizi ni Frank Komba, ambaye ni mwamuzi msaidizi bora nchini kwa misimu mitatu pamoja na Black Tubuke.

Mechi zinazohusishwa hapa ni Yanga dhidi ya Azam FC, Prisons dhidi ya Simba na Namungo dhidi ya Coastal Union.

Sitaki kueleza jinsi ilivyokuwa kwani mashabiki wengi wa soka wameona namna waamuzi hawa walivyochezesha, makosa waliyoyafanya na walivyofungiwa.

Labda kwa kuongezea tu naweza kusema Aragija yeye anapelekwa kwa kutomudu michezo yote miwili kati ya Yanga dhidi ya Azam na pia Prisons dhidi ya Simba, wakati Komba yeye alikuwa pamoja na Aragija kwenye mechi ya Yanga dhidi ya Azam. Anadaiwa kutomsaidia vyema mwamuzi wake.

Tubuke yeye alikuwa na Aragija kwenye mechi ya Prisons dhidi ya Simba, naye anadaiwa kumtomsaidia mwamuzi wa kati katika mechi hiyo.

Kwanza niseme hii si mara ya kwanza wala ajabu kwa waamuzi kupelekwa kwenye Kamati ya Waamuzi ili kuadhibiwa kwa makosa ya uwanjani.

Ilitokea na itaendelea kutokea kwa sababu kwenye mpira wa miguu, kama mchezaji anakosea, basi na waamuzi huwa wanakosea.

Hata hivyo, waamuzi wetu wa Kibongo jinsi wanavyokosea wanatia shaka. Kama alivyowahi kusema Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Almasi Kasongo mechi hiyo hiyo moja anaweza kumwonya mchezaji wa timu A kwenye kosa, lakini hilo hilo likifanywa na timu B anatoa kadi ya njano.

Ni kwamba makosa yao ya kibinadamu mara nyingi huzinufaisha zaidi timu kubwa, zenye mashabiki na uwezo kuliko ndogo.

Tulisikia hivi karibuni kuna waamuzi watatu tu ambao ndiyo wanaochezesha mechi za timu za Simba na Yanga. Yaani hawa wanazunguka nazo. Nao ni Aragija, Ramadhani Kayoko na Heri Sassi.

Pamoja na taarifa ya Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi, Nassor Hamdoun iliyotolewa ufafanuzi inatokana na sifa zao kwani ni waamuzi kwenye beji ya FIFA na pia ni wazoefu. Ni kweli haipingiki na wala hatukatai, lakini binafsi hili naona ni kosa kubwa.

Kuwepo kwa waamuzi hao hao wanazichezesha timu hizo hizo ni kutengeneza mianya ya rushwa.

Hili suala la rushwa mara nyingi wadau wengi wa michezo huwa wanalikwepa kulitaja hadharani kama halipo, lakini ukizisikia za 'chini ya kapeti' unabaki kupigwa butwaa.

Kwenye nyanja za soka inaonekana watu wanakwepesha sana kuhusu suala hili, lakini hebu angalia katika nyanja nyingine wanavyokuwa makini nalo.

Huwezi kukuta hakimu akikaa kwenye mahakama moja kwa muda mrefu, au askari polisi kuwapo kwenye kituo kimoja kwa miaka mingi.

Hii yote ni kwa sababu ya kukwepa watu hao kuzoeana sana na watu, kitu ambacho kitasababisha utendaji wao kubwa mgumu na hasa wakilenga rushwa. Sasa kama serikali tu inakuwa macho na watendaji wake muhimu hao, sembuse waamuzi kuchezesha timu mbili au tatu tu kila zinakokwenda?

Watoa rushwa watajua tu waamuzi wetu ni hao tu, hivyo ni rahisi 'kucheza nao.'

Inaonekana Shirikisho la Soka Nchini (TFF), na kamati zake za waamuzi wanatoa adhabu kwa waamuzi wanaovurunda, lakini hawatafuti kiini kwa nini wanafanya hivyo.  Kama ni hivyo wataendelea kuwafungia.

Binadamu anayeumwa ni lazima kwanza afahamu nini anaugua ndiyo aweze kujitibia.

Inavyoonekana hadi sasa Kamati wa Waamuzi haijajua tatizo ni nini, marefa hawajui kuchezesha, wana mapenzi kwa klabu, wanashindwa kutafsiri sheria kwa makusudi au rushwa, posho hazitoshi au mafunzo wanayotoa ni hafifu?

Nadhani hapa kwanza ndiyo inafaa waanze napo. Vipo vyombo vya kuchunguza, tena vya serikali. Kwanini wasianze kufanya uchunguzi wajue tatizo lipo wapi ili waje na ufumbuzi wa kudumu?

Ndiyo kwanza ligi ipo raundi ya nne, tayari fungiafungia imeanza, kwa hili inaweza kujikuta imefungia waamuzi wote.

Kuna kitu kinatakiwa kifanyiwe kazi ambacho kinakwepwa. Kama ni VAR basi mchakato uanze. Kama ni viashiria vya rushwa TAKUKURU ipo. Kama hawajui basi mafunzo yaongezeke.

Klabu zinazidi kuwekeza fedha kwa wachezaji na makocha, wadhamini wanamiminika na kuifanya ligi kuwa bora, sasa ni aibu kubwa waamuzi wake ndiyo chanzo cha kuondoa ubora na ushindani wa Ligi Kuu. Je imefika wakati sasa na waamuzi nao watoke nje ya nchi?