Katika mchezo wa kwanza uliochezwa Jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es Salaam na kusimamiwa na waamuzi kutoka Sudan Kusini, Taifa Stars ilifungwa bao 1-0.
Baada ya kumalizika kwa mchezo huo, siku iliyofuata Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lilitangaza kuachana na aliyekuwa Kocha Mkuu, Kim Poulsen, na mikoba yake kumkabidhi Mzambia, Honour Janza na nahodha wa zamani wa kikosi hicho, Mecky Maxime.
Janza na Maxime waliongoza kikosi hicho juzi na kikubwa walieleza wanakwenda huko kupambana na kuhakikisha wanapata matokeo chanya na hatimaye wanasonga mbele kwenye michuano hiyo inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Nipashe, tunawakumbusha viongozi wa TFF, benchi la ufundi, wachezaji na wadau waamini kazi bado haijamalizika na si kwa Tanzania ambayo iko nyuma, hata kwa Waganda ambao wako mbele kwa goli moja.
Janza na kikosi chake wanatakiwa kufahamu wamekwenda Uganda kupeperusha bendera ya nchi, hivyo kila mmoja anawajibu wa kutimiza majukumu yake kwa kiwango cha juu ili kufikia mafanikio na malengo ambayo yanatarajiwa.
Wachezaji wa Taifa Stars wanatakiwa wasifikirie matokeo ya mechi iliyotangulia na badala yake wajikite kupambana kusaka ushindi katika mchezo ulioko mbele yao kwa kuamini wako katika fainali na matokeo wanayoyahitaji ni ya ushindi tu na si vinginevyo.
Kwa kuweka mawazo katika mchezo huo, itawasaidia kupata nguvu kwa sababu hakuna kisichowezekana, kama Waganda walipata ushindi katika dakika 90 za kwanza, basi inawezekana nao wakapata matokeo chanya kwenye dakika kama hizo zilizobakia.
Kama timu hiyo ikiwa na Juma Kaseja langoni mwaka 2019, Kocha Mrundi, Etienne Ndayiragije, ilifanikiwa kuwachapa Sudan mabao 2-0 wakiwa kwao Khartoum na kufuzu fainali za CHAN, ikumbukwe Stars ilifungwa goli 1-0 hapa nyumbani, pia mwaka huu inawezekana ikarudia rekodi hiyo na kubakia kwenye mashindano.
Kuongeza juhudi na umakini, kufuata maelekezo ya benchi la ufundi na kutokubali wenyeji wamiliki mpira kwa kiasi kikubwa, ni mambo ambayo yataisaidia Stars kuvuka kwenye mtihani ambao uko mbele yao.
Mbali na wachezaji kuipa nchi matokeo chanya, wakumbuke mashindano hayo ni daraja la kutangaza vipaji vyao kwa mawakala mbalimbali wanaofuatilia michuano hiyo ambao wanasaka nyota wa kuwapeleka kwenye klabu mbalimbali za Ulaya.
Sifa ya kwanza ya mchezaji kupata klabu kwenye mataifa ya Ulaya ni kuonekana katika kikosi cha nchi yako, sasa kama mchezaji atakayepata nafasi na akajituma, huyo atakuwa amejiandalia 'tiketi' ya kufuatwa na mawakala na kuwafanya watimize ndoto zao za kucheza soka la kulipwa kwenye mataifa hayo yaliyoendelea.
Mbali na kufikiria kupata timu nje, lakini mechi hizi za mashindano ya CHAN, ni nafasi nyingine muhimu kwa wachezaji ambao walikuwa wanakosa namba kwenye kikosi cha Stars kinachoshiriki mashindano mengine, kulishawishi benchi la ufundi na hatimaye kuingia kwenye 'first eleven' ya Tanzania.
Tunawakumbusha mashabiki na wadau wa soka walioko sehemu mbalimbali kwamba huu ni wakati wa kuungana na timu hiyo kuiombea dua njema ili ifikie malengo na si muda wa kutafuta 'mchawi' huku wapinzani wetu wakiendelea kuungana.
Tunafahamu vyema umoja na ushirikiano huzaa matunda, tunawakumbusha mashabiki ambao watapata nafasi ya kwenda Kampala kuwashangilia, wafanye hivyo kwa sababu itawaongezea nguvu wachezaji wetu na kujiona wanawajibu wa kupambana hadi kwenye tone la mwisho.









