Wakati mwafaka dawa asilia kuchukua nafasi yake nchini

08Sep 2022
Yasmine Protace
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Wakati mwafaka dawa asilia kuchukua nafasi yake nchini

​​​​​​​TIBA asili ni hali ya kutumia mitishamba isiyokuwa na dawa kemikali na wakati huohuo, ni chakula cha kujenga mwili na viini vyake.

Kwa mujibu wa takwimu mbalimbali zilizopo, inaonyesha zinatoa mchango mkubwa kwa jamii katika upatikanaji wa matibabu salama kwa njia ya tiba asili.

Hadi sasa kuna hesabu inayotajwa ya dawa za asili 85 zilizosajiliwa tangu Septemba mwaka jana na Baraza la Tiba Asili. Pia, hivi karibuni serikali imeanza kutoa huduma jumuishi za tiba asili na tiba za kisasa nchini katika vituo vya Momela wilayani Meru mkoani Arusha na Maibong-SukiDar, Dar es Salaam.

Nikimrejea  Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Kusirye Ukio, katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Tiba Asili ya Mwafrika, alipomwakilisha Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu katika kilele cha maadhimisho hayo ambayo yalifanyika mkoani Morogoro, amenena mambo kadhaa ninayoyaona yana mashiko kitaifa.

Dk.Kusirye anasema, kuanzishwa huduma hizo ni mafanikio makubwa kwani tangu uhuru wa nchi, kuna huduma chanya ya kuboreshwa na kuendelezwa tiba asili.

"Miongoni mwa mafanikio mengine ni tiba asili kutambuliwa katika Sera ya Afya,kutungwa kwa sheria ya Tiba Asili/Mbadala,kanuni na miongozo mbalimbali pamoja na kuongezeka kwa tafiti za tiba asili zinazofanywa na vyuo vikuu vya serikali," anasema.

Anafafanua, mchango wa tiba asili umedhihirika zaidi wakati wa mapambano ya maradhi UVIKO-19 na kwamba viongozi wa Serikali za Kiafrika wanawajibika kuona umuhimu wa kuboresha tiba hiyo katika mapambano ya adui maradhi.

"Huduma za tiba asili zilitumika wakati wa UVIKO-19 na zilifanya kazi kubwa sana kuwahudumia wahitaji ambapo dawa takribani 21 za asili zilitumika, kutokana na hilo Watanzania wamekuwa na imani kubwa na huduma za tiba asili," ametamka.

Rai yake nchini katika suala la kuendeleza huduma za tiba asili, mojawapo inajikita kuwa sehemu ya vipaumbele kiserikali sasa.

Kwa upande mwingine, anavutia katika maono yake kwa Waganga wa Tiba Asili, kutengeneza dawa zenye ubora na kuhakikiwa na Mamlaka zinazotambulika ikiwa pamoja na Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.

Anaongeza kuhusu usalama wa dawa zao, zile zilizothibitishwa zina usalama kwa kiwango kinachokubalika na ndizo zinapaswa kusajiliwa.

Hapo akapiga hatua ya kuwataka waganga wa asilia kuacha kuchanganya dawa za kisasa kwenye dawa zinazotengenezwa na kuuzwa kwa wahitaji na kuongeza kuwa Wizara ya Afya, kwa kushirikiana na taasisi za utafiti na vyuo inaendelea kufuatilia dawa zote za tiba asili zilizopo sokoni.

Hapo kuna angalizo muhimu kwamba, dawa yoyote itakayokutwa imechanganywa na dawa za kisasa, hatua kali zitachukuliwa kwa mmiliki wa dawa husika.

Inavutia pale Mkurugenzi wa Uzamili na Utafiti kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Profesa Esron Karimuribo, anasema Tanzania ina mazao mazuri yanayofanya vizuri, yamethibitishwa ubora katika tiba na kuhakikiwa yanafanya vizuri.

Anaendeleza hoja zake za kisomi kwamba, kutolewe elimu kwa wataalamu wa tiba asili na kwa kuanza wamekuja na utaalamu wa vifungashio kwa dawa hizo, pamoja na utoaji dozi kamili ili kupata matokeo mazuri.

Hiyo nayo inaingia katika hesabu ya hatua zaidi kama taifa, tunajumuisha juhudi za tiba asili katika nyendo zetu kusaka afya sahihi.

Ni hoja inayojaziwa na kauli ya Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza la Tiba Asili/Mbadala, Elizabeth Lema, anayesema kutokana na kutatua changamoto za Baraza hilo, hivi sasa wamewakamata ‘vishoka’ na matapeli wanaopita kuwasajili waganga hao na hatua kali za kisheria zinachukuliwa dhidi yao.

Nikitanguliza pongezi  kwa lile la Lema,  anahimiza vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, kuacha matangazo yasiyo na vibali kutoka Baraza hilo na kwamba litaendelea kutoa elimu, ili kuwa na wigo mpana wa kutoa tiba za asili nchini.