Majaji wanawake waonyeshe kuwa wanaweza kwa vitendo

30Aug 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Majaji wanawake waonyeshe kuwa wanaweza kwa vitendo

RAIS Samia Suluhu Hassan, jana aliwaapisha majaji 21 wa Mahakama Kuu ya Tanzania aliowateua hivi karibuni ili kuongeza kasi ya utendaji na ufanisi wa mhimili huo wa dola ambao umekuwa ukilalamikiwa kwa kuchelewesha mashauri, hivyo wananchi kukosa haki pamoja na kutumia gharama kubwa hadi kumalizika.

Uteuzi wa majaji hao ni mwendelezo wa kuhakikisha mhimili huo unafanya kazi zake kwa weledi na pia majaji kupunguziwa mzigo wa kesi ambazo zimerundikana kwa muda mrefu. Tangu aingie madarakani miezi 17 iliyopita, Rais ameteua majaji 43 hatua ambayo imeongeza ufanisi katika Mahakama Kuu na ile ya rufani ambayo ni ya juu kabisa katika kutafsiri sheria na kutoa uamuzi katika kesi mbalimbali za jinai na madai.

Miongoni mwa majaji walioteuliwa na Rais wamo wanawake 23. Hatua hiyo imemwezesha mhimili wa Mahakama kufikisha asilimia 37 ya majaji wanawake, hivyo kuifanya Tanzania kupiga hatua katika azma ya kufikia usawa wa kijinsia wa asilimia 50 kwa 50 kwa mujibu wa makubaliano na mikataba mbalimbali ya kimataifa kuhusu usawa wa kijinsia kwenye ngazi za uamuzi, zikiwamo za siasa, uongozi na utendaji kitaasisi.

Katika hafla hiyo, Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma, alibainisha kwamba ongezeko la majaji katika ngazi hizo, limepunguza malalamiko yaliyokuwa yakitolewa dhidi ya mhimili huo.

Kwa hatua hiyo, Rais anastahili pongezi katika uteuzi mbalimbali anaoufanya, si kwa majaji tu bali hata kwa viongozi wa wizara na taasisi mbalimbali za serikali wakiwamo mawaziri na manaibu wao, wakuu wa mikoa, wilaya na makatibu tawala wa mikoa na wilaya. Kila anapoteua, kumekuwa na idadi ya kuridhisha ya wanawake lengo likiwa kuelekea usawa wa 50 kwa hamsini wa kijinsia kwenye ngazi za uamuzi.

Pamoja na kuteuliwa wanawake wengi, suala hapa si kuangalia idadi pekee bali utendaji wenye viwango na weledi vinatakiwa ili kumhakikishia Rais kwamba hakufanya makosa kuwateua katika nafasi hizo. Msemo kwamba wanawake wakiwezeshwa wanaweza, udhihirike katika utendaji wenye kasi, viwango na weledi.

Katika miaka kadhaa iliyopita, kuliibuka malalamiko kuwa baadhi ya majaji wanaoteuliwa, wakiwamo wanawake, walikuwa hawaandiki huku hatua iliyosababisha wananchi waliokuwa na mashauri mahakamani kukosa haki.

Licha ya kulalamikiwa kuhusu kutoandika hukumu kwa mwaka mmoja au zaidi, pia kulikuwa na tuhuma za rushwa dhidi ya baadhi ya majaji kuwa walikuwa wakiandika hukumu mbili katika kesi moja kuangalia nani atatoa dau kubwa ili ampendelee kwa kumpa ushindi.

Ni vyema majaji wapya wanawake wanapoanza kazi hiyo yenye heshima kubwa katika jamii, ni vyema wakazingatia viapo vyao na kufanya kazi kwa misingi ya kitaaluma bila kuwa na upendeleo wala huba kwa upande wowote kwenye kesi husika. Kwa maneno mengine, wanatakiwa kufuata misingi ya sheria na taratibu zinazowaongoza katika kusikiliza hoja zinazotolewa na hatimaye kutoa hukumu stahili.

Ni dhahiri kwamba kwa kufanya hivyo, wataonyesha imani kubwa kwa wananchi pamoja na Rais ambaye amewaamini kushika nyadhifa hizo pamoja na vyombo vilivyofanya uchunguzi hadi kupatikana kwao kwamba wanafaa kuwa majaji. Ni wazi kwamba kulikuwa na majina mengi yaliyopendekezwa kuwa majaji na hatimaye kupatikana watu 21 ambao Rais aliridhia na kuwateua.

Mbali na kufanya kazi kwa weledi, majaji hao wanawake wanapaswa kufuata miiko na desturi kwa ajili ya kuonyesha kwamba nafasi hizo ni za heshima, hivyo kila wanalofanya mahali popote, kikazi au maisha binafsi, waonyeshe heshima na nidhamu ya hali ya juu.

Mwisho, majaji hao wanawake wanapaswa kuonyesha kuwa Rais hakuwapendelea katika kuwateua, hivyo waonyeshe uwezo katika majukumu yao mapya ili aendelee kuwa na imani nao na hatimaye kuteua wanawake zaidi. Kwa mantiki hiyo, wasimwangushe Rais bali waonyeshe kuwa wanaweza.