Wazazi, walezi msijisahau kukabili, kumaliza utoro

06Sep 2022
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Wazazi, walezi msijisahau kukabili, kumaliza utoro

ELIMU bora ni msingi mkuu wa maendeleo, kwani bila kujua kusoma, kuandika na kuhesabu pamoja na ufahamu wa mazingira yanayomzunguka mwanadamu, inakuwa vigumu kuanzia familia hadi taifa kusonga mbele.

Kwa kawaida elimu ya msingi ni muhimu, kwa ajili ya kumjengea mwanafunzi msingi imara ambao utamwandaa kikamilifu hatimaye aweze kuendelea na ngazi za juu zaidi.

Hata hivyo, baadhi ya jamii ina mtazamo hasi kuhusu umuhimu wa elimu ya msingi, hali inayochangia kuwafanya baadhi ya wanafunzi kuwa watoro bila kuwachukulia hatua na hatimaye kuiacha shule.

Ninaamini kuwa, watoto wasipojengewa msingi wa kupenda elimu kuanzia ngazi ya chini, inaweza kuwa vigumu kupenda shule, hivyo ipo haja kwa wazazi na walezi kuhamasisha umuhimu wa elimu kwa watoto wao.

Katika mazingira hayo ya kutokuwa na mwamko na elimu, wapo baadhi ya wanafunzi wanadaiwa kuhudhuria vipindi vya masomo shuleni mara mbili, tatu kwa wiki, hali hiyo isipodhibitiwa inazaa utoro na hata kuacha shule.

Huenda ingekuwa ni vyema sasa kuunga mkono juhudi za serikali za kudhibiti utoro ziungwe mkono ili wote wapate elimu bila kuwapo na visingizio vya kutohudhuria shuleni.

Miongoni mwa sababu zinazochangia utoro, kukatisha masomo zinatajwa kuwa ni umaskini wa kipato kwenye familia, mimba za utotoni, mwamko duni wa elimu kwa baadhi ya jamii.

Ili kukabiliana na utoro wa wanafunzi wanaotoka familia maskini, Juni mwaka huu Waziri wa Fedha alipendekeza kuanzishwa kwa dirisha maalum kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), litakalosaidia watoto wanaotoka kwenye familia maskini.

Waziri anapendekeza kuanza utaratibu huo kwa kuwekeza Shilingi bilioni nane, kwa ajili ya watoto wa familia maskini watakaopatikana kwenye kanzidata ya TASAF na taarifa za wabunge na madiwani.

Hatua hiyo inachukuliwa kuonyesha ni jinsi gani elimu inapaswa kupewa kipaumbele kikubwa kama msingi imara wa kufikia malengo ya kuwa na taifa lenye wasomi na siyo wanaokwepa shule kwa visingizio mbalimbali.

Kutokana na mkakati huo, ni wazi kwamba kila mmoja wetu anahusika katika kudhibiti vitendo vya utoro ikiwamo kuanzia nyumbani kwa wazazi na walimu pia ili wanafunzi wote wahudhuria masomo.

Wapo wanafunzi ambao wanaweza kusingizia kuwa wanaumwa na kutohudhuria vipindi shuleni, na wakati mwingine ni ujanja tu na pia wapo wanaoaga kwenda shule na kuishia njiani.

Lakini katika mazingira hayo, kuna haja ya kuwapo ushirikiano kati ya wazazi na walimu, ili kupeana taarifa za maendeleo ya mwanafunzi kama njia mojawapo ya kudhibiti vitendo vya utoro.

Ushirikiano huo kati ya wazazi na walimu ni mojawapo ya kudhibiti utoro, lakini iwapo wadau hao kila mmoja akidhani siyo wajibu wake kudhibiti vitendo hivyo, utoro utaendelea kuwapo nchini.

Serikali imeonyesha nia ya kutaka wanafunzi wote wapate elimu kwa kuondoa ada na pia imekuja na mkakati wa kusaidia familia maskini, hivyo ni wajibu wa wazazi na walezi kuhimiza watoto wao kupenda elimu. 

Hatua hiyo ingeenda sambamba na kuwapo kwa chakula shuleni, watoto wao wapate angalau uji asubuhi na mlo wa mchana ili kupunguza utoro, unaolezwa kuwa unachangiwa na ukosefu wa chakula shuleni.

Pamoja na hayo, ninadhani michezo, muziki na stadi za kazi vingepewa kipaumbele kama njia ya kuvutia wanafunzi kupenda shule, kwani navyo vina sehemu yake hasa kukuza vipaji.