Kipigo Stars kila mtu abebe lawama

05Sep 2022
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kipigo Stars kila mtu abebe lawama

SAFARI ya Tanzania kusaka tiketi ya kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji Wanaocheza Ligi za Ndani (CHAN), ilimalizika juzi kwenye Uwanja wa St Mary Chitende kwa kuchapwa mabao 3-0 dhidi ya timu ya Taifa ya Uganda, The Cranes.

Taifa Stars baada ya kufungwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Agosti 28, mwaka huu, juzi ilikubali tena kipigo cha 3-0 hivyo kutolewa kwa jumla ya mabao 4-0 na kuwaacha wenyeji wakifuzu fainali hizo zitakazofanyika mwakani nchini nchini Algeria.

Pamoja na kutimua benchi lake la ufundi lililokuwa likiongozwa na Kim Poulsen, bado haikuwa na ubavu dhidi ya kikosi cha Uganda Cranes licha ya kuwa na kocha mpya, Honour Janza na Msaidizi wake, Mecky Maxime.

Mara ya mwisho ilikuwa mwaka 2019 ilipokata tiketi ikiwa ugenini Uwanja wa Omdurman nchini Sudan ilipowafunga wenyeji mabao 2-1, licha ya kufungwa bao 1-0 nchini ikafuzu kwa bao la ugenini kutokana na matokeo ya jumla kuwa mabao 2-2, ikiwa chini ya kocha Mrundi Etienne Ndayiragije na kucheza fainali hizo zilizofanyika nchini Cameroon 2020.

Kila Mtanzania amekuwa na maoni tofauti juu ya kipigo hicho ambacho hakikutarajiwa. Inawezekana ikawa Stars ingeweza kutolewa, lakini kwa jumla ya mabao 4-0, hivyo kuzua mjadala mkubwa sehemu mbalimbali nchini, vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Awali ilipofungwa bao 1-0, ilikuwa rahisi tu kumnyooshea kidole kocha Poulsen, ikidaiwa yeye ndiye sababu kwani ameishiwa mbinu.

Na wengi walidhani hivyo, ikiwamo baadhi ya wachambuzi. Baada ya mabao 3-0 hali imebadilika, hivi sasa kama kawaida ya Watanzania kila mmoja anatafuta mtu wa kumbebesha lawama. Siyo Poulsen tena, kwa sababu hayupo. Nadhani kama asingetimuliwa, jumba bovu lingezidi kumwangukia yeye na ilikuwa ndiyo atimuwe, huku kila mmoja akimimina tatizo lilikuwa yeye.

Hii si mara ya kwanza kwa Stars kufungwa kwenye michuano mbalimbali ya kimataifa. Stars imekuwa ikifuzu AFCON na CHAN unaweza kusema kibahati zaidi kuliko uhalisia wenyewe.

Ndiyo maana haijawahi kufuzu kwa kuongoza kundi. Wapo wanaolilaumu Shirikisho la Soka nchini (TFF), kwa sababu zao wanazozijua, wengine wakilaumu kuwapo kwa wachezaji 12 wa kigeni kwenye Ligi Kuu kuwa eti ndiyo inasababisha kusiwe na wachezaji wenye uwezo Stars, lakini wapo wanaolaumu moja kwa moja wachezaji.

Binafsi nasema kuwa kutofanya vema kwa Stars kila Mtanzania anastahili kubeba lawama, kwa sababu kushindwa huko kunaanzia mbali sana.

Wanaosema ni kwa sababu ya kuwapo kwa ruhusa ya wachezaji 12 wa kigeni kwenye Ligi Kuu kwa kila timu, inafaa aulizwe kwa nini wachezaji wa Kitanzania wao hawaendi nje ya nchi, na ikichaguliwa wawe wanatoka huko, huku Ligi Kuu ya Tanzania kukiwa na wachezaji wachache?

Na kama ni CHAN ambayo ni ya wachezaji wa ndani tu, kwani ni lazima wote watoke Simba, Yanga au Azam ambao wana uwezo wa kusajili idadi hiyo ya wachezaji?

Mbona timu ya Taifa ya Uganda wachezaji waliotunyanyasa wao wengi wametoka kwenye klabu ndogo tu za Vipers,  Wakiso Giants, URA, KCCA, Proline,  BUL FC, Onduparaka, Arua Hill na mmoja tu kutoka klabu kubwa za Express na watatu tu SC Villa.

Wenzetu wanaangalia uwezo kwa wakati huo na si kukariri majina ya wachezaji wa klabu kubwa kama Express na SC Villa.

Hapa Tanzania wachezaji wanachaguliwa kisiasa zaidi kuliko uwezo. Wakati Uganda ikiwa na wachezaji ambao misimu michache iliyopita walicheza mechi za vijana chini ya miaka 17, Stars ilikuwa na John Bocco ambaye ana zaidi ya miaka 10 kwenye Ligi Kuu.

Na Bocco anachukuliwa kutokana na hawa wachezaji wetu vijana wanakuwa hawana mwendelezo wa viwango vyao. Wengi wanakuwa mastaa wa msimu mmoja au miwili tu, matokeo yake hadi leo tunakuwa na wachezaji wale wale tu.

Hapa kuna sehemu tunakosea, na tuanzie chini kabisa, kwenye kutengeneza vijana hakuna makocha sahihi kwani mpaka leo wanafundishwa kupokea pasi, malezi kutoka kwa baadhi ya wazazi, kutokuwa na viwanja vya michezo ambavyo vingi kwa sasa vimegeuzwa gereji baada ya kupigwa bei na mamlaka husika, pamoja na mtindo wa maisha ya kisasa kwa wachezaji wetu yanawafanya wawe na matatizo mengi.

Ukitaka kujua matatizo ya wachezaji wa Kitanzania wawe peke yao kwenye timu moja kama hivyo Stars, utagundua mengi tofauti wakichanganyika na wachezaji wa nje ya nchi ambao huwa wanawafichia makosa.

Hii inaonyesha kuwa tatizo la Stars ni mtambuka, halikuanza kufungwa leo au jana, kila mtu abebe mzigo wake. Hakuna wa kumlaumu mwenzake mpaka hapo, hadi Watanzania wote tutakapoanza kubadilika.