Si wengi walikuwa wanajua ni mchezaji mzuri, ingawa binafsi nilimwona akiwa na Timu ya Taifa ya Kenya (Harambee Starlets), iliyokuja nchini kushiriki mashindano ya Kombe la Chalenji ya Afrika Mashariki na Kati kwa wanawake yaliyofanyika mwaka 2019 na kufanikiwa kutwaa kombe hilo, mechi ya fainali wakiifunga Twiga Stars mabao 2-0.
Sikuwa na wasiwasi na uwezo wake, ingawa nilidhani angepata tabu kwenye mechi za mwanzo kama kawaida ya baadhi ya wachezaji ambao ni lazima kwanza azoee mazingira.
Kilichotokea ni kwamba hata kabla ya Ligi Kuu ya Wanawake ya Tanzania haijaanza, amefanya vyema kwenye michuano ya Afrika Mashariki na Kati kwa ngazi za klabu Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
Alicheza kama vile yupo katika kikosi cha Simba Queens kwa misimu kadhaa. Hata uchangamfu wake ndani na nje ya uwanja ilionekana kama ni mchezaji wa muda mrefu.
Katika michuano ya CECAFA , pamoja na kwamba ni kiungo mkabaji, alifunga mabao matano ambayo kwa kiasi kikubwa yaliiwezesha Simba Queens kutwaa ubingwa na kupata nafasi ya kuuwakilisha ukanda wake kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake itakayofanyika mwezi ujao nchini Morocco.
Kwenye mechi ya fainali dhidi ya She Corporate, pamoja na ugeni yake alichukua jukumu la kupiga mkwaju wa penalti.
Akajitoa muhanga licha ya kwamba kulikuwa na wachezaji wengi wazawa kama Oppa Clement, lakini pia wageni ambao wapo kwenye kikosi kwa muda mrefu kama vile Mrundi Joelle Bukuru.
Akaukwamisha mpira wavuni na lilikuwa bao pekee kwenye mchezo huo lililoifanya Simba Queens kutwaa ubingwa.
Corazone ambaye alianza soka akiwa na miaka tisa tu akiwa Mikongeni High School alikonga nyoyo za mashabiki wa Simba Queens kutokana na umahiri wake kwenye kukaba, akitumia urefu na nguvu alizonazo, akiwa pia na uwezo wa kumiliki mpira, na kupiga pasi ndefu kwa usahihi.
Kwenye vibanda umiza, baadhi ya mashabiki wa Simba, walisikika wakisema wangepata kiungo kama Corazone mwenye uwezo wa kukaba vile na kupiga pasi ndefu kwenda kwa mawinga na mastraika kwa haraka na usahihi kwenye timu ya wanaume, wangefurahi sana.
Baada ya sifa hizi, Corazone ana sifa nyingine ambayo ndiyo ingefaa sana kuwa somo kwa wachezaji wa soka la wanawake Tanzania. Nalo ni kuendelea kujiweka kama mtoto wa kike.
Pamoja na umahiri wote, kiasi cha kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa michuano, Corazone ni mrembo hasa. Amebaki kuwa mwanamke halisi. Ukimwona nje ya uwanja unaweza kukataa kama ni mcheza soka.
Hii inaondoa dhana ya wachezaji wengi wa soka la wanawake hasa Tanzania kuwa ni lazima wajiweke kama wanaume ndiyo ucheze kandanda.
Labda ukiendelea kuonekana kama mtoto wa kike huwezi kuwa na nguvu na uwezo wa kucheza, hii si kweli.
Corazone amethibitisha msichana anaweza kucheza kwa kiwango cha hali ya juu, lakini akiendelea kubakia na haiba ile ile ya kike.
Wakati soka la wanawake likianza na hata leo hii, baadhi ya wachezaji wamekuwa wakijiweka kama wanaume kuanzia uvaaji, unyoaji, mapozi na hata utembeaji, hii si sahihi, haifai na umefika wakati nyota hao wabadilike.
Hii imewafanya wazazi wengi kukataa au kuwapiga marufuku watoto wao wa kike kujiingiza kwenye soka kwa kuogopa watapotea.
Wanaona kuna maisha baada ya soka, hivyo wakianza kuwa na haiba ya kiume inaweza kuwaletea matatizo mbele ya safari ya maisha yao.
Angalau kwa miaka ya hivi karibuni baadhi ya wachezaji wameanza kujirekebisha, lakini kuna waliodhani wachezaji wanaojiweka kike zaidi wanakuwa na uwezo wa kawaida tu, hawawezi kuwa mastaa zaidi kwa jinsia yao huku wengine wanaojiweka kama wanaume.
Kiungo huyo wa Kenya ameondoa dhana hiyo kwa wachezaji aliokuwa nao, kwani nimeona hata baadhi ya wenzake kwenye timu wameanza kumuiga.
Nadhani hata wachezaji wengine wa klabu za Ligi Kuu ya Wanawake , Corazone anaweza kuwa kioo kwao, kwa kuthibitisha unaweza kucheza soka huku ukiendelea kuwa mrembo.
Amewafanya mpaka baadhi ya wazazi ambao walikuwa wakimshuhudia kwenye televisheni shughuli aliyokuwa akiifanya uwanjani, licha ya urembo wake kulegeza kamba na kuwaruhusu watoto wao wa kike kuingia kwenye soka, lakini wabaki kama Corazone kwa sababu kumbe inawezekana.



.jpg?itok=nfwjwDzv)








