Hatua madhubuti zichukuliwe kupunguza ajali za barabarani

10Aug 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Hatua madhubuti zichukuliwe kupunguza ajali za barabarani

WIMBI la ajali za barabarani nchini limeendelea kuongezeka katika maeneo mbalimbali huku watu kadhaa wakipoteza maisha na wengine kujeruhiwa na kupata ulemavu wa kudumu.

Matukio hayo ya ajali yamekuwa kama jambo la kawaida kutokana na vyombo vya habari na vyombo vya usalama hususan polisi, kuripoti mara kwa mara. Mfano, jana watu 20 walifariki dunia na wengine 15 kujeruhiwa katika ajali iliyohusisha magari mawili na trekta katika eneo la Mwakata, Msalala, Kahama mkoani Shinyanga barabara itokayo mji mdogo wa Isaka kwenda Kahama.

 

Ajali hiyo iliyotokea usiku wa kuamkia jana, ilihusisha gari aina ya Toyota IST lenye namba za usajili T 880 DUE, Hiace, T 350 BDX na lori aina ya Scania T 658 DUW, baada ya kugongana uso kwa uso.

 

Tukio hilo ni mwendelezo wa ajali zinazoendelea kutokea na kusababisha watu kupoteza maisha huku ndani ya mwaka huu pekee, kumekuwa na ajali kadhaa ambazo zimegharimu maisha ya watu.

 

Ndani ya kipindi cha takriban mwezi mmoja, kuna ajali kadhaa zimetokea ikiwamo ile ya mkoani Mtwara iliyosababisha watu 13 wakiwamo wanafunzi wanane kufariki dunia papo hapo na wengine majeruhi wakiendelea kupatiwa matibabu. Julai 12, mwaka huu,  pia watu wanane wakiwamo watano wa familia moja walipoteza maisha katika ajali iliyotokea Nyakahuri, Biharamulo mkoani Kagera baada ya gari walilokuwamo kugongana uso kwa uso na lori la mizigo.

 

Aidha, mwanzoni mwa Julai, mwaka huu, watu watano walipoteza maisha katika ajali iliyosababishwa na lori lenye shehena ya mahindi kufeli breki na kugonga basi dogo la abiria aina ya Toyota Coaster kwenye mteremko mkali wa barabara kuu ya Mbeya- Dar es Salaam.

 

Hizo ni ajali chache kati ya nyingi zilizotokea mwaka huu lakini Februari 14, mwaka huu, watu watano wakiwamo watatu wa familia moja, walifariki dunia eneo la Tura, Uyui mkoani Tabora. Ajali hiyo ilisababishwa na lori la mizigo na gari dogo aina ya Toyota RAV 4 lililokuwa likitoka Tabora kwenda Dar es Salaam.

 

Kama vile haitoshi, Machi 27, mwaka huu, watu saba walifariki dunia na wengine wanane kujeruhiwa baada ya lori la mizigo kugonga Bajaj katika eneo la Kidulya nje kidogo ya mji wa Bariadi mkoani Simiyu.

 

Sababu za kutokea kwa ajali hizo karibu zinafanana. Katika ajali ya jana, kwa mfano, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi (ACP) Leonard Nyandahu, alisema chanzo ni uzembe wa madereva wote ambao hawakuchukua tahadhari wakiwa katika vyombo hivyo.

 

Kamanda huyo alibainisha kuwa katika tukio hilo, kulitokea ajali mbili tofauti, ya kwanza ilihusisha trekta lililokuwa limesimama pembezoni mwa barabara bila kuwapo kwa viashiria kuonyesha kusimama, hivyo kusababisha Toyota IST kugonga kwa nyuma na kupata majeruhi.

 

Ajali ya pili, alisema ilihusisha Toyota Hiace iliyokuwa ikitokea Kahama kwenda Tinde wilayani Shinyanga, baada ya kugongana uso kwa uso na lori wakati ikijaribu kukwepa IST na trekta. Mbali na sababu za ajali ya jana, katika matukio ya nyuma imekuwa ikielezwa kuwa vyanzo vya ajali ni uzembe wa madereva, breki kufeli na mwendokasi wa madereva.

 

Kwa ujumla, ajali hizi sasa zimekithiri, hivyo hatua kali na za makusudi zinatakiwa kuchukuliwa ili kudhibiti ongezeko na kupotea kwa nguvu kazi ya taifa ambayo imekuwa ikiteketea kila uchao.

 

Jambo moja kubwa linalotakiwa kuchukuliwa ni udhibiti wa vyombo vya moto viwapo barabarani na kwa kuanza kabisa kukagua magari yote pamoja na kutoa elimu ya usalama barabarani.