Wabunge hao wamekuwa wakitekeleza wajibu wao muhimu wa kupitisha bajeti ya serikali, kutunga sheria, kuishauri na kuisimamia serikali kwa niaba ya wananchi katika masuala mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya nchi na watu wake.
Hata hivyo, inawezekana kuna sehemu wabunge hao wameshindwa kutimiza wajibu wao na sasa wanakumbushwa kurudi kwenye mstari, ili waweze kuwakilisha wapigakura wao kikamilifu.
Hilo ni kutokana na kauli ya Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana ya kuwataka wabunge na madiwani kupitia chama hicho kuwa wakali katika kuisimamia serikali ili itekeleze ahadi za miradi ya maendeleo kwa wananchi.
Anatoa kauli hiyo hivi karibuni katika mikoa ya Kanda ya Ziwa kwamba kuna baadhi ya miradi ikiwamo ya maji, tiba, elimu na miundombinu ambayo inatengewa fedha, lakini zinaelekezwa sehemu nyingine.
Makamu Mwenyekiti Kinana akajipambanua kuwa ni miongoni mwa wale wanaopenda wabunge wawe wakali kidogo kuhusu mambo ya serikali, na kwamba sio wakali kwa maana ya kuisakama serikali bali kwa kuiwajibisha na kutoa mawazo mbadala ya kuboresha maisha na hali za wapigakura ambao ni Watanzania.
Katika ufafanuzi wake, anasema chama hicho ndicho kinachokwenda kwenye uchaguzi, kuomba kura, ndicho kitakachopewa viongozi au kitakachonyimwa na sio serikali, na akwamba watendaji na watumishi wa serikali wataendelea kuwapo, huku chama kikishindwa kutokoana na wao kutotimiza wajibu.
Jambo hili la wabunge kuishauri na kuisimamia serikali, lilishawahi kuzungumzwa na mara kwa mara wanakumbushwa kuwa waamke na kujenga hoja badala ya kuwa 'mabubu', ili kutekeleza wajibu wao kikatiba.
Kwa hiyo ndani ya bunge ndipo kunapelekwa bajeti ya serikali, kunatungwa sheria na mipango ya serikali, hivyo ni vyema wakatimiza wajibu wao kwa kuhakikisha zinatungwa sheria bora kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.
Akapigilia msumari kwa kusema, sio vyema kwa mbunge kujipendekeza ili aonekane ana nidhamu kwenye chama au serikali, kwa kuwa kufanya hivyo hatokuwa ametimiza wajibu wake wa kuwasemea wapigakura wake, Kinana anawakumbusha viongozi hao na wawakilishi wa wananchi.
Ninadhani hayo yaliyosemwa na viongozi yanatosha kuwaamsha wabunge na kuchukua hatua za kutimiza wajibu wao bungeni kwa ajili ya maendeleo ya wananchi na ustawi wa nchi.
Hadi kufikia kusema hadharani kuwa wabunge wawe wakali kidogo kwa serikali, inaonyesha kuna mahali hawajatimiza wajibu wao inavyotakiwa. Hivyo ingependeza kama watatafakari kauli hiyo na kuifanyia kazi.
Kimsingi, serikali inaongozwa na binadamu, inaweka bungeni jambo likiwa na mapungufu, hivyo ni wajibu wabunge kurekebisha penye mapungufu na si kulipitisha kama wajibu tu.
Hivyo, mjadala wenye lengo la kuboresha kwa faida ya wananchi ni suala muhimu na hali hiyo inaweza kuondoa dhana iliyojengeka miongoni mwa watu kuwa wabunge wamekuwa ni watu wa kukubali kila jambo.
Ninadhani jambo la muhimu kama anavyoshauri kiongozi wa chama Kinana, ni wabunge kuwa wakali kwa mambo ya wananchi, hasa wanapoona mambo yanakwenda ndivyo sivyo, kwa kujenga hoja zenye manufaa kwa umma.



.jpg?itok=nfwjwDzv)






