...baada ya kufanya vibaya katika mechi za kusaka tiketi ya kucheza fainali za wachezaji wanaocheza Ligi za Ndani Afrika (CHAN).
Stars ilishindwa kufuzu CHAN baada ya kuchapwa jumla ya mabao 4-0, ikikubali bao 1-0 nyumbani na kufungwa mabao 3-0 ugenini nchini Uganda, dhidi ya wenyeji, The Cranes.
Si tu Taifa Stars ilifungwa, lakini pia kwenye mechi zote mbili haikucheza vizuri kitu ambacho kiliwafanya mashabiki wengi wa soka nchini kupaza sauti wakitaka kitu kifanyike kwa ajili ya kuisuka upya.
Moja kati ya vitu alivyovitaja vitafanyika ni serikali kuchukua jukumu la kumlipa kocha ili kupatikana kwa mwalimu mwenye uwezo mkubwa kama ilivyokuwa zamani.
"Jambo la kwanza ni makocha, lazima tuwe na makocha wazuri, tunataka makocha wenye ujuzi mkubwa na si wa kawaida. Zamani kulikuwa na makocha walikuwa wakifanya vizuri sana kwa sababu serikali ilikuwa inawagharamia, alisema waziri huyo.
Lingine alisema ametoa siku 14 kwa baadhi ya watu waliowapa kazi wamletee taarifa ili kujua wachezaji wazuri walipo na hakuna tena sababu ya kuwa na mchezaji kuwamo kwenye kikosi cha timu ya taifa ambaye hajitumi hata kama ana jina kubwa kiasi gani.
"Katika mambo tuliyoyagundua watu wetu ni wavivu, lakini pia watu wetu hawajitumi, kwa sababu katika michezo hii miwili iliyochezwa, utagundua tu watu wetu hawajitumi na sisi kama wizara tunaangalia ni hatua gani ambazo tunaweza kuchukua. Nimeagiza siku 14 waniletee taarifa ili tujue mchezaji gani yupo wapi, wale ambao tunaona hawafanyi vizuri, hakuna tena sababu ya kuwa na mchezaji hata kama ana jina kubwa kuwamo kwenye kikosi cha timu ya taifa."
Ukiangalia anayosema Mchengerwa, ni wazi kabisa kuna baadhi ya wachezaji walionyesha wanacheza mpira wa kawaida sana kwenye zile mechi mbili japo majina yao ni makubwa katika medani ya soka.
Utashangaa kuona mchezaji anayecheza vile kwenye kikosi cha timu ya taifa, ndiyo yule ambaye anajituma na kupambana akiwa katika klabu yake.
Kwa wachezaji wa wenzetu nje ya nchi, mchezaji kucheza kwenye timu ya taifa ni fahari, yupo tayari kuandika barua ya kuhama kama hapati namba kwenye timu kubwa, aende kucheza timu ndogo itakayompa nafasi ya kucheza kwa sababu tu ili achaguliwe kucheza katika kikosi cha taifa lake.
Huu unaitwa ni ukosefu wa uzalendo. Haiwezekani mchezaji anacheza hadi tone la mwisho la damu yake, lakini akiwa kwenye kikosi cha Stars anacheza kawaida sana ili tu kutimiza wajibu ili dakika 90 zimalizike.
Pamoja na kwamba udhaifu wa Stars ni matatizo mtambuka, lakini inashangaza kuona hata kuteua kikosi bado ni tatizo.
Mara nyingi kikosi huteuliwa kutokana na wachezaji waliofanya vyema kwa kipindi hicho. Lakini Stars inaweza kuchagua wachezaji ambao wapo siku zote hata kama kwenye klabu zao hawachezi, au viwango vyao vimepungua na wakiwa kwenye timu ya taifa hawajitumi.
Na kuna wachezaji ambao wanakuwa wamefanya vyema kwenye kipindi hicho, lakini hawachaguliwi. Hili linaifanya timu kudumaa kuwa na wachezaji ambao hawapambanii namba kwani wanajua wataitwa tu kutokana na ustaa wao na hata wakifika huko wanacheza pia kistaa.
Wakati mwingine mpaka mashabiki wapige kelele mchezaji fulani hajachaguliwa, ndipo achaguliwe.
Wachezaji wa Kitanzania nao wana tatizo la kutokuwa na mwendelezo. Leo atacheza hivi kesho vile. Hii nayo inawapa tabu sana makocha wa timu ya taifa kuchagua.
Bado kama nchi hatuna wachezaji angalau sita au saba hivi wa viwango vya juu wanaocheza nje ya nchi.
Wachezaji wetu wamebweteka nchini hadi wapo baadhi ya watu wanapigania kuwatengenezea kanuni ya kuwalinda kwa kupunguza wachezaji wa kigeni, wakati nao hawajafungiwa milango wanatakiwa watoke waende nje ya nchi kwa maslahi yao na timu ya taifa.
Pia namwomba waziri aangalie sasa uwezekano kwenda bungeni kupigania itungwe sheria ya uraia pacha angalau kwa wanamichezo tu, ili tupate Watanzania waliozaliwa nje au wenye uraia wa nchi mbili waitumikie Stars.
Kama nilivyosema matatizo ya Stars ni machache sana na ni mtambuka, kwa leo ni haya niliyoyabainisha na wanamichezo sasa tumuunge mkono Mchengerwa ili atekeleze majukumu yake vyema, hususan la kuifanyia mabadiliko timu ya taifa akishirikiana na Shirikisho la Soka Nchini (TFF).



.jpg?itok=nfwjwDzv)








